Leo nataka kujikita katika suala la Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote Smart Partnership Dialogue, ambayo ni dhana ya kiubunifu na msingi wake ni kanuni ya ‘Stawi Jirani Yangu kwa Manufaa Yetu Sote’.

Kanuni na utamaduni wa utaratibu wa ushirikiano kwa manufaa ya wote kwa nia ya kujenga ushirikiano baina ya Serikali na sekta nyingine, zinazochangia katika kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi, ni ukombozi kwa Tanzania yenye rasilimali lukuki tena nyingine zinazopotea bila habari au kwa kutojua.

Mfumo wa kukuza uchumi kwa njia hiyo ulianzia nchini Malaysia ambapo kwa mara ya kwanza majadiliano yalifanyika mwaka 1995 katika mji wa Langkawi, na hadi sasa Malaysia imepiga hatua kubwa kiuchumi kwa wananchi wake kuonja maisha bora.

 

Tanzania kwa kuwa ni mwanachama wa Umoja wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, iliwatuma wataalamu kwenda kujifunza Malaysia ambayo ni mwanzilishi na wanachama wengine ni Botswana, Lesotho, Swaziland, Zambia, Zimbabwe, Msumbiji, Malawi, Namibia, Uganda na Barbados.

Nchi hizo wanachama ukizitizama katika uhalisia wake uchumi wao upo juu, kwa kuwa zinafuata na kuzingatia kanuni zinazotawala umoja huo ambazo zinaeleza kwamba majadiliano yatafanyika kila mwaka katika ngazi zote za kijamii na si majadiliano ya mara moja kama vile mikutano ya hadhara au midahalo.

Kanuni zinazotawala majadiliano hayo ni dira ya pamoja, uelewa mzuri wa uwezo na udhaifu wa kila mbia, kuaminiana, kuwa tayari kuafikiana, uvumilivu na kuvumiliana, kupata mafanikio halisi au kuinua ubora ambao utakuwa endelevu.

Niliposhiriki mjadala wa kitaifa kufanya majumuisho kutoka kwenye kanda, ambao ulifanyika Mei 31 hadi Juni 2 mwaka huu katika Ukumbi wa Serena Hoteli jijini Dar es Salaam, vilitajwa Mtaji, Utaalamu na Teknolojia kuwa nguzo muhimu kwa ajili ya kuleta ufanisi kwenye juhudi za ushirikiano kwa manufaa ya wote.

Lakini pia ilibainishwa kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto za msingi tatu ambazo ni kubadili nchi kutoka uchumi usiokuwa wa viwanda kuwa nchi ya kisasa ya viwanda, kuwa na mfumo thabiti wa vipaumbele, utaratibu na uzingatiaji.

Changamoto nyingine ni kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo, zinazotokana na nchi yenyewe pamoja na nyingine za kimazingira na zile zinazotokana na mdororo wa uchumi duniani.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Tanzania inahimizwa kujenga ubia na nchi nyingine wanachama chini ya utaratibu wa ushirikiano kwa manufaa ya wote, kwani jukwaa la ushirikiano huo linatoa fursa kwa Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Madola kutambua udhaifu na uwezo uliopo kwa lengo la kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wao na nchi kiujumla.

Hapo ndipo nilipoanza kupata shaka na kuuliza swali; Rais Kikwete, hivi fisi anaweza kumbusu mbwa kwa amani? Hapa ninamaanisha kwamba nchi ina rasilimali nyingi yakiwamo madini, ambazo kwa pamoja nazifananisha kama mnyama mbwa ambaye akiwa nyumbani ni mlinzi, ukimpeleka msituni anawinda na kumpatia kitoweo mfugaji.

Vivyo hivyo, nafananisha baadhi ya wawekezaji au mataifa tajiri duniani ama nchi zile zinazofuata mfumo wa uchumi wa kibepari kama nguvu na uwezo wa fisi aingiapo katika zizi la mbwa humnyakua kiubabe na kumtafuna bila huruma tena hata mfupa habakizi.

