Wakati kampuni ya Coca Cola inaanza iliuza chupa 25 tu za soda ndani mwaka mzima! Hii inaonyesha kuwa kila mwezi waliuza takribani chupa mbili za soda.

Najua umeshangaa maneno niliyoanza nayo hapo juu, lakini hiyo ni historia ya kweli.

Leo hii Coca Cola ipo kila mahali. Ni kampuni ambayo imeweza kudumu muda mrefu ukilinganisha na kampuni nyingi duniani tangu kuanzishwa kwake katika karne ya 19, leo hii tupo karne ya 21.

Coca Cola inakadiriwa kuuza chupa za vinywaji zaidi ya bilioni 1.7 kwa siku. Na imefika katika nchi zaidi ya 200 duniani. Matajiri wakubwa kama Warren Buffet wamewekeza katika kampuni ya Coca Cola. Kila mtu anaifahamuCoca Cola. Karibu kila kona ukipita utakutana na bango au tangazo la Coca Cola, kwenye televisheni, redio, mitaani na kadhalika. Inawezakana hata wewe leo hii umejiwekea lengo la kupata mlo wako wa mchana ukishushia Coca cola baridi.

Tujifunze nini kutoka kwa Coca Cola? Kitu cha kwanza na cha msingi ambacho inatupasa kujifunza hapa ni ukitaka kuacha kumbuka kwanini ulianza.
Watu wengi wanakuwa na ndoto kubwa wanapoanza kufanya kitu fulani, mfano biashara, kazi fulani, anasomea kitu fulani, lakini baadaye ndoto zao huyeyuka kama mshumaa. Malengo yao yanapotea.

Ulipokuwa unaanza ulikuwa na sababu milioni za kufanikiwa, lakini leo hii unaona milima tu. Hebu rudi nyuma tazama zile sababu zilizokusukuma kuanza kufanya kile unachokifanya. Ingawa huoni kama umepiga hatua inakupasa ukomae na usikate tamaa. Safari ya kuanza na chupa 25 ndani ya mwaka mzima kwa Coca Cola hadi kufikia chupa bilioni 1.7 kwa siku iwe fundisho kubwa kwako.

Inawezekana mwaka huu uliona ni mwaka wa neema kwako, lakini hadi leo hii unaona balaa tupu. Ngoja nikwambie rafiki yangu. Miezi iliyobaki inaweza kuwa miezi yenye maajabu makubwa sana kwako kama hautaamua kukata tamaa. Kama utaweka nguvu na jitihada.

Nakubaliana na King Martin Luther Jr, aliyewahi kusema “Ukishindwa kukimbia, tembea. Ukishindwa kutembea, tambaa. Katika kila unachokifanya hakikisha unapiga hatua fulani.”

Pili, Jifunze kutokana na kushindwa.
Kuna somo kubwa katika kushindwa. Lakini somo hili wanalielewa wale tu wenye mtizamo chanya. Ukishindwa rudi nyuma angalia ulikosea wapi na urekebishe makosa. Waliofanikiwa wana sifa moja ya kuwa ving’ang’anizi hawajawahi kukubali kushindwa, Thomas Edison alishindwa kutengeneza balbu ya umeme zaidi ya mara elfu moja, lakini hatimaye alifanikiwa na leo hii anaitwa Baba wa Umeme duniani. Je, wewe umeshindwa mara ngapi na kujiona hufai na umekata tamaa? Inawezekana mara moja. Ukianguka simama tena.

Tatu, Wakati mambo yanapokuwa magumu ndio wakati yakupasa wewe kusimama imara. Robert Schuller, mchungaji na mwandishi mashuhuri wa vitabu aliwahi kusema, “Nyakati ngumu hazidumu, lakini watu wagumu hudumu.” Hivyo unahitaji kupiga moyo konde na kuendelea na kile unachokifanya.

Wakati kama huu ndipo utakapokutana na maneno mengi ya kukurudisha nyuma. Watu watakutukana na kukwambia “Tulikwambia jambo hilo haliwezekani.” Lakini mimi nakwambia “Jambo hilo linawezekana.” Maji yale yale ya moto ambayo hufanya kiazi kuwa laini ndiyo hufanya yai kuwa gumu.

Hakuna kitu kinachopatikana kirahisi. Mafanikio yoyote yanahitaji jitihada. Mafanikio hayana lifti kwamba upande ufike mapema unapotaka kufika. Mafanikio yana ngazi ambazo unahitaji kuzipanda. Ukitaka kufanikisha ndoto zako lazima ukubali kulipa gharama.

Kumbuka, Nuhu alijenga safina ndani ya miaka 120 bila kuona hata tone la mvua. Watu waliokaa naye karibu walimcheka na kumkebehi wakimwona mpumbavu wa kutupwa. Kipindi hicho mvua hata zilikuwa hazinyeshi kwani Mungu alikuwa akimwagilia mimea na maji yaliyotoka chini ya ardhi yakipanda juu. Nuhu aliishi mamia ya maili kutoka bahari ilipokuwa (inawezekana hakuwahi kuiona bahari), lakini hakukata tama. Alikuwa mtu mwenye msimamo na hatimaye aliimaliza safina.

Watoto wake pia walimshangaa wakiona baba yao kama anapiga ngoma kwenye maji wakisema “Baba anatengeneza kitu gani miaka 120 hata tone la mvua hatujawahi kuliona!” Coca Cola iwe fundisho kubwa kwetu.Ukitaka Kuacha, Kumbuka Kwanini Ulianza.

Please follow and like us:
Pin Share