Wiki iliyopita, sehemu ya kwanza ya makala haya pamoja na mambo mengine, mwanajeshi na mbunge mstaafu, Frank Maghoba, alieleza mtazamo wake kutokana na kauli ya vitisho inayodaiwa kutolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame dhidi ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Sasa endelea na sehemu hii ya mwisho…

Chanzo cha msuguano

Inaelezwa kuwa msuguano huo baina ya Rwanda na Tanzania ulianza kujitokeza siku chache baada ya kumalizika kwa kikao cha viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu, kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, chini ya uenyekiti wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kuzishauri Serikali za Rwanda na Uganda zifungue mlango wa mazungumzo ya amani na waasi wao. Alitaja vikundi vya uasi vilivyopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Habari zinasema ushauri huo wa Rais Kikwete uliungwa mkono na Rais Museveni, lakini kwa upande mwingine, unadaiwa kutoifurahisha Serikali ya Rwanda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, alilieleza Bunge kwamba Rwanda ilikuwa na uhuru wa ama kuupokea, au kuukataa ushauri huo badala ya kutoa kauli ya kejeli na vitisho kwa Tanzania.

Ampongeza rais, Mkuu JWTZ

Kwa upande wake, Maghoba anasema; “Binafsi sioni kosa lolote lililofanywa na Rais Kikwete kuishauri Serikali ya Rwanda, kwani kuna nchi nyingi zinazogombana lakini zinakubali ushauri wa kufanya mazungumzo ya amani kuepusha umwagaji damu.”

Maghoba anataja baadhi ya nchi zilizokubali ushauri wa kukaa meza moja kutafuta ufumbuzi wa ugomvi kuwa ni Korea Kusini na Korea Kaskazini, ambazo ni miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa duniani.

“Rais Kagame atambue kuwa ushauri aliopewa na Rais Kikwete ni msimamo wa Watanzania wote waliopo ndani na nje ya Tanzania,” anasema na kuongeza:

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania ni watu waliozoea amani, hatupendi machafuko na hata tunapowaona majirani zetu wanagombana hatusiti kuwashauri ili wamalize tofauti zao.

“Kama Rais Kagame ana dhamira ya kweli ya kutaka kumaliza mgongano nchini mwake, aukubali ushauri aliopewa na Rais Kikwete kwani machafuko yoyote ya vita yanamalizwa kwa mazungumzo, vinginevyo wananchi wa nchi husika wataendelea kupata matatizo.”

Kwa upande mwingine, Maghoba anawapongeza Rais Kikwete na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange kwa kuwahakikishia Watanzania usalama na mipaka ya nchi yetu.

“Nimefurahi kusikia Rais na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wakikemea wanaotaka kuchezea usalama wa Watanzania na mipaka ya Tanzania,” anasema Maghoba.

Alhamisi iliyopita, Rais Kikwete alihutubia wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa wa Tanzania mkoani Kagera na kutahadharisha kuwa yeyote atakayejaribu kuchezea usalama na mipaka ya Tanzania atakiona cha mtema kuni, akisisitiza kuwa JWTZ liko tayari kuilinda Tanzania wakati wote.

“Laleni usingiza salama. Msisikilize maneno ya mitaani, jeshi liko imara kulinda nchi na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia au kuichokoza atakiona cha mtema kuni.

“Ujumbe wetu wa leo ni kwamba tuko tayari wakato wote na saa yoyote kuilinda nchi na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine, hivyo kamwe hatuwezi kumruhusu yeyote kuichezea au kuimega,” alisisitiza Rais Kikwete.

Naye Jenerali Mwamunyange aliwataka wananchi, hususan wa mikoa ya mipakani kuendelea na shughuli zao bila wasiwasi kwa kuwa JWTZ liko imara.

“Endeleeni na shughuli zenu kwa amani, mipaka ya nchi iko salama, hivyo msihofu chochote,” alisema Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi.

Maghoba anawashauri Watanzania kuwa makini na kuhakikisha hawarubuniwi na kutumiwa katika kuvuruga amani ya nchi yetu iliyojijengea heshima kiasi cha kubatizwa jina la kisiwa cha amani duniani.

“Naomba kusisitiza kuwa Watanzania tuendelee kushikamana na kulinda heshima ya nchi yetu na tusisahau kulinda amani tuliyonayo kwani ni tunu ambayo wengine hawana. Tusiwape mwanya maadui waje kuharibu umoja na mshikamano wetu,” anasema Maghoba.

Anaishauri serikali kufanya uchunguzi wa kina kujua kama kauli za vitisho dhidi ya Tanzania zinazodaiwa kutolewa na Rais Kagame ni za kweli, ili ichukue hatua ya kutafuta ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Ajivunia haki ya kikatiba

Maghoba anasisitiza kuwa kujitokeza kuzungumzia suala hilo kutekeleza haki yake ya kikatiba inayompa uhuru wa kutoa mawazo.

Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema, “Kila mtu (a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi.

Wiki iliyopita, Marekani ilikaririwa na vyombo vya habari ikiitaka Rwanda kuacha mara moja kukisaidia kikundi cha waasi cha M23 kinachopambana na majeshi ya serikali na kuua raia wasio na hatia kaskazini mwa DRC.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki, alisema nchi yake hiyo ina uhakika kwamba Rwanda inawasaidia M23 kufanya mauaji ya kinyama kwa watu wasio na hatia.

“Tunaitaka Rwanda iache mara moja kuwasaidia wapiganaji wa M23, na iwaondoe wanajeshi wake wanaoshirikiana na waasi kufanya vitendo vya kinyama nchini DRC,” alisema Psaki.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha tuhuma hizo, ikisema haihusiki kuwasaidia M23.

Hivi karibuni, iliripotiwa katika mitandao ya kijamii kwamba waasi wa M23 wamemkamata askari wa Tanzania anayejulikana kwa jina la Christopher George Yohana, katika eneo la Kinyandonyi huko Kivu ya Kaskazini, DRC.


1297 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!