Mfano mwingine hai ni kuwa Tanzania inafuata mfumo wa uchumi wa kijamaa kwa mujibu wa Katiba ya yetu ya sasa, na inafahamika wazi Ujamaa umemezwa na mfumo wa kibepari au mfumo changamano, hivyo hapa kwetu tunapoingia katika mfumo huo wa majadiliano kwa manufaa ya wote, tutafuata mfumo upi wa uchumi ikizingatiwa nchi nyingi wanaotekeleza mfumo huo wa ushirikiano ni zile zinazofuata mfumo wa kibepari?

Hakuna ubishi kuwa majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote ni ukombozi wa maisha ya Watanzania tena waishio vijijini,  endapo utekelezaji wa vipaumbele vilivyokusudiwa vitafanyiwa kazi kikamilifu bila kuathiriwa na siasa, ubinafsi na uongo.

Nayaeleza hayo kwa kuwa katika mfumo mzima unatawaliwa na suala la wawekezaji wakubwa na wadogo, ambao watakuja kulingana na maeneo wanayotaka kuwekeza kutokana na vipaumbele vya nchi yetu.

 

Wawekezaji hao ni kuwa watakapokuwa wanawekeza katika zao fulani na pembeni yao kuna wakulima wadogo wanalima, watatakiwa kuwasaidia kiushauri kwa lengo la kuwataka kuzalisha mazao bora yatakayoweza kukubalika katika soko.

Kupitia utaratibu huo nimefurahi Tanzania kuweka vipaumbele vya kilimo, miundombinu (Umeme, Reli, Barabara na Mawasiliano), Maji, Biashara, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Elimu ambavyo ukiviangalia vinagusa maisha ya kila siku ya Watanzania.


Katika kilimo kwa kuwa ni sekta pana, Serikali imepanga kuanza na mazao ya chakula na hapa limechaguliwa zao la mahindi na mpunga na biashara limechaguliwa zao la miwa.

Mary Sheto kutoka Wizara ya Kilimo anaeleza kwamba kwa kuwa wananchi wengi masikini wapo vijijini na uchumi wa wanchi awali ulitegemea kilimo kwa asilimia 98, hivyo imeona ipo haja ya kuwasaidia Watanzania hao.

Alieleza kuwa lengo kwa mwaka ni kuzalisha tani milioni tano za mahindi na milioni mbili za mpunga ili nchi ijitosheleze kwa chakula kwa nia ya kupunguza mfumuko wa bei ya chakula nchini na kuongeza kipato kwa mkulima hatimaye kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuuza ziada ndani na nje ya nchi ambako imebainika kuwa na soko kubwa la mazao hayo.

Anafafanua kwamba tatizo kubwa mara nyingi linakuwa ni ukosefu wa soko la uhakika kwa zao la mahindi, lakini katika hilo Serikali imejipanga kikamilifu kwani wamekwishafanya mazungumzo na Shirika la Chakula Duniani (WFP) liyanunue mahindi hayo na wameonesha kukubali, lakini kwa masharti ya kuzingatia ubora wa mahindi husika.

Kwa kuzingatia hilo, Serikali katika wilaya ambazo zitaanzishiwa utaratibu huo, wakulima wataelekezwa namna ya kuandaa zao hilo kwa ubora unaotakiwa kisha kuwahimiza kuwa katika vikundi huko huko vijijini ambako ununuzi utafanyika.

Katika kwenda sambamba na hilo, Serikali itahakikisha maghala mapya yanajengwa na yale ya zamani yataboreshwa kwa kukarabatiwa, ili mahindi yawe katika mazingira safi kwa lengo la kumvutia mnunuzi atakayenunua zao hilo katika soko la pamoja la wakulima.

