Nianze waraka wangu kwa kuwakumbusha kuwa sasa ni rasmi tunaelekea kuugawa mwaka, wenye malengo yao naamini wanafanya tathmini walipo na wale ambao walisherehekea mwaka kwa kuangalia tarehe, labda hawana chochote cha kufanyi tathmini zaidi ya kusubiri tarehe ya mwaka mpya.

Leo kumekucha na makucha yake. Nilikuwa na furaha sana asubuhi hii mpaka nilipokerwa na dereva mmoja aliyenipa lifti kwa kuniamrisha nifunge mkanda katika gari lake huku akielezea maana ya kufunga mkanda kwa faida ya usalama wangu.

Nilikubaliana naye nikafunga mkanda, wakati tukiendelea na safari aliendelea kunisimulia jinsi maisha yake ya kuendesha gari yalivyopitia misukosuko mingi ya kupigwa faini mbalimbali ikiwamo ya kutofunga mkanda na kuvuka katika alama za pundamilia.

Kwa hakika nilimuelewa na nilimuonea huruma sana huku nikitafakari hatua ambazo katika suala la usalama barabarani naona kama tunalivalia njuga katika mazingira ambayo labda tumeyapokea kwa haraka bila kufanya tathmini sawasawa.

Wakati tunaendelea na safari nilianza kuangalia mambo yanayokinzana na sheria yenyewe ambayo dereva huyu yamemfanya ajutie kuingiza gari barabarani na kupigwa faini, japo nilijua umuhimu wa sheria yenyewe lakini nikawa ninajiuliza mambo machache sana.

Hivi hawa waendesha pikipiki ambao wanatupita kwa kasi na ambao hawajavaa kofia ngumu za pikipiki na badala yake wamevaa kofia za ujenzi wa majengo wanafungaje mkanda? 

Hivi hawa waliomo katika magari ya mizigo na wamekaa nyuma ya gari na wanatupita wamefungaje mikanda yao?

Ndipo nikakumbuka baadhi ya sheria zingine ambazo tumezigeuza na kutungiwa kanuni kama vile aliyesema ugali unatakiwa kuwa mkubwa ila mboga inatakiwa kuwa ndogo ni nani? 

Aliyesema mlango wa sebuleni ni fasheni lakini tunapita mlango wa jikoni ni nani? Na nani aliyesema sikukuu lazima tuvae nguo mpya na kula vizuri?

Nikaona baadhi ya mambo yanatokana na mazoea. Ni kweli kwamba kufunga mkanda ni muhimu katika gari lakini swali ni katika mwendo gani? Hivi kwa foleni ya mjini ambako mtu anatumia nusu saa kuendesha kilomita hamsini anastahili kuvaa mkanda? 

Na kama asipovaa, kwa nini busara ndogo ya kujua namna ya kumshauri badala ya kumwandikia adhabu inakosekana?

Kama suala ni mwendo na hatari ya ajali, inakuwaje abiria huyo huyo akipanda pikipiki haulizwi mkanda ila akipanda gari lazima afunge mkanda? 

Hivi hawa abiria ambao wapo katika maroli wakienda mnadani na kasi ile huwa hawaulizwi kama hawajavaa mkanda?

Najua tunafuata sana sheria na kwamba kuvuka au kupita katika kivuko cha waenda kwa miguu bila kusimama ni makosa, hivi sheria hii tumeitafsiri namna gani? Kwamba kila kivuko ambacho hakina mvukaji ni lazima kusimama? 

Dereva atasimama mara ngapi kutoka Mwanza mpaka Songea? Nini huwa kinatokea dereva akipita bila kusimama wakati hakuna mvukaji?

Zipo sheria nyingi sana ambazo naona zinasumbua japo tumezizoea, mazoea yanakuwa sheria kimyakimya na yanatunyoosha wenyewe, mimi si dereva lakini nawaonea huruma sana madereva kwa kuogopa mambo mengi sana ambayo ni ya kuchukua tahadhari.

Nikiachana na hizo sheria ambazo zinafanyiwa kazi sana, sasa najiuliza kuhusu suala la mazingira, wale jamaa wanaotumia redio za mikononi kwa kutangaza bidhaa zao wana ruhusa ya kusumbua watu wasiohitaji huduma zao? Huduma za chawa, panya na kunguni? Au huduma za nguvu za kiume na uzazi?

Kwani mipaka ya watu wa mazingira inaishia katika mifuko na chupa za plastiki tu? Kuna wale mabingwa wa kuanzisha madampo kwa hiyari yao katika sebule za watu, sheria inasemaje? Au mpaka dampo lijae ndipo kwa huruma wanaanza kushughulikia kikanuni?

Najua mimi ni bwege lakini kwa ujinga wangu ni kama nataka kukubaliana na baadhi ya sheria kwamba ziangalie kwa jicho la usasa na usomi, vipi kuhusu PF3 ambayo mpaka juzi imebatilishwa, tunadhani imegharimu maisha ya watu wangapi? Na sheria ya matunzo ya watoto hivi bado ni ile 150/- kwa mwezi?

Sishangai kuwaona watoto wa mitaani kwa sheria hiyo, sishangai kuona tuna hazina kubwa ya vibaka na wezi kwa sheria ambayo tungeibadilisha mapema tungeokoa maisha ya wengi.

Ni vema jambo ambalo linakera tusianze na mikakati na michakato inaendelea, hayo ni maisha ya wenzetu, tuwe makini sana. Tusipozuia mapema itatugharimu siku zijazo. 

Wasalamu,

Mzee Zuzu.

Kipatimo.

By Jamhuri