Sakata la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu limechukua sura mpya baada ya wapinzani kumtaka Waziri wa Tamisemi, Selemen Jafo, kujiuzulu kutokana na ofisi yake kuvuga uchaguzi huo.

Kuondolewa kwa zaidi ya asilimia 90 ya wagombea wa upinzani kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kasoro wakati wa ujazaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea kumesababisha vyama kadhaa vya upinzani kujitoa katika uchaguzi huo na kusababisha kuibuka kwa mtanziko wa kisiasa nchini.

Takriban vyama saba vya upinzani vimesema havitashiriki uchaguzi huo kwa sababu umevurugwa makusudi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) chini ya Waziri Jafo.

Wapinzani wanaeleza kuwa Tamisemi wanatakiwa kubeba lawama zote kuhusiana na kile kinachotokea kuhusiana na uchaguzi huo, huku viongozi wa Chadema kupitia Baraza la Vijana (BAVICHA) wakimtaka Waziri Jafo kuachia ngazi kama sehemu ya kuonyesha uwajibikaji.

Lakini wakati wapinzani wakitangaza kujitoa, kwa upande wake Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetamba kuingia kwenye uchaguzi huo huku kikiwa tayari kimekwisha kujihakikishia ushindi wa asilimia 51 baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa katika vijiji 6,248.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni ameipongeza serikali kwa msimamo wake wa kukataa kuyumbishwa na vyama vya siasa vilivyotangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo.

Katika mkutano huo Polepole alisema CCM itashiriki katika uchaguzi huo kwani serikali za mitaa ndio msingi wa kitaasisi wa kupanga maendeleo ya wananchi. Alibainisha kuwa CCM imeweka msingi mzito katika uchaguzi huo na imeweka nguvu ili kulinda watu wake katika msingi wa maendeleo.

“Uchaguzi huu si mchezo wa kombolela, CCM haifanyi mchezo huo bali imejipanga,” amesema Polepole.

Amesema ushindi ambao CCM itaupata katika uchaguzi huo unatokana na maandalizi ya kutosha waliyoyafanya huku akiwananga wapinzani kwa kufanya mzaha wakati wa mchakato wa utungaji wa kanuni za uchaguzi huo.

“Wenzetu wameweka mpira kwapani, wameamua kukimbia nao. Tuwaulize wakati hizi sheria za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinatungwa wao walikuwa wapi?” amehoji Polepole.

Pia ametoa rai kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuvichunguza vyama vya upinzani kama vilikuwa na michakato ya uchaguzi ndani ya vyama vyao.

Amesema ikibainika kuwa vyama hivyo havikuwa na michakato hiyo, yatakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma, kwa sababu vyama hivyo vinapata fedha kupitia ruzuku, kwa hiyo vinapaswa kusimama kama taasisi za umma.

Amedokeza kuwa CCM itakuwa na viongozi 24 wa kitaifa (hakutaja majina yao), watakaosimamia mchakato mzima wa uchaguzi katika chama chao na kuhakikisha kinapata ushindi.

Lakini Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrick ole Sosopi, amesema kutokana na uchaguzi huo kugubikwa na kasoro nyingi, ni vema Rais John Magufuli atoke na kuwaeleza wananchi nini kinatakiwa kifanyike. Amesema asipotoa tamko kuhusu uchaguzi huo atakuwa hapendi amani ya nchi.

“Sisi kama baraza tunataka Waziri Jafo awajibike kwa sababu mpaka sasa yeye na Tamisemi hakuna kazi ambayo wanafanya.

“Inaonekana dhahiri kuwa Waziri wa Tamisemi amechanganyikiwa, kwani ametoa kauli nne tofauti kuhusu uchaguzi huu,” amesema Sosopi.

Ameongeza kuwa kuvurugika kwa uchaguzi huo kumechagizwa na kuhamishwa kwa Wizara ya Tamisemi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu hadi kuwa chini ya Ofisi ya Rais.

“Lakini haya yote yanatokea na rais yuko kimya, inashangaza sana,” amesema Sosopi.

Kiongozi huyo wa BAVICHA ametilia shaka hatua ya Rais Magufuli kuwaita watendaji katika ngazi za vijiji Ikulu na kubainisha kuwa upo uwezekano mkubwa mkutano huo ulitumika kupanga mikakati ya kuharibu uchaguzi.

Amepingana na taarifa ya Waziri Jafo aliyoitoa kwa umma kwamba CCM imepita bila kupingwa kwa asilimia 51, kwamba ni ya uongo, kwani takwimu zinaonyesha chama hicho kimepita bila kupingwa kwa asilimia 71.

Amewashangaa CCM kujinadi kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati hawana watakayeshindana naye.

“Tumemsikiliza Polepole anasema kwamba wanakwenda kufanya kampeni za kistaarabu, hatujui wanakwenda kushindana na nani wakati vyama karibia vyote vimejitoa,” amesema.

Aidha, amewataka watu wote waliokuwa wamegombea kwa tiketi ya Chadema kuendelea kuandika barua za kuukataa uchaguzi huo hata kama majina yao yamerejeshwa katika orodha ya wagombea.

Amesema sakata lote ni kiashiria kuwa CCM inaogopa ushindani na kushangaa chama hicho tawala kinaogopa nini wakati kila siku viongozi wake wanajinadi kuwa serikali yao imefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Kutokana na mkanganyiko huo, Ole Sosopi amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umekosa uhalali.

Naye Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, amelieleza JAMHURI kuwa wamekwisha kutoa maelekezo kwa wanachama wao nchi nzima kuwa wasishirikiane na kiongozi yeyote atakayechaguliwa katika uchaguzi huo ili wakose uhalali.

“Shughuli yoyote ya kimaendeleo ili ifanyike kijijini inatakiwa kupitishwa na wananchi wa kijiji husika kwa asilimia 80, endapo kijiji kikiwa na wanachama wengi wa Chadema hapo si unaona mikutano mingi ya kimaendeleo itakosa uhalali,” amesema Makene.

By Jamhuri