Ndugu Rais, katika kurasa za mwanzo za kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, ‘’Kila kaya iache kibatali chake kikiwaka. Tumelishauri  jua lisitokee mpaka nchi itakaporudishwa kwa wananchi. Nenda katangaze neno hili. Usinitaje, kwaheri!’’

Kila tusomapo maandiko haya hutulia na kujiuliza, kati yetu ni nani anayeiona kesho yao wana wa nchi hii?

Awaambie basi watu wa Mungu kwa maana mioyo yao imejazwa hofu baada ya matumaini yao kufifia. Kuwatia hofu wana wa Muumba ni kuitafuta laana.

Sasa wanakwenda kwa kupapasa wakihofia mwisho wao ambao haujulikani jinsi utakavyokuwa! Kwa mwendo huu, mwisho wa yeyote unaweza kuwa vyovyote!

Iliandikwa kwa wino usiofutika kuwa Butiama kuna kaburi. Ole wao wanaokwenda bila ufahamu wa kuwa ndani ya kaburi lile hakiingii chochote kinyonge kwa maana amelala mteule! Tunasema ole wao kwa kuwa wamekiuka maagano. Tuliagizwa tumpende Mungu wetu kwa moyo wetu wote na kwa akili zetu zote. Kisha, tumpende jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe. Jirani leo tumemgeuza kidudu-mtu wa kumteka, kumtesa na hata kumuua! Hakika hatutaikwepa laana ya Muumba wetu!

Tumekwenda Butiama kuchukua ithibati ya makali ya upanga dhidi yetu.

Na kwa sababu hiyo siku yetu ikifika, dhiki kuu itatushukia. Maandiko katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu yanasomeka hivi. ‘…Pamoja na suluba yote hiyo, bado Mwalimu Mkuu wa Watu aliweza kusema, akiwa kama mtu aliyepagawa au aliye na mapepo, akamwambia Msauzi, ‘Uhai wangu na wako na wa yeyote yule, ni mali ya Mungu. Yeye tu ndiye mwenye haki ya kuutoa na kuutwaa. Kwa upofu ulionao unadhani utatatua matatizo yako kwa kuniua mimi! Maskini wee! Hujui kuwa kumbe ndiyo kwanza utakuwa unamwaga petroli katika moto uwakao! Nimekuja kukuambia kuwa siku yako ya hukumu imewadia. Una macho makubwa, lakini hayaoni. Una masikio mapana lakini hayasikii. Laiti ungelikuwa na macho yanayoona ungeliona kalenda ya siku zako ilivyomalizika. Laiti ungelikuwa na masikio yasikiayo, ungeisikia kasi ya siku yako ya hukumu inavyokujia. Zikumbuke siku za ujana wako utaona kuwa wewe sasa ni sawa na mpira usiokuwa na upepo au upatu uvumao. Siku ulizobakiza zinaenda kama moshi ufukao baada ya moto kuzimwa. Hutapakaa angani na kuisha bila kuacha alama yoyote’’’.

Baba imeandikwa kuwa hatutahukumiwa kwa madaraka tuliyokuwa nayo, bali kwa jinsi tulivyoyatumia madaraka hayo tuliyokuwa nayo! Majuto yatakuwa mengi siku hiyo yatakayosababisha kukumbukwa majuto ya Waziri Mkuu kama yalivyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu nukta kwa mkato. Imeandikwa nafsi ya Waziri Mkuu ilianza kumsuta na kumfanya aweweseke na kusema peke yake, “Sijui nimlaumu nani, kati ya nafsi yangu au shetani. Nailaumu roho yangu kwa kuniongoza katika njia mbaya na potofu. Leo hii mimi Waziri Mkuu nimekuwa mpofu, zumbukuku, mzungu wa reli asokuwa na mbele wala nyuma. Tabu na shaka vimenizingira.

“Ukuu wangu sasa siuoni. Nasononeka peke yangu. Natanga na njia wa kunisaidia simuoni. Ni kweli huu ndiyo mwisho wa kipindi cha neema? Je, huu ndio mwanzo wa kipindi cha dhiki kuu?” Akatulia tuli.

