S

alamu zenu waungwana ambao naamini wengi wenu mnaosoma waraka wangu ni wale wenye umri wangu na kweli mnakumbuka pamoja na mimi.

Nawapa salamu kwa sababu naamini kuwepo kwetu mpaka leo ni kwa neema tu na matunzo tuliyopata kutoka kwa wazazi wetu, wazazi ambao hawakupata mafunzo ya malezi kutoka mahali popote zaidi ya kujitegemea na kutumia mbinu za asili.

Hawakuwa wachawi kama ambavyo wengi wanaamini, kwa maisha yetu tulitumia tiba mbadala nyingi hata katika mambo mazito ambayo leo yanahitaji upasuaji na mengine hata kupelekwa India kwa matibabu ya kisasa.

Sisi ilikuwa ukivunjika, kuna vitu unapakwa na kufungwa kwa maganda ya miti maalumu kwa muda mfupi, maradhi kama meno na tumbo yalikuwa yakihitaji muda mfupi kuyamaliza.

Kulikuwa na waganga wa kienyeji wa kweli, kulikuwa hakuna waganga wa kienyeji wachawi, waganga ambao wanaomba ng’ombe na kuku weusi.

Kulikuwa hakuna waganga wanaoomba mchanga wa kaburi wala koromeo la binadamu, kulikuwa hakuna waganga wanaoomba sehemu za siri za watoto au kuwa na dawa za kuongeza akili, nguvu za kiume, vyeo na hata uongozi.

Yapo mengi sana ya kukumbuka, hasa katika nyuga mbalimbali za maisha, na sijui yanatufundisha nini kwa maisha haya ya leo na kizazi hiki cha dotcom, kizazi ambacho kinaishi maisha ya Instagram, Twiter, Facebook na sinema za Ulaya, ni kizazi cha kina ‘Junia’ wengi wasiotaka kujifunza uhalisia.

Ni kizazi ambacho kinalishwa mambo mengi kutoka katika mitandao ya kijamii na mambo mengi hayana uhusiano na maisha yetu ya asili, ni kizazi cha kujifunza mambo mengi kwa wakati mmoja na kuwa na walimu wengi kuliko sisi, ni kizazi kinachojifunza mitaani zaidi kuliko shuleni na wazazi.

Enzi zetu nakumbuka watangazaji wa redio hawakuwa kama hawa wa leo, watangazaji wetu walikuwa wanachagua jambo la kuongea, walikuwa wanafundisha, hawatupotoshi, walikuwa wanaonya na kutufurahisha.

Yeyote wa zamani pasi na shaka atakubaliana nami, na ndiyo maana nikikumbuka majina yao na vipindi vyao natamani kulia, najiona mdogo nikisikiliza lakini dunia inakwenda kasi ghafla na kujiona mzee katika ulimwengu mpya usiojulikana.

Wakati wetu wa maisha ya ujamaa na kujitegemea nazikumbuka hotuba za viongozi wetu wa jembe na nyumba, hotuba zilizokuwa zimesheheni uhamasishaji wa kufanya kazi na kujitegemea.

Hotuba zilizokuwa na matokeo chanya kwa maisha yetu ya wakati ule, hotuba zilizokuwa zikijirudia vichwani kwa sababu ya ari zake. Sikumbuki hotuba ya matusi na kuchambana kama iliwahi kutolewa, sikumbuki mipasho, ila nakumbuka mwisho wa hotuba wote tuliimba nyimbo maalumu za chama na kupongezana sisi kwa sisi.

Nakumbuka nyimbo zetu na za bendi zetu za wakati ule, kwanza hakuna bendi ambayo ilitunga wimbo uliokwenda tofauti na fikra zetu, nyimbo nyingi zilipigwa na kurekodiwa baada ya kuhaririwa.

Wanamuziki wetu walikuwa na vipaji maalumu vya kufanya kazi nyingine na muziki ulikuwa ni starehe baada ya kazi, leo ni vitu viwili tofauti, muziki ni kazi na mimi sipingi, nakubaliana na mabadiliko haya.

Wakati wetu kuwa mtumishi wa umma ilikuwa sifa ya kuaminika kwako katika jamii, mtumishi wa umma alikuwa na picha zaidi ya moja ambayo anaibeba, alikuwa kioo cha jamii katika kilimo, ufugaji, usafi na nidhamu miongoni mwa jamii inayomzunguka.

Wakati huo ukiambiwa huyu ni mwalimu, anabaki kuwa mwalimu hata kwa matendo yake. Hali kadhalika askari na daktari na wengine wote waliokuwa watumishi wa umma, sina hakika kama wote walikwisha kustaafu na matendo yao bila kuwarithisha waliowaacha.

Nayakumbuka sana mashirika yetu na viwanda vyetu, na hapa ndipo ninapotambua kuwa zamani tulikuwa na maendeleo kabla ya kuingia katika ulimwengu wa vita ya kiuchumi kama ni kweli, kiasi cha kuanza kufikiria wawekezaji ambao walikuja kuwekeza mambo tofauti kabisa.

Kiwanda kinageuka kuwa godauni na shirika linakufa na kuwa na madeni mengi baada ya mwekezaji kuchukua alichokuwa anakihitaji, haya ndiyo mambo ninayokumbuka, najua wengi mnakumbuka kuliko mimi na tujiulize tulikosea wapi? Au ndicho kiitwacho uzalendo?

Wasalamu, 

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.

By Jamhuri