Upendo ni mtihani, palipo na husuda, hakuna upendo. Palipo na chuki hakuna upendo. Palipo na umbea hakuna upendo. Maneno kwenye kanga za kina mama yanabainisha upendo ni mtihani.
Chokochoko za jirani hazinitoi ndani, mtamaliza visigino kwa safari za umbea. Hunilishi, hunivishi na wala hunibabaishi, vikao kaeni, umbea  acheni, penye udhia penyeza rupia. Usisafirie nyota ya mwenzio, macho yanacheka, moyo unalia. Muogope nguru mbili, chuki humchoma anayeitunza. Maneno hayo yote yanabainisha upendo ni mtihani.

“Kuna mtoto aliyepewa mwanasesere. Baadaye alimwambia mama yake: “Nampenda mwanasesere lakini yeye harudishi upendo.” Unaweza kumpenda mtu asirudishe upendo. Unaweza kuwapenda watu wasirudishe upendo, upendo ni mtihani.
Upendo ni mtihani, anayekupenda anakwambia ukweli katika upendo. Charles Lowery alilalamikia maumivu ya mgongo akiwa ana rafiki yake, alitaka kuhurumiwa na rafiki.
Badala yake rafiki yake alimwambia: “Sifikiri kuwa mgongo ni tatizo lako, tatizo lako ni tumbo, tumbo lako ni kubwa sana linavuta mgongo. Punguza tumbo, shida yako unakula sana. Charles Lowery hakukasirika badala yake aliufanyia kazi ushauri wa rafiki yake.

Alipunguza tumbo na maumivu ya mgongo yakaisha polepole. “Majeraha utiwayo na rafiki yanaonyesha uaminifu; lakini busu la adui ni udanganyifu.” (Mithali 27:6). Charles Lowery alitiwa jeraha la moyo lakini linaonyesha ukweli katika upendo, baadaye aligundua kwa kula sana kupita kiasi alikuwa hajipendi.

Upendo unadai kujipenda, kutojipenda ni kama kuendesha gari bila breki. Huwezi kumpenda mwingine kama hujui kujipenda na kujithamini, kujipenda ni kipimo cha upendo kwa mwingine.
Kujipenda si ubinafsi ni kujipendelea. Katika matukio fulani fulani watu huambiwa: “Unajipenda au hujipendi?” Kama unamtafuta mtu ambaye atabadili maisha yako mtazame kwenye kioo. Mtu huyo ni wewe, jipende.
“Jipende kwanza na mambo mengine yataingia kwenye msitari wake. Lazima ujipende ili jambo lolote lifanyike katika dunia hii,” alisema Lucille Ball.

Upendo ni mtihani, unadai kupenda na kupendwa na kwa msingi huo upendo ni mtihani.  Mwenye upendo uliokomaa anasema: “Nakuhitaji kwa vile nakupenda.” Mwenye upendo ambao haujakomaa anasema: “Nakupenda kwa vile nakuhitaji.”
Katika msingi huo upendo ni mtihani juu ya ukomavu, penye upendo hakuna umbali. Utampenda mtu zaidi ya umbali uliopo kati yako na yeye. Tumeumbwa kupenda na kupendwa.
“Upendo wa kweli ni yote mawili, kupenda na kuruhusu kupendwa. Ni vigumu kuruhusu kupendwa kuliko kupenda,” alisema Papa Francis. Waruhusu wengine wakupende.
Upendo unadai kuwapenda adui zako ni mtihani. “Upendo utashinda chuki,” alisema Mohandas Gandhi. Mtu ambaye amekuwa adui yako anaweza kuwa rafiki yako. “Upendo ndio nguvu pekee inayoweza kumbadili adui akawa rafiki,” alisema Martin Luther Junior wa Marekani.

Unapompenda adui unadhoofisha uadui, unamnyima nguvu adui, upendo unaweza kukua au kudumaa.  “Upendo unakufa, unapobinafsishwa unakua kwa kutoa,”  alisema Elbert Hubbard.
Upendo ni suala la moyo. “Kila mmoja anaweza kuwa mtaalamu wa moyo, jambo moja linalohitajika ni kumpenda mtu,” alisema Angle Papadakis.
Unapopita acha alama za moyo wa upendo, kila unapopita unaacha alama, alama za vidole kwenye vitasa, kuta, vitabu, vijiko, milango. Sasa ujitahidi kuacha alama za moyo (heartprints).
“Upendo unaweza kumbadili maskini omba omba akawa kama mtoto wa mfalme,” alisema TB Joshua. Upendo unatajirisha, anayependwa ni tajiri wa upendo,  lisilowezekana linawezekana.
Tunaweza kupenda na kupendwa. Unapomsaidia mwenye shida, unaacha alama za moyo, unapomtembelea mgonjwa unaacha alama za moyo, unapoyagusa maisha ya wengine kwa ukarimu unaacha alama za moyo.
Unapokutana na watu wanapima kichwa chako lakini unapoondoka wanapima moyo wako wa upendo.

By Jamhuri