Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora imewezesha Kikundi cha Vijana cha Umoja mkopo usio na riba wa shilingