Ujinga ni pepo la mabwege. Ndivyo Mpita Njia (MN) anavyoanza kwa kusema.

Anasema hivyo kwa sababu tangu serikali itangaze uwepo wa wagonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, baadhi ya watu wanajitoa akili na kuleta mizaha mbele ya ugonjwa huo.

Akiwa mitaani, MN amewasikia wananchi wakijinadi kuwa virusi vya corona haviwezi kuwadhuru kwa sababu eti havikutengenezwa kwa ajili yao. Ni nani kawaambia kuwa vimetengenezwa?

Utawasikia wakijitapa eti tangu kutangazwa kuwapo ugonjwa huo nchini hakuna kifo kilichoripotiwa. Watanzania bwana! Furaha yao ni kuona watu wakifa au?

Eti ugonjwa huu ni kwa ajili ya ngozi nyeupe, kwamba mbele ya ngozi nyeusi utadunda tu. Huko ni kujidanganya.

Imani hiyo potofu na ya kijinga inamfanya MN aamini kuwa watu wamepotoka na kupuuza wanayoelekezwa na wataalamu wa afya kujikinga na virusi hivyo.

Kinga ni bora kuliko tiba, ila MN anayoyaona jijini Dar es Salaam ni kama watu wamebadili tiba kuwa ndiyo bora kuliko kinga! Mbele ya corona tutakwama. Tutakuwa tumechelewa.

Muda wa kugombania mashine moja ya hewa Mloganzila kwa wagonjwa 200 hautatosha. Watapona wachache. Mungu aepushie mbali. Kwanini MN anasema hivyo? Uhalisia unaonyesha katika mataifa ambako virusi vya corona vinasababisha maafa makubwa, dalili kwa walioambukizwa zilianza kujionyesha kati ya wiki mbili hadi tatu tangu ulipoingia kwao.

Baada ya hapo mambo yalibadilika, hali ikawa mshikemshike. MN anasema Tanzania isifikishwe huko na wapuuzi wachache wanaotaka kuutumia ugonjwa huo kukuza majina yao. Huu si muda wa kuaminishana ujinga. Ni muda wa kuhimizana kuchukua tahadhari na umakini mkubwa. Ni muda wa kuelekezana kwamba saa za masihara zimekwisha. Corona imetoka China sasa ipo kwetu, tunafanyaje?

Wanaojitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba wamepatwa na corona wapuuzwe kabisa, hao wanataka kuleta mazoea kwenye vitu hatari. Wapuuzwe kabisa, hizo ni mbwembwe na maono dhaifu juu ya gonjwa hili hatari.

Hali itakapobadilika na kuwa kinyume, MN anaiomba serikali iwakamate hao wanaoleta masihara na kuwafungulia mashitaka kwa kusababisha watu kuupuuza.

Ule umakini ulioonyeshwa na watu siku mbili za mwanzo ulipotangazwa kuwapo nchini umepungua na kinachoupunguza MN amebaini ni mizaha na ujuaji kwenye mitandao ya kijamii.

MN anashauri TCRA kuanza kuwachukulia hatua wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kukejeli hata tahadhari na hatua zinazohimizwa na serikali.

994 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!