Sehemu iliyopita, mwandishi alinukuu ibara ile ya kwanza ya

Mkataba wa Muungano na kusema mtu akiisoma atajua ilikuwa na viashiria vya undugu na umoja wetu wa asili kati ya watu wa nchi hizi mbili – Tanganyika na Zanzibar. Hii ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala ya Katiba Mpya iakisi uzalendo. Endelea

Maneno mazito namna hii na ya kizalendo kutoka kwa watu wa Zanzibar, leo mtu aje aseme mbona hatukushauriwa: Oh! mbona hatukuulizwa hivi. Wanaofyatuka kusema hivi walikuwa na umri gani Aprili 24, 1964? Pengine wala hawakuwa wameingia ulimwenguni. Leo waje na stori za watu wa Zanzibar eti waulizwe wanautaka Muungano au hawautaki ndipo Katiba yetu iandikwe ni sahihi kweli wazee wenzangu?

Labda Mzee Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki ambaye ndiye pekee yu hai miongoni mwa wale wajumbe 14 wa Kamati ile iliyoongoza Mapinduzi Januari 12, 1964 aulizwe kama haya ninayoyaandika ni matukio ya kweli au la.

Mwingine ni Mzee Hassan Nassor Moyo aliyehudhuria hata kile kikao cha Katiba kule Lancaster House, Uingereza, Septemba 20-24, 1963 na ndiye aliyefuatana na Sheikh Abeid Amani Karume katika mikutano yake na Mwalimu Nyerere mara baada ya Mapinduzi, anasemaje? Kinachokosekana hapa ni elimu na maelezo ya kihistoria kwa vizazi vipya waone na watambue Muungano ulikotoka mwaka ule wa 1964.

Nimetumia muda mrefu kuelezea hali ya Muungano ulivyoanza ili kusiwe na utata (ambiguity) katika mawazo ya wananchi kuhusu umuhimu wa kupata Katiba sahihi, sanifu na ya watu wote.


Tusipumbazwe na makelele ya wenye uchu wa madaraka. Maswali muhimu hapa ni je, sisi sote leo hii kwa hali ilivyo tu Taifa gani? Tuko mataifa mangapi katika nchi hii? Tunataka Katiba mpya ili iweje? Tuwe na uraia wa mataifa mengine au Taifa moja tu?


Kwa namna Muungano wetu ulivyo, pande zote mbili za Jamhuri zinanufaika. Bila kuwa na hali namna hii ingewezekana kweli mtu wa Zanzibar kuwa Mbunge wa Jimbo lolote huku Bara? Hivi kwa style yetu hii ya muungano tulikuwa na Mbunge wa Mkuranga mwenye asili ya Visiwani, nani alishtuka?


Leo hii, tunapodai Muungano una kero nyingi mbona wa Visiwani zaidi ya watu wake 600,000 (Jamhuri Toleo No. 88 la tar 18-24 Juni Uk. 2) wana umiliki wa ardhi huku Bara? Wametapakaa huku Bara wana majumba, mashamba na miradi kemkem.


Wapemba wapo Rukwa, Kigoma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Mtwara hata Ruvuma. Je, hawa si wataathirika sana? Kero wanaziona viongozi wa siasa wenye uchu wa madaraka, lakini wa visiwani wengi wanafaidi sana maisha ya huku Bara. Wameoa na kupata watoto ambao ni WATANZANIA. Je, wanaweza kuwa Wazanzibari kesho Katiba ikiamua hivyo? Watoto wetu namna ya hao watapata malezi ya Taifa lipi?  Tanganyika, Zanzibar au Tanzania? Mie sintofahamu lolote katika hili. Kule visiwani kweli ipo ardhi ya kuwameza hawa “Wazanzibara” wakirejea kule? Tuwe tunasema kwa kufikiria matokeo ya wengi siyo kusema kwa kunogewa na madaraka ya kisiasa.


Moja ya Kero za Muungano wetu wa sasa ni kukosa MAADILI YA KITAIFA. Hili limetufikisha hapo pa kudai Muungano umeshindwa kabisa kutuunganisha kuwa wamoja. Hata vazi la Taifa tu, Tanzania hatuna! Kwa muda wa miaka 50 ya Muungano tumeshindwa kuwa wazalendo. Je, tukiwa na Serikali tatu si ndiyo maadili yatamomonyoka zaidi? Wazanzibari watakuwa na utamaduni wa Kiarabu, Watanganyika watabaki hoi hawajui wawe na utamaduni upi. Je, sasa hao raia wa Serikali ya Muungano mpya watakuwa na utamaduni upi? Visiwani walianza kudai bendera ya Zanzibar, wakadai na wimbo wa Zanzibar, sasa kwa Katiba hii watamalizia dai la dola ya ZenjBar! Tutakomea wapi?


Tukiweza kutafakari hayo na kutoa uamuzi sahihi tutakuwa tumefanikiwa kupata Katiba ya wananchi. Kero zipo katika kila aina ya Muungano – zipo za Serikali huku Bara na pia zipo za Serikali kule Visiwani. Kamwe hakuna Katiba itakayoandikwa eti ikawa ni fool proof ya kuondoa kero zote za nchi yoyote ya Muungano ulimwenguni na hivyo kupokewa na jamii yote. Hakuna.


Kisayansi sote tuliokwenda shule tunajua fika mashine zimetengenezwa kuturahisishia kazi zetu. Lakini hakuna mashine hata moja yenye asilimia 100 za urahisishaji kazi za mwanadamu. Tunasema “No machine has 100% mechanical advantages”. Sisi tunaotaka Katiba kamilifu tutaipata wapi na itakuwa kwa watu wa aina gani?


Ombi langu na wazo langu, tuipe Tume mawazo yetu, vionjo vyetu, maoteo yetu kisha tuisaidie itimize kazi yake ya kutuandikia Katiba Mpya na mwafaka kwa Watanzania wote. KATIBA YA KIZALENDO. Tukichungulia nyuma tu kule tulikotoka tutajageuka mawe! Hapo majuto ndiyo yatakuwa mjukuu.

Basi, kwa mtazamo wa sisi wazee na mimi nawafikiria zaidi wazee wa sekta isiyo rasmi, ni vema Katiba Mpya iwaainishie haki zao waziwazi. Jinsi zilivyoandikwa mwenye rasimu hii kwa mtazamo wa sisi tusiokuwa na elimu ya kisheria hatuelewi; ni bora ikaandikwa waziwazi na kwa lugha nyepesi. Rasimu hii ya Katiba ingesema hivi;-


SURA YA NNE: HAKI ZA BINADAMU, WAJIBU WA RAIA NA MAMLAKA ZA NCHI

SEHEMU YA KWANZA: HAKI ZA BINADAMU – Kifungu No. 47 haki za wazee.

Hapa ilivyoandikwa ninaona Katiba imechujisha (diluted) sana uzito wa haki za wazee. Vifungu 42, haki za watoto; 43 haki na wajibu wa vijana; 44 haki za watu wenye ulemavu na 46. Haki za wanawake humo Rasimu ya Katiba Mpya imeainisha vizuri kabisa na wala hakuna utata wala kutoa dhana ya hali ya kuwa na maana nyingi (no ambiguity whatsoever).


Lakini kile kifungu na. 47 ndiko kwenye utata.

Kilio cha wazee ni kuwa haki zao zimefinyangwa, basi napendekeza ziandikwe wazi wazi na bila utata kama hivi:-

 

1. Wazee watambuliwe huo utu wao wa uzee na waheshimiwe pasipo kudharauriwa (enhance the recognition of the dignity of older persons while eliminating all forms of neglect, abuse and violence).

 

2. Wazee walelewe na kupata misaada kutoka familia zao, jamii na mamlaka ya nchi, (the primary responsibility of government in promoting, providing and ensuring access to basic social services such as universal and equal access to health care, shelter, food an clohing). Wapate hifadhi ya jamii.

