MAISHA NI MTIHANI (31)

Nyota njema huonekana pia jioni

Namna ya kumaliza ni mtihani.  Hoja si namna unavyoanza, hoja ni namna unavyomaliza. “Kuanza vizuri ni jambo la kitambo; kumaliza vizuri ni suala la maisha yote,” alisema Ravi Zacharias – mtunzi wa vitabu. Mwanzo unaweza kuwa mbaya lakini mwisho ukawa mzuri. Lakini kuna uwezekano mwanzo ukawa mzuri na mwisho ukawa mbaya.

“Afadhali taabu zianze, za mwishoni zinaumiza.” (Methali ya Wahaya). Maana ya methali hiyo ni afadhali taabu za ujana, za uzeeni zinaumiza. Mwisho mzuri ni jambo zuri. Kwa kawaida watu husifia mwanzo mzuri. Sifa hizi zinajitokeza katika methali zifuatazo: Nyota njema huonekana asubuhi; atakayekula vizuri huonekana wakati wa kunawa; kuku atakayekuwa jogoo humulikwa akiwa bado kwenye yai. Kusema kweli, wakati mwingine nyota njema huonekana jioni.  Nyota njema inaweza ikapotea mwanzoni mwa shughuli, mwanzoni mwa safari, wakati wa ujana na ikaonekana mwishoni mwa shughuli au uzeeni.

Franklin Delano Roosevelt alikuwa Rais wa 32 wa Marekani kuanzia mwaka 1933 hadi 1945. Akiwa na umri wa miaka 39 alipatwa na ugonjwa wa polio uliomfanya kupooza. Licha ya hali hiyo nyota njema ilionekana jioni – aliweza kuongoza Marekani kwa mihula minne. Ni huyu aliyesema: “Nafikiri tunafikiria sana juu ya bahati njema ya ndege aamkaye asubuhi sana na hatufikirii bahati mbaya ya mnyoo huamkao asubuhi sana.”  Kuna mwanzo mzuri kwa ndege anayeamka asubuhi na mapema na kupata mnyoo kama mkate wake wa asubuhi. Lakini kwa mnyoo ulioliwa na ndege asubuhi nyota njema haionekani asubuhi.  Juu ya kumalizia rais huyu alisema: “Ukifikia mwisho wa kamba yako, funga fundo na ning’inia kwenye fundo.” Kwa kifupi usikate tamaa.

Henry Martin Ford alikuwa mhandisi na mfanyabiashara wa Marekani (1863 – 1947). Ni mwanzilishi  wa Kampuni ya Ford Motor Company. Alianza kutengeneza magari mwaka 1896. Alishindwa na kufilisika mara tano kabla ya kufanikiwa. Nyota njema kwake haikuonekana asubuhi. Lakini ilionekana baadaye. Alituachia maneno yafuatayo ya busara: “Huwezi kujijengea jina kwa lile ambalo utafanya.” Suala hapa ni kutenda na kufanya na kutekeleza mipango uliyonayo. Kwake, “kushindwa ni fursa tu ya kuanza upya, wakati huu kwa akili zaidi.”

Christiano Ronaldo dos Santos Aveiro aliyezaliwa Februari 5, 1985 Madeira, Ureno aliwahi kusema: “Nilimwambia baba yangu tutakuwa na mali na utajiri mkubwa wakati tukiwa katika ufukara mkubwa lakini hakuamini, leo hiyo ndiyo hali halisi.”

Ni huyu aliyesema: “Upendo wako unanifanya niwe na nguvu, chuki yako inanifanya niwe asiyeweza kusimamishwa.” Usiwasikilize wanaokuchukia bali chuki yao dhidi yako iwe motisha. Maneno yake yanatusaidia kujua namna ya kumalizia mambo: “Hatutaki kuzungumzia ndoto zetu, tunataka kuzionyesha.” Usiwaambie watu unalotaka kufanya, acha waone unalifanya.” Dk. Theodor Seuss Geisel (1904-1991), mwandishi wa vitabu na mchoraji wa katuni ni mfano wa mtu ambaye nyota yake ilionekana jioni, yaani baadaye. Kitabu cha Dk. Seuss cha kwanza cha watoto kilikataliwa na wachapishaji 23. Mchapishaji wa 24 aliyekikubali aliuza nakala milioni sita. Alimaliza vizuri.

Kama una ujasiri wa kuanza kuwa na ujasiri wa kumaliza. Wazo lolote unalolifanyia kazi, hakikisha unafuatilia mwisho wake. Kuwa na ramani ya namna ya kumaliza ulilolianza. Wewe si bahati mbaya. Wewe si ajali. Mungu ana mipango nawe. Hoja si umeanzia wapi? Hoja unaishia wapi?