Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Serikali imeipongeza Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii baada ya kutoa shilingi milioni 33.6 kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wa pwani pamoja na kuhifadhi mazingira katika Jiji la Tanga.
Fedha hizo zinalenga kusaidia jamii zinazoishi karibu na Kituo cha Kuhifadhi Mafuta (Marine Tank Terminal – MTT) na gati katika Rasi ya Chongoleani, kwa lengo la kuongeza kipato huku zikihamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Bw. Dadi Kolimba, aliipongeza EACOP kwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha ustawi wa wananchi.
“Ni jukumu la Serikali kujenga uchumi wa wananchi wake, lakini tunahitaji pia wadau kushirikiana nasi katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” alisema.
“Tunaishukuru EACOP kwa kusaidia wananchi walioathiriwa na mradi (PAPs) pamoja na kulinda mazingira ya pwani yetu.”
Fedha hizo zimetolewa kupitia taasisi ya MWAMBAO Coastal Community Network Tanzania, ambayo ni mkandarasi wa EACOP katika masuala ya bioanuwai na maendeleo ya maisha, na zimegawiwa kwa vikundi 16 vya jamii vya MKUBA katika eneo la pwani la Mchomapunda.
Vikundi hivyo, vyenye jumla ya wanachama 480 kutoka Chongoleani na Putini, kila kimoja kimepokea shilingi milioni 2.1 kupitia akaunti za benki, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ujumuishaji wa kifedha.
Hafla ya makabidhiano ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Putini, Kata ya Chongoleani, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa EACOP na MWAMBAO pamoja na wanajamii walionufaika.
Meneja wa Ardhi na Masuala ya Kijamii wa EACOP Tanzania, Bw. Abraham Youz, alisema kuwa mpango huo kwa ajli ya kurejesha hali za maisha za waguswa wa mradi ni sehemu ya mradi wa miaka 4 ulioanza Mei 2024 unaojulikana kama “Biodiversity Offsetting and Livelihood Restoration for Communities of the Mchomapunda Community Fisheries Management Area.”
Alisema mradi huo unalenga kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi wa jamii huku ukilinda mazingira.
“Tuna fahari kushirikiana na jamii zilizoathiriwa na mradi kwa kusaidia kurejesha maisha yao kupitia shughuli kama kilimo na ufugaji,” alisema.
“Msaada huu unaonyesha dhamira yetu ya kuleta manufaa ya kudumu na maisha endelevu.”
Kwa upande wake, Meneja wa Utendaji wa Kijamii wa EACOP kwa Uganda na Tanzania, Bi. Rosie Birungi, alisisitiza umuhimu wa mpango huo katika ngazi ya kaya, akibainisha umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wanawake.
“Ninafurahi kuona wanawake wengi wamenufaika. Kumwezesha mwanamke ni kuiwezesha familia na jamii kwa ujumla,” alisema.
Mpango huo unaotekelezwa na MWAMBAO unalenga maeneo manne muhimu: urejeshaji wa miamba ya matumbawe, uoteshaji wa mikoko, programu ya mikopo ya kiikolojia ya MKUBA, pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAMBAO, Bw. Said Khalid, alisema mpango huo ni wa mabadiliko makubwa kwa jamii, ukiwawezesha kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira huku wakiboresha maisha yao.
“Ruzuku hizi ni mwanzo wa safari mpya. Kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na fursa za kiuchumi, tunajenga maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Wanufaika walieleza matumaini yao kuhusu msaada huo. Bi. Mwasiwa Abdallah wa kikundi cha Heri ya Moyo alisema anatarajia kupanua biashara yake ya kuuza Khanga ili kusaidia familia yake.
“Msaada huu utanisaidia kukuza biashara yangu na kuboresha maisha ya familia yangu,” alisema.
Mnufaika mwingine, Bi. Mwanaisha Salim wa kikundi cha Tupendane, alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira.
“Tumejipanga kupanda miti zaidi, kulinda mazingira na kupambana na uvuvi haramu kama sehemu ya wajibu wetu,” alisema.
Sehemu muhimu ya mpango huo ni mfumo wa mikopo ya kiikolojia wa MKUBA, unaotoa nafasi kwa jamii ya kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa bioanuwai. Mfumo huo unawawezesha wanajamii kupata kipato endelevu huku ukipunguza athari za uharibifu wa rasilimali za bahari.
Kadiri utekelezaji unavyoendelea, mpango huu unatarajiwa kuwa mfano bora wa uhifadhi unaoongozwa na jamii pamoja na ukuaji wa uchumi shirikishi katika maeneo ya pwani nchini Tanzania.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni mradi wa urefu wa kilomita 1,443 wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale, Hoima nchini Uganda hadi Rasi ya Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.
Wanahisa wa mradi huu ni TotalEnergies (asilimia 62), huku Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) na Shirika la kusimamia mafuta nchini Uganda ( UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja, huku shirika la kusimamia nishati hiyo nchini China (CNOOC) likimiliki asilimia 8.






