📌 Shule ya Sekondari Nkololo yaachana na kuni pamoja na mkaa

Bariadi, Simiyu📍

Timu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa imezindua rasmi mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Nkololo, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Mradi huo, uliozinduliwa tarehe 30 Julai 2026, una lengo la kutokomeza kabisa matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, kama sehemu ya kulinda mazingira na afya za Watu.

Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Wazo Michael Mwang’onda, aliipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji madhubuti wa mkakati huo wa serikali.

Bw. Mwang’onda alibainisha kuwa mradi huo utaleta tija kubwa kwa shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 606.

“Kupitia mradi huu, Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida. Hali hii itaboresha afya na usalama wa wanafunzi, walimu, pamoja na wapishi wanaotumia jiko hili kila siku,” alisema Kiongozi huyo.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi ya Nishati kutoka REA, Mha. Davidi Malima, alifafanua kuwa wakala huo umewekeza shilingi milioni 15 katika Shule ya Sekondari Nkololo. Fedha hizo zimefanikisha ununuzi wa majiko mawili makubwa yenye uwezo wa lita 200 kila mmoja, pamoja na usimamishaji wa tanki la gesi ya kupikia (LPG) lenye ukubwa wa tani moja.

Mha. Malima aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kitaifa unaolenga kuzifikia taasisi 453 katika mikoa yote nchini, ambapo jumla ya shilingi bilioni 25.8 zimetengwa.Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Katika kufanikisha azma hiyo, kampuni ya Taifa Gas Limited ilishinda zabuni ya kusambaza na kufunga mifumo ya gesi ya LPG kwenye taasisi, huku kampuni ya Hanny G Investment ikikabidhiwa dhamana ya kusambaza majiko banifu na masufuria makubwa kote nchini.

Utekelezaji wa mradi huu unakuja wakati ambapo takwimu za mazingira nchini zikionyesha hali ya isiyoridhisha; ambapo Tanzania inapoteza zaidi ya hekta 370,000 hadi 470,000 za misitu kila mwaka. Sehemu kubwa ya uharibifu huu inasababishwa na uvunaji wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, huku zaidi ya asilimia 90 ya kaya na taasisi nchini zikiwa bado zinategemea nishati hiyo (Kuni na mkaa wa kawaida).

Mbali na uharibifu wa mazingira, matumizi ya kuni kwenye majiko yasiyo rasmi yanasababisha uchafuzi mkubwa wa hewa ndani ya nyumba na taasisi. Moshi wa kuni unaozalisha gesi hatari za ukaa (Carbon Monoxide) na chembechembe za moshi hubeba athari kubwa za kiafya, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa upumuaji, matatizo ya macho, na hata vifo vya mapema kwa Watumiaji wa nishati hiyo