Mafanikio yoyote yana sababu (36)

Na Padri Dk. Faustin Kamugisha

Kufanya mambo upesi yaliyo muhimu ni
sababu ya mafanikio. “Kuahirisha jambo
rahisi unalifanya liwe jambo gumu na
kuahirisha jambo gumu kunalifanya liwe
lisilowezekana,

” alisema George Horace
Lorimer. Kama mama wa uvumbuzi ni
ulazima, mjomba wa mafanikio ni uharaka
au wepesi.
Tatizo ni kufikiria kuwa una muda mwingi au
una miaka 1,000 ya kuishi hapa duniani.
Ngozi ivute ili maji. Udongo upatilize uli
maji. Methali hizi huambiwa mtu
anayesitasita kutenda linalostahili kutenda
sasa. Tenda sasa wakati una nguvu.
Tenda sasa wakati fursa imejitokeza.
Zamani kuna kanuni ya msituni ilisema
mwenye nguvu mpishe au msaliaji ni

mwenye nguvu. Siku hizi ni anayefanya
mambo upesi sana mpishe au msaliaji ni
mtenda mambo upesi sana.
Usingoje dakika ya mwisho kufanya
mambo. “Kesho ni kisingizio cha wavivu na
kimbilio la wasioweza,

” alisema Norbert
Quayle. Suala la uharaka wa kufanya kazi
linasisitizwa katika Injili ya Yohana: “Lazima
tufanye kazi za yule aliyenituma kukiwa
bado mchana; usiku unakuja ambapo
hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi.”
(Yohana 9:4).
Kama kuna mlima wa kupanda usifikiri
kusitasita kutageuza mlima huo kuwa
kichuguu.
Katika kikao cha viongozi wa kampuni fulani
meneja mauzo alisema: “Naona tatizo
kubwa sana katika kampuni yetu ni
kusitasita.” Mwenyekiti wa kikao juu ya hilo
alisema hivi: “Jambo hilo tusiliongee sasa
hivi. Tutalitafutia mahali pake wakati ujao.”
Katika maneno ya mwenyekiti tunaona
kusitasita.
Hakuna jambo la pekee linalomjia mtu
anayesitasita isipokuwa uzee. Uzito wa

kufanya mambo au hali ya kuchelewa
inaitwa uzohali. Tenda kwa uharaka.
Kusitasita hakuna sifa nzuri. Kusitasita
kunaua fursa. Kusitasita kunaua motisha.
Kusitasita ni mwizi wa muda. Kusitasita ni
kutoazimia kufanya lolote. “Ahirisha tu
mpaka kesho lile ambalo uko tayari kufa bila
kulifanya,

” alisema Pablo Picasso.

Kusitasita si matokeo ya kukosa muda wa
kumaliza kazi fulani, bali ni mtazamo ambao
lazima ubadilishwe. Barabara ielekeayo
mahali panapoitwa ‘Kushindwa’
imetengenezwa kwa mawe ya maazimio
yaliyoahirishwa. “Usikubali hofu ya kupoteza
kuwa kubwa sana kuzidi furaha ya
kushinda,

” alisema Robert Kiyosaki.

Kuna maneno yanayokwamisha mafanikio:
labda, ningejua, wiki ijayo, baadaye, siwezi
na bahati. “Neno linaloharibu maisha zaidi
ya maneno yote ni kesho,

” alisema Robert

Kiyosaki.
Alizidi kufafanua: “Tatizo na kesho ni
kwamba sijawahi kuiona kesho. Kesho
haipo. Kesho ipo katika akili za waota ndoto
na washinde.” Nakubaliana na Rais wa

zamani wa Marekani, Abraham Lincoln,
aliyesema: “Huwezi kukwepa wajibu wa
kesho kwa kuukwepa leo.”
Akizungumza juu ya jamii yake, Mwamerika
Brian Tracy, alisema: “Watu asilimia mbili
katika jamii yetu wana moyo wa uharaka.
Hawa ni watu ambao hatimaye wanapanda
daraja la juu kwenye taasisi. Unapojijengea
sifa ya kasi na kutegemewa katika kila kitu
unachokifanya, unajivutia fursa zaidi na
zaidi ya kufanya zaidi na zaidi mambo ya
umuhimu zaidi na umuhimu zaidi.”
Tujifunze katika maneno haya kujijengea
sifa ya kasi na uharaka katika kufanya
mambo bila kuathiri vibaya ubora. Kuna
hadithi juu ya shetani ambaye wakati fulani
aliamua kuangamiza dunia. Aliwaalika
mapepo kumpa mawazo.
Pepo Hasira alitoa wazo kuwa atafanya
ndugu wakasirikiane na watajiangamiza.
Pepo Tamaa ya Mwili alisema kuwa
ataangamiza dunia kupitia tamaa ya mwili.
Watu wataishi kama wanyama kwa kufanya
upendo wa kweli utoweke.
Pepo Uchoyo alitoa wazo kuwa

ataangamiza dunia kupitia uchoyo. Tamaa
ya mali, ubinafsi na kujipendelea. Pepo
Ulevi alitoa wazo kuwa ataangamiza dunia
kupitia kunywa pombe kupindukia. Shetani
hakuridhika na mbinu hizi. Msaidizi wa
Shetani ambaye alitoa jibu la kuridhisha
aliitwa Pepo Kusitasita.
Alisema: “Nitawaambia watu wawe na ndoto
ya kufanikiwa. Nitawatia moyo wawe na
malengo mazuri na mipango mizuri. Lakini
nitawaambia wasiwe na haraka ya
kuyafanyia kazi. Nitawaambia haraka
haraka haina baraka.”
Shetani alikubaliana na mawazo ya Pepo
Kusitasita. Mkakati wa kutofanikiwa ni
kusitasita. Ili ufanikiwe kuwa na uharaka wa
kufanya mambo bila kushusha ubora.

Mwisho