“Niliitwa Mheshimiwa. Nilikuwa na madaraka makubwa. Nilitembea kwa kuongozwa kama mtu asiyejua aendako. Safari zangu ziliitwa msafara. Niliongea kwa kushauriwa. Watu wazima wasomi waliitwa wasaidizi wangu.

“Wako wapi washirika wangu, wakubwa wenzangu walionishauri kuutenda ukatili huu? Niko peke yangu Kafriko Mchumiatumbo mimi. Si kitu tena. Nimekuwa Kindengereka. Kinyangarika tu. Kidubwasha cha kutupa jalalani.

“Waje basi washikaji zangu angalau wanitie moyo. Wanipatie ushujaa na kunijengea ari hata kama si mpya ili nipate kasi ya kutoka hapa kwenda mbali kutafuta mwelekeo mpya ili kuepuka aibu hii.

“Waje hapa wajifunze kwangu wale viongozi dhalimu na watesi wa raia. Wala rushwa na wafujaji wa fedha za walipa kodi. Wale walevi wa madaraka na wafifishaji wa haki za raia. Wapotoshaji wa maadili ya utaifa na wakiukaji wa haki za binadamu. Waje waone mfadhaiko na kutapatapa kwangu.

“Ala kumbe! Hata ukimiliki nguvu za dola haziwezi kukusaidia kufa kifo chema. Basi, wajifunze kwangu wale watakaoyaona mahangaiko ya kufa kwangu. Ala, kumbe! Kila zama na watu wake.

“Walikuwepo wafalme waliokuwa na mamlaka na majeshi yenye nguvu kupindukia. Watawala walioitawala dunia kwa upanga wa moto. Leo wako wapi? Hawako tena. Wamekwishapita. Na sisi tunapita. Wanaojiita waheshimiwa watawala badala ya watumishi wa wananchi waje wajifunze hapa.

“Walikuwepo masultani waliofanya kila aina ya ufirauni, wao wakiuita starehe! Je, leo wako wapi? Hawako tena! Wamekwishapita. Na wale majemedari nduli walioua raia na askari kwa maelfu kwa utashi tu na ujivuni, nao leo wako wapi? Wamekwishapita kusikojulikana! Ni wajibu wetu kuwaachia watoto wetu nchi nzuri kama tulivyoikuta. Nchi yenye mito iliyojaa maji na samaki wa kila aina. Makonde yenye majani mabichi na miti iliyosheheni ndege wazuri waimbao juu yake. Nchi ya maziwa na asali. Nchi ya amani na upendo. Yenye utajiri mwingi juu na chini ya ardhi. Kwa kufanya hivyo tunakuwa tunajitengenezea mwisho mwema.

“Itanifaa nini mimi hata nikikusanya watu wengi kupindukia siku ya maziko yangu? Hata wakija viongozi mbalimbali wa dunia na maiti yangu ikafunikwa sanda ya bendera ya taifa itanisaidia nini huko niendako?

“Nitakuwa peke yangu. Ala, kumbe! Nilikuja bila kitu na nitaondoka bila kitu. Haijalishi jeneza langu litakuwa na thamani kiasi gani, lakini litafukiwa chini. Kweli duniani tunapita tu. Ee Baba uliyewatuma manabii na mitume wako nasi tukawapuuza, kama hutasamehe, ukatuhesabia makosa yetu yote, kati yetu sisi nani atasimama? Wa kuiona mbingu watakuwa wachache.

“Walisema utavuna ulichopanda. Natamani kupanda upya ili nibadilishe mbegu, lakini msimu wangu wa kupanda umekwishapita na mvua za kupandia kwangu haziko tena. Bora basi nizame kabisa katika hili dimbwi ili uwe ndiyo mwisho wa maumivu ya kukumbuka kilichotokea.”

“Mioyo ya masikini wa nchi hii inazidi kufifia kadri siku zinavyosonga. Labda walichokitarajia sicho!

Please follow and like us:
Pin Share