Umoja wa Mataifa (UN) umepanga Februari  21, kila mwaka ni ‘Siku ya lugha ya mama duniani.’ Siku hii ina lengo na madhumuni ya kukumbusha na kudumisha utamaduni (historia, mila na desturi) wa kuzungumza lugha mama ambayo ndiyo lugha ya asili kwa mtu yeyote duniani.

Katika utafiti uliofanywa na umoja huo, na ripoti yake kutolewa mwaka jana inaeleza kila baada ya wiki mbili lugha ya mama, yaani lugha ya asili inapotea duniani. Hii si taarifa njema kwa mataifa yote duniani.

Taarifa hii si ya kuisoma, kuipokea na kuiadhimisha tu, ni taarifa inayohitaji kuangaliwa kwa undani na kuzingatiwa kwa umakini katika kufanyiwa kazi ili kunusuru upoteaji wa lugha mama. Kwa sababu lugha hii ni lugha ya asili kabla ya kujifunza lugha nyingine.

Lugha yoyote inazaliwa, inazungumzwa na inalelewa na mtu au watu wanaoitumia. Lugha inatumika katika mawasiliano, kutoa elimu na kuunganisha fikra za mtu na mtu kama vile mama na binti, baba na mwana, meneja na watu walio chini yake, padri au sheikh na waumini wake.

Lugha isipofanyiwa matumizi au malezi, ikapuuzwa au kuachwa, inakufa. Hapa ndipo kilipo kiini cha Umoja wa Mataifa (UN) kuhabarisha mataifa duniani na kuchukua hadhari kunusuru lugha mama kupotea.

Ni dhahiri, tayari lugha kadhaa zimepotea (kufa) duniani kwa mujibu wa taarifa hii. Sisi Watanzania hatuna budi kujitathmini iwapo tumekwisha kupoteza au tunaelekea kupoteza lugha mama. Kwa vyovyote vile, nia iwepo ya kufufua au kutumia.

Lugha mama au lugha ya asili ni lugha ambayo mtoto (mtu)  ameanza awali kuisikia, kuielewa na kuitumia katika mawasiliano ya malezi na wazazi wake. Tunasema ni lugha iliyomuogesha jimbo na kubembelezewa na mama yake tangu akiwa mtoto mchanga.

Hapa Tanzania tuna makabila zaidi ya 125 na kila moja lina lugha mama. Ndiyo lugha ya awali mtoto kuifahamu na baadaye kujifunza lugha mpya, lugha za mapokeo kutoka makabila au mataifa mengine.

Nazungumzia lugha ya Kiha, Kihaya, Kizaramo, Kimwera, Kisukuma, Kichaga, Kizanaki, Kihehe, Kinyamwezi, lugha za makabila mengine na kadhalika. Hata Kiswahili ni lugha mama kwa watu ambao hawana lugha nyingine iliyowaogesha jimbo, ila hii ya Kiswahili.

Watu hawa aghalabu hupatikana katika maeneo ya upwa, tangu pande za Lamu hadi huko Kusini (hasa upwa wa Kaskazini wa Msumbiji) pamoja na visiwa vya Unguja, Pemba na Ngazija. Watu hawa wanatumia Kiswahili ikiwa lugha mama.

Hivi leo wakazi wengi wa mijini wanatumia Kiswahili katika mawasiliano, kupata elimu na kufanya biashara ikiwa ni lugha ya mapokeo, wakati wakazi wa vijijini wengi wao wanatumia lugha mama katika shughuli zao zote za kila siku zikiwemo za kiuchumi, kimila na kidini.

Zipo dalili ya lugha ya asili (lugha mama) kupotea kwa sababu watu fulani wanaona kuzungumza lugha ya asili ni ushamba na ushenzi. Kumbe kutumia lugha mama ni ustaarabu na ukweli wa utii wa kuzingatia mila na desturi njema za kabila kama vile kati ya Mgogo na Mgogo au kati ya Mbulu na Mbulu na kadhalika.

Mkinga kuoa Mkurya au Mfipa kuolewa na Myao si vibaya, ni njia moja wapo ya kuimarisha umoja, utaifa na kukuza Kiswahili. Jambo la maana na muhimu ni wazazi hawa kumfunza mtoto wao lugha zao. Kikurya au Kikinga ndiyo lugha mama, binti au mwana afunzwe.

Tukumbuke taifa lisilo na utamaduni ni taifa lililokufa. Utamaduni ni kielelezo cha utashi na uhai wa taifa katika maisha ya kila siku ya watu wake. Tuthamini na kutumia lugha mama.

Please follow and like us:
Pin Share