Zaidi ya wakazi 300 wa Mtaa wa Bunju ‘B’ jijini Dar es Salaam wamo katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko baada ya vyoo na nyumba zao kuzingirwa na maji yaliyotokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Bunju ‘B’, Salama Ali, akimwonyesha mwandishi eneo ambalo nyumba zake zimezingirwa maji ya mvua kutokana na kuziba kwa mifereji katika barabara za eneo hilo. (Picha na Aziza Nangwa).

Akizungumza na JAMHURI, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Bunju ‘B’, Salama Ali, amesema wamekuwa  wakiishi kwa shida sana tangu mvua zianze kunyesha Dar es Salaam kutokana na nyumba zao na vyoo kujaa maji.

Amesema hii si mara ya kwanza eneo hilo kujaa maji kila mvua zinaponyesha na jitihada zao za kutaka hali hiyo irekebishwe hazijazaa matunda.

Amesema hali hiyo inatokana na miundombinu hafifu katika eneo hilo ambayo haina uwezo wa kuhimili kasi ya mvua inaponyesha.

Wakazi hao wanamlaumu mkandarasi anayefanya kazi ya ujenzi wa barabara inayoelekea Mabwepande na barabara ya akiba ya Bunju ‘B’.

Wamedai kuwa mvua inaponyesha maji yanashindwa kufuata mikondo yake asilia kwa sababu mjenzi huyo wa barabara hakujenga mitaro ya kuongoza maji kama inavyotakiwa.

“Hakuna mtaro wa kupitisha maji na mvua inaponyesha maji yote yanatiririka kuelekea kwenye makazi ya watu. Kama unavyoona eneo lote hili limejaa maji, nyumba na vyoo vimezingirwa na maji na watu wamelazimika kuzikimbia nyumba zao,” anafafanua Ali wakati akimwonyesha mwandishi athari za mafuriko hayo.

Amesema kila mvua inaponyesha maji hutuama kwa muda mrefu katika eneo hilo na kuwa mazalia ya mbu na wadudu wengine ambao wanasababisha kukua kwa maambukizo ya maradhi mbalimbali kama vile malaria.

“Maji ya chooni nayo yanachanganyika na maji ya mvua na kusambaa eneo lote hili, ni hatari sana,” anabainisha.

Amesema watoto wadogo wapo kwenye hatari zaidi kwani wengi wao hucheza kwenye maji hayo kwa sababu hawajui madhara yake.

“Wale waliolazimika kubaki katika nyumba zao huishi kwa shida kwa sababu ndani kote kuna maji, inabidi uweke matofali ili kuinua vifaa visiharibiwe na maji,” amesema.

Amesema kwa muda mrefu wamefikisha malalamiko yao kwa diwani, mbunge na mwenyekiti wa serikali ya mtaa, lakini hakuna lolote lililofanyika kurekebisha hali hiyo.

Amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutembelea eneo hilo na kusikiliza changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Sophia Hamisi, amesema analazimika kuwabeba watoto wake kila siku asubuhi kuwapeleka shuleni ili kuwakinga wasikanyage maji hayo na kupata maradhi.

Goodluck Kabage, Ofisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa Bunju ‘B’, amesema kuwa tatizo lililopo la majumba na vyoo kujaa maji ni kubwa na limedumu kwa muda mrefu.

“Tumelalamika sana kuhusu tatizo hili lakini hakuna kiongozi wa juu ambaye ameonyesha nia ya kulishughulikia,” amesema.

Kabage amesema kuwa ofisa Mipango Miji aliwahi kufika katika eneo hilo na akashauri baadhi ya nyumba zibomolewe ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kupitisha maji lakini hilo lilishindikana.

Amesema ujenzi wa mitaro ya maji ndiyo Suluhu, lakini iwapo hilo litafanyika wananchi wanaitaka serikali iwalipe fidia wale ambao nyumba zao zitabomolewa.

370 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!