 

3. Wazee wapewe fursa ya kuendelea kutumia utaalamu na ujuzi wao kwa manufaa ya umma. Ni watunzaji wa mila, desturi, na utamaduni wa Taifa. (Enable society to rely increasingly on the skills, experience and wisdom of older persons, and should have the opportunity to work for as long as they wish and are able to work in productive work. They are custodians of cultural heritage and customs). Wapewe fursa ya kuendeleza mila na utamaduni wa Taifa.

 

4. Serikali iwajibike kuwapatia wazee uongozi thabiti katika utayarishaji na uundaji wa asasi za wazee katika kutekeleza mambo yote ya wazee na kuzeeka (government has the primary responsibility of providing leadership on aging matters to effect collaboration between national and local governments and international agencies).

Huu ni mtazamo wangu na maombi yangu kuwa Katiba ianishe waziwazi haki namna hiyo za wazee. Aidha, waandishi wa rasimu hii wote ni wazee kwa umri, lakini kwa vile hali zao zilikuwa nzuri walipokuwa wanalitumikia Taifa katika sekta rasmi na walikuwa na vyeo vya juu, hawajui adha ya wazee makabwela wa ile sekta isiyokuwa rasmi.

Enzi za TANU, Katiba ya chama kimoja haikuwagusa kabisa wazee licha ya kuweka katika katiba ya chama sehemu ya Baraza la Wazee. Kosa lile sasa ndiyo muda mwafaka kulirekebisha. Ni kero kubwa kwa wazee wa nchi hii. Wamesahauliwa, wanateseka na hata kuuliwa kwa visingizo vya uchawi huku hali ya maisha yao ikiwa inajulikana dhahiri kuwa ni ngumu sana.

Basi, naona huu ni muda mwafaka kwa Taifa kuwatambua wazee kikatiba. Umoja wa Mataifa uliwatambua hivyo pale walipowaingiza katika haki za binadamu mwaka 1948 katika kifungu 25 (1). Pia Umoja huo umewatambua tena wazee mwaka 1999 ulipotangaza na kuweka Oktoba Mosi ya kila mwaka kuwa Siku ya Wazee Duniani. Ni shinikizo tosha kuwa Taifa letu liweke kwenye Katiba yake mpya haki za wazee wake kama walivyotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Wazee ni hazina ya Heshima na Busara; ndiyo maana Kamati ya kuandika Katiba yetu mpya ina wajumbe wazee wengi kuliko vijana. Katiba Mpya isiwe na mtazamo wa kisiasa zaidi, bali iwe na mtazamo wa UHALISIA. (The elderly are a reality and not an imaginary living being). Tupo, tunaumia huku vijijini. Serikali inatutambua kupitia ripoti za watoto wetu wataalamu wa vyuo vikuu! Ninaomba watuone na watusikilize ana kwa ana. Hakuna ugumu wa kupata wazee kutoka kila mkoa wa nchi hii kutukutanisha na kutuona kihalisi (physically) na kutusikiliza. Serikali itajua mengi na kuwa na maandalizi sahihi ya kutupa pensheni kwa wote kwa mpango wa hifadhi ya jamii.

Kwa vile mwisho wa Julai mwaka huu nimetimiza umri wa miaka 83 ya kuzaliwa kwangu, napendeza makala haya ya Katiba Mpya yaakisi Uzalendo – ifunge uandishi wangu wa makala katika magazeti.Ukongwe unapendeza zaidi kuwa mtulivu na mkimya. Kwa kirumi wanasema: “Sic tarsis prudentere vidises”. Ninawaomba wasomaji na wapenzi wa makala zangu radhi kwa hili la kuacha kabisa kuandika makala kutokana na ukongwe wangu.

Fundi Konde enzi zetu akiimba kule Mombasa wimbo wa JABALI LILE, alimalizia kwa maneno MKIONA KIIMYA KWA HERINI! MKIONA KIIMYA KWAHERINI” Alamsiki au Adios! Wasomaji wa makala zangu.


1709 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!