Maisha ndio mtihani mgumu sana, kuushinda mtihani huu ni kufanya maisha yavutie. Ukipata kazi mtihani, usipokuwa na kazi mtihani. Ukiwa na pesa mtihani, usipokuwa na pesa mtihani.

Kama umesoma sana mtihani, kama haujasoma mtihani. Inasemwa kuwa: “Ukiona elimu ni gharama jaribu ujinga.” Ukiwa na usafiri wako mtihani, usipokuwa na usafiri wako mtihani. Ukiwa na marafiki mtihani, usipokuwa na marafiki mtihani. Ukiwa na ndugu zako mtihani, usipokuwa na ndugu mtihani. Ukioa au kuolewa ni mtihani, usipooa au usipoolewa ni mtihani.

Yaliyopita ni mtihani na yajayo ni mtihani. Ingawa tunasema yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo, tunaweza kuyatazama yaliyopita kwa shukrani.  Mike Rowe alisema: “Nayatazamia yajayo na kuwa mwenye shukrani kwa yaliyopita.”

Ukiwa na mipango, mtihani. Biblia yasema: “Binadamu hupanga mipango yake, lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi Mungu.” (Mithali 16:1-2). Usipokuwa na mipango ni mtihani, maana hatupangi kushindwa lakini tunashindwa. “Maisha ni ndoto ya wenye hekima, mchezo kwa wapumbavu, mchezo wa kuchekesha kwa matajiri, janga kwa maskini,” alisema Sholom Aleichem.

Maneno ya Sholom yanabainisha kuwa maisha ni mtihani. Maisha ni mtihani kwa vile kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka. “Maisha ni kama kitunguu: unaondoa ganda baada ya ganda, na wakati mwingine unatoa machozi,” alisema Carl Sandburg.

Ukipanda cheo mtihani, ukishuka mtihani. Ukipanda cheo ni kuwa katika hali ya hatari. Kuna wenye wivu, kuna ambao wanataka kukuvuta chini uwe kama wao. Sababu zilizokupeleka juu si zile ambazo zitakufanya kubaki juu. Nalo hilo ni mtihani.

Kila mara unaweza kupandishwa cheo mpaka ukafikia cheo cha kuwapandisha wengine wakati wewe haupandi tena, nalo hilo ni mtihani.

Kushindwa ni mtihani, upitie bila kukata tamaa.  John F. Kennedy alisema: “Mafanikio yana baba wengi, lakini kushindwa ni yatima, hakuna anayetaka kujitambulisha kama baba yake.” Maisha ni mtihani, yana kushinda na kushindwa. Ukishinda katika maisha ni mtihani, unaweza kuwa na maadui na kuonewa wivu. Ukishindwa katika maisha ni mtihani, unaweza kudharauliwa. Lakini kushindwa ni vijilia ya mafanikio.

“Nilishindwa baadhi ya masomo kwenye mtihani, lakini rafiki yangu alishinda masomo yote. Kwa sasa yeye ni mhandisi katika Kampuni ya Microsoft na mimi ni mmiliki wa Kampuni ya Microsoft,” alisema Bill Gates.

Kushindwa ni mtihani, lakini Bill Gates alishinda mtihani huo. Mtihani ni njia ambayo mtu anapimwa. Kushindwa ni njia ambayo mtu anapimwa. Katika maisha unahitaji kujiamini.

Bill Gates alijiamini licha ya kushindwa. Ndege anayekalia tawi la mti haogopi kuwa tawi litavunjika kwa sababu imani yake haipo katika tawi bali katika mbawa zake.

Watu wakikuona kuwa una sura nzuri, ni mtihani, kwa sababu methali ya Tanzania inasema, ‘wazuri hunuka mdomoni’. Watu wakiona una sura mbaya ni mtihani. La msingi sisitiza uzuri wako wa ndani. Hadithi ya maisha ya Jennifer Tress inasema yote.

Aliolewa na mwanachuo wake akiwa na umri wa miaka 23 na ndoa yao ilivunjika akiwa na umri wa miaka 26. Aliambiwa na mume wake, “You’re Not Pretty Enough,” (Wewe si mrembo kamili).

Alitumia maneno hayo kutunga kitabu juu ya maisha yake ambacho kimependwa sana. Kitabu hicho ni wimbo unaoimbwa katika karatasi. Mwanamama huyo amebainisha uzuri wake wa ndani. 

Maisha ni mtihani. Inavyoonekana kila mtu ana karatasi yake ya maswali. Tatizo watu wanapotazamia wengine wanafanya mtihani ambao si wao. Kuiga ni kujiwekea mipaka. Kama mbili kujumlisha na sita ni nane, elewa kuwa nne mara mbili ni nane pia. Njia yako ya kufikia nane si njia moja tu. Heshimu njia za wengine.

Unapomaliza mitihani shuleni au chuoni, unaingia katika shule ya maisha. Maisha ni mtihani. “Janga la maisha ni kile kinachokufa ndani mwa mtu wakati anaishi,” alisema Albert Schweitzer. Kama maisha ni mtihani, uufanye hata kama ni mgumu, lisilowezekana linawezekana. 

1463 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!