MAISHA NI MTIHANI (38)

Malezi ya mama ni mtaji wa watu mashuhuri

Umama ni mtihani. Kila nyuma ya mtu mashuhuri kuna mama makini. Mama ni mzaa chema, lakini kila nyuma ya mshika mkia kuna mama mzembe au hakuna mama.

“Mungu asingeweza kuwa kila mahali, hivyo aliumba kina mama.” Ni methali ya Wayahudi ikisisitiza umuhimu wa mama.

Kina mama ni watengenezaji wa historia, cha kusikitisha wanawake wengi hawaishi muda mrefu kuona matunda ya kazi yao. “Kila mama ni kama Musa. Haingii nchi ya ahadi. Anaandaa dunia ambayo hataiona,” alisema Papa Paul VI.

Mama wa mwanasayansi Sir Isaac Newton, Bi. Hannah Ayscough, alisali kila mara na mtoto wake na kumwombea kila siku ya Mungu. Akiwa kwenye kitanda cha mauti alisikitika sana kwamba anamuacha mtoto wa miaka saba kwenye huruma ya dunia yenye machafuko.

Lakini Newton alisema: “Nilizaliwa kwenye nyumba ya mama mcha Mungu na nilitolewa kwa Mungu katika utoto wangu.” Mchango wa mama mcha Mungu ni mkubwa. Inasemwa kuwa mama mcha Mungu ni zaidi ya wachungaji mia moja.

Mheshimiwa Winston Churchill (aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa Vita ya Pili ya Dunia) alipoletewa muswada wa maisha yake, alitazama kwenye orodha ya walimu waliomfundisha, alisema kuwa anakosa mwalimu mkubwa katika maisha yake, yaani mama yake.

Juu ya mama yake alisema: “Mama yangu, kwangu alikuwa ni kama binti mfalme kwenye hadithi ambaye huwa na nguvu za ajabu: alikuwa ni mtu mwenye furaha usoni, mwenye utajiri na nguvu visivyo na kipimo. Alimetameta kwa ajili yangu kama nyota ya jioni, nilimpenda sana.” Mama yake aliitwa Bi. Lady Randolph Churchill.

Abraham Lincoln alisema: “Si mtu maskini ambaye ana mama mcha Mungu.” Juu ya mama yake alikuwa na haya ya kusema: “Jinsi nilivyo au ninavyotumaini kuwa ni kazi ya mama yangu.”

Mama yake alikuwa mtu wa sala, juu ya hili Abraham Lincoln alisema: “Nakumbuka sala za mama yangu na zimenifuata kila mara, zimening’angania maisha yangu yote.”

George Washington alikuwa na haya ya kusema juu ya mama yake: “Jinsi nilivyo ni kazi ya mama yangu. Sababu ya mafanikio yangu yote ni elimu ya kimaadili, kiakili na kimwili niliyopokea kutoka kwake.”

Mama yake alimfundisha tunu za Biblia za maadili ya kisiasa na kijamii ambazo zilimsaidia kulijenga taifa. Familia ilisali mara mbili kwa siku na kusoma maandiko matakatifu kila mara.  Mama yake aliitwa Mary Ball Washington.

Msomi Augustino wa Thagastre, Algeria (354-430) alibadilika na kuwa mcha Mungu kwa maombezi ya mama yake Monica. Monica alikuwa ameolewa na Patrisio, Monica hakuchoka kumwomba Mungu kusudi Augustino aongoke, alimwaga machozi chungu nzima yaliyolowesha ardhi kwa ajili yake.

Askofu mmoja alimwambia Monica: “Mtoto wa machozi hayo hatapotea.” Alifia Ostia (Italia) wakati alipokuwa anatoka kumtafuta mtoto wake. Augustino alikuwa Mkristo akiwa na miaka 33, padri akiwa na umri wa miaka 36, na askofu akiwa na umri wa miaka 41. Aliandika vitabu vingi vya theolojia.

Mama wa mtu mkubwa hana pembe, ni wa kawaida. Mtoto hakui kwa mama yake. Tuwape heshima mama zetu. Mama yako ni mama yako, hata akiwa na miguu midogo (methali ya Malawi).  Kumbuka unapozaliwa maisha hayakupi kanuni bali mama. Lugha yako ya kwanza inaitwa ‘lugha mama’.