Baadhi ya wilaya zitakazofaidika na mpango huo ni pamoja na Songea, Iringa, Mbozi na Sumbawanga, ambako hadi sasa hakuna ubishi ndiko kunakoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa mahindi hapa Tanzania hadi katika maeneo hayo ya mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya na Rukwa inaitwa ‘the big four’.

Kuhusu zao la miwa alieleza imekuwa ni aibu kubwa kuagiza sukari kutoka nje ya nchi wakati uwezo wa kuzalisha miwa kupitia mabonde yetu yenye maji ya kudumu mwaka mzima upo hivyo, miwa italimwa kwa wingi kuwezesha viwanda vya sukari vizalishe sukari nyingi na ziada iuzwe nje ya nchi.

Alieleza utekelezaji huo utafanyika kwa pamoja kwani tayari Serikali imetenga mashamba 25 kati ya hayo 9 ya mpunga na 16 ya miwa na kwamba baadhi ya maeneo yatakayonufaika ni pamoja na mradi wa Bagamoyo na Rufiji  Mkoa wa Pwani (Mpunga), Mpanda Mkoa wa Katavi (Mpunga), Iringa (Mpunga), Mvomero mkoani Morogoro (Mpunga) na Kilombero (Miwa).

Ilielezwa kuwa kwa sasa sekta ya mifugo haiongezi pato la Taifa, hivyo Serikali imeona ianze na mazao matatu – mpunga, mahindi na miwa. Hata hivyo, bado ufugaji wa wanyama, samaki, kuku, ulimaji wa maua, misitu na bustani navyo vitaendelea.

Hata hivyo, hayo yote hayawezi kukamilika na kuleta tija endapo suala la miundombinu halitapewa kipaumbele na ndiyo maana katika hilo Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha barabara zinapitika kwa mwaka mzima, mawasiliano yanakuwa ya uhakika na kwamba umeme ndiyo chachu ya mafanikio hayo.

Imeelezwa kwamba umeme uliopo kwa sasa hauwezi kulitoa Taifa hapa lilipo kwani gharama ya kuzalisha umeme kwa siku ni bilioni 5 wakati mapato ya TANESCO ni madogo ikilinganishwa na matumizi hayo. Kiasi kikubwa kinatumika kununua mafuta.

Serikali katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2016 imekusudia kuzalisha umeme MW 1,000 hadi MW 2,000 kwa kutumia rasilimali zetu hapa nchini, kwani imelenga kujenga njia za umeme umbali wa kilomita 3,000. Lengo ni kuhakikisha hata vijjini ambako hakuna umeme uwafikie waende sambamba na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) isiyokua bila nishati hii.

Huu ndiyo msingi wa Rais Kikwete kumwalika Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye ameahidi kuisaidia Tanzania katika mambo mengi ikiwamo suala la umeme ifikapo mwaka 2016 hivyo yapimwe mafanikio kwa kilichopangwa na Serikali kupitia  Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote.


Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika nchi ya Malaysia imechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi na kuondoa umasikini kwa wananchi wake kwa kuwa iliweza kuwaingiza wananchi katika mifumo rasmi ya kifedha.

Kennedy Komba wa Benki Kuu ya Tanzania anasema Watanzania walio wengi hawapo katika mifumo rasmi ya kifedha, na ndiyo maana wanashindwa kudhaminiwa kupata mikopo kwenye taasisi kubwa za kifedha.

Akitoa mfano anasema hivi sasa Watanzania wengi wanaweka fedha kupitia utaratibu wa kujiunga na VICOBA bila kujua kwamba si sekta rasmi inayotambuliwa na Benki Kuu, ambayo ndicho chombo kinachoshughulika na mifumo ya malipo hapa nchini.

Alifafanua kwamba Watanzania waliopo kwenye mifumo rasmi ya kifedha ni asilimia 12 tu, jambo linaloendeleza umasikini katika nchi yetu na kuonekana kundi dogo lina uwezo kiuchumi na kubwa limeachwa solemba.

Hivyo alieleza kuwa TEHAMA inaweza kuwaingiza wananchi kwenye mifumo rasmi ya kifedha kwa mfano kupitia mtandao wa M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money ambako wananchi wengi wanaweka fedha zao lakini bila kupata tija nyingine zaidi ya kutuma na kupokea fedha.

Kwa mantiki hiyo kupitia majadiliano hayo ya Dar es Salaam iliamriwa kuanzisha mchakato wa kutumia TEHAMA kama chanzo cha kukuza uchumi wa nchi.

TEHAMA ni eneo jipya kwa Watanzania walio wengi hususani huko vijijini, hivyo ipo haja ya kufanya kweli katika mitaala ya elimu kuweka somo la kompyuta shule zote kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu.

Hata hivyo, katika mijadala wakati wa kutembelea vikundi, kipaumbele cha kilimo washiriki walihoji ikiwa huko vijijini kunatolewa hatimiliki za kimila na inaelezwa kuwa zinatambulika na Serikali, lakini mbona wakulima wanapotaka kukopa katika taasisi za kibenki hawapewi mikopo?

Jibu lilikuwa kwamba kama ardhi itawekwa kama dhamana ya mkopo, mkulima akashindwa kulipa na ardhi ikachukuliwa huyu mkulima atakwenda wapi? Hata hivyo eneo hili ilielezwa na Serikali kuwa linahitaji mjadala ili kulinda haki ya pande zote mbili.

Pamoja na hayo yote katika hilo wananchi watahoji tu kwamba hivi mashamba makubwa kama vile Nafco, Kapunga wilayani Mbarali, Matombo Morogoro na Sasakawa Global 2000 yalianzishwa kwa madhumuni gani, na kama yalikufa aliyaua nani pia sababu zipi zilichangia kufeli kwa miradi hiyo?

Vile vile viwanda vya korosho, ngozi, nguo, magunia vipo wapi na kama vilikufa nani akliyeviua na kitu gani kilisababisha kifo hicho?

Kulikuwa na mfumo wa wakulima kuuza mazao yao kupitia vyama vya msingi na vikuu vya ushirika; je, hali hiyo ipoje kwa sasa hapa nchini ikiwa lengo lilikuwa ni kuwa na soko la pamoja kwa mazao ya wakulima, lakini ilishindikana?

Je, ni kitu gani kitakachofanya mfumo huo wa zamani ambao sasa unatajwa kuwa mpya wa soko la pamoja la wakulima usife? Je, waliochangia kufa kwa ushirika wapo au wapo wapi na wanafanya nini? Je, ni kweli mipango hiyo ni ya kweli au ni kisindikizo cha uchaguzi wa 2015?

Chonde Rais Kikwete, mfumo huo usije ukawa kama kituko cha mnyama simba ambaye siku moja alivamia kundi la swala ghafla, swala wakubwa wakakimbia akabaki mtoto ambaye alikuwa hawezi kusimama vizuri, simba akamsogelea yule swala mtoto na kuanza kumlamba.

Kutokana na uchu wa simba, alimlamba swala huyo mtoto hadi kumchuna ngozi na damu zikawa zinabubujika kisha alipoona amechunika, simba akaamua kumtafuna moja kwa moja na ndiyo ukawa mwisho wa uhai wake.

Rais Kikwete, ebu wadhihirishie Watanzania kwamba ule msemo wa kuwa mtu anajikwaa wakati wa kwenda na si wakati wa kurudi, ni wa kweli kwa kufanikisha mfumo huo wa  Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue) dhana ya kiubunifu ambayo msingi wake ni kanuni ya ‘Stawi Jirani Yangu’ kwa ‘Manufaa Yetu Sote’.


Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika ili mpango huu wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue) uivishe nguo Tanzania yenye rasilimali nyingi, lakini wananchi wake ni masikini.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba

0767655598 au [email protected].


Please follow and like us:
Pin Share