Badili picha mbaya kuwa picha nzuri

Kuna wanaoona miiba kwenye ua waridi na kuna wanaoona waridi kwenye miiba. Penye ubaya kuna jambo jema limejificha, penye ugumu kuna furaha imejificha, penye matatizo kuna fursa zimelala.

Uwezo wako wa kubadili picha mbaya na kuonekana kuwa picha nzuri ndio utakufanya uishi maisha yenye furaha na amani.

“Maisha yanapokupatia limau, tengeneza juisi ya limau,” alisema Joan Henrietta Collins. Limau ni kitu kinachoonekana kidogo na hakina thamani lakini juisi ya limau ina thamani. Ukienda sokoni utauziwa limau moja shilingi mia moja au mia mbili lakini hauwezi kuuziwa juisi ya limau shilingi mia moja.

Ili chuma kiwe chuma cha pua hupitishwa katika moto mkali, vivyo hivyo katika kupitia magumu kuna watu wamejua thamani yao halisi. Wanasema bahari shwari haitoi wanamaji hodari, anga lililotulia halitoi rubani aliyebobea, barabara nzuri haitoi dereva mbombezi.

Kuna watu wamebadili picha mbaya na kuifanya picha nzuri.

Tairi bovu la gari sasa linaweza kutengenezwa kiatu, pia kuna watu nimeona wanatumia matairi hayo kutengeneza mapambo na kuyatumia kama viti, ambapo matairi hayo hupakwa rangi na kurudishiwa thamani, ukiyaona hauwezi kusema ni matairi mabovu yaliyoharibika. Kuna wengine wanachukua chupa tupu za divai na kuzibadili kuwa mapambo.

Hawa ni watu ambao maisha yanawapa limau, wao wanatengeneza juisi ya limau. Picha mbaya sasa inabadilishwa na kuwa picha nzuri. Kabla ya Yesu kuwapo kifo cha msalaba kilikuwa kifo cha aibu sana. Watu waliofanya makosa kama wizi, ubakaji na mauaji walisulubiwa msalabani. Lakini Yesu aliposulubiwa msalabani aliubadili msalaba na kuwa alama ya wokovu. Yesu aliibadili picha ya msalaba. Hadi leo hii watu wanauona msalaba kama ishara ya wokovu.

Ili kubadili picha mbaya kuwa picha nzuri, anza kwa kubadili kile unachoamini ndani yako. Siku zote hauwezi kufanya zaidi ya kile unachokiamini.

Siku moja kijana mmoja alitembelea mji fulani, baada ya kutembea umbali mrefu alihisi kiu. Akaamua kwenda mahali kulipokuwa na kisima ili apate maji ya kupoza kiu yake. Kwenye kile kisima alizoea kukaa mzee mmoja wa makamo.

Alipofika pale kisimani alimuuliza yule mzee: “Watu wa mahali hapa wakoje?” Yule mzee alijibu akisema: “Ulikotoka watu wakoje?” Yule kijana akasema: “Nilikotoka watu ni wakarimu, wanapendana, wema na marafiki wa kila mtu. Niliumia nilipotoka mahali kule.” “Utakuta watu kama hao mahali hapa,” alijibu yule mzee.

Siku hiyo hiyo kijana mwingine alipita katika kisima kile kukata kiu yake akitokea barabarani. Alipomuona mzee yule alimsalimu na kusema: “Watu wa mahali hapa wakoje?” Mzee yule aliuliza pia swali kama la mwanzo: “Na ulikotoka watu wakoje?” Kijana yule akajibu akisema: “Watu wengi wanaojipendelea na wenye mawazo mabaya.” Yule mzee akasema: “Utawakuta watu kama hao mahali hapa.”

Mtu mmoja aliyesikia mazungumzo hayo mawili aliuliza: “Kwanini ulitoa majibu tofauti kwa swali linalofanana?” Mzee yule akasema: “Yule ambaye hajaona jambo lolote zuri moyoni mwake hawezi kukuta jambo lolote zuri mahali popote.”

Nakubaliana na Sunday Adelaja aliyewahi kusema: “Yeyote anayeufanya moyo wake kuwa mgumu, hauwezi kuiona dunia kama sehemu nzuri.”

Badili picha mbaya ya wazo lako kuwa picha nzuri. Nnamdi Ezeigbo ni raia wa Nigeria aliyekuwa na wazo la kutengeneza simu za laini mbili. Wazo lake alilipeleka katika Kampuni ya Nokia na likaonekana kama wazo bovu. Wakati huo mtu kutembea huku ameshikilia simu nyingi zenye kutumia laini moja ulikuwa ni ufahari.

Baada ya wazo hilo kukataliwa, Nnamdi alikutana na Mchina mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya kutengeneza simu iliyojulikana kama BIRD. Walikwenda wote Nigeria, baada ya hapo simu aina ya TECNO ziligunduliwa. Sikumbuki mara yangu ya mwisho kuona simu ya Nokia ni lini lakini mara yangu ya mwisho kuona simu ya TECNO ni jana. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba Nnamdi Ezeigbo pia ni mmiliki wa Kampuni ya Infinix.

Madini yenye kina kirefu huchimbwa chini kabisa ardhini, ni katika kujitafuta na kujua kwa undani wewe ni nani na umezaliwa kufanya nini, ndipo utakapoweza kuibadili picha mbaya na kuwa picha nzuri. Maisha yanapokupatia limau, tengeneza juisi ya limau. 

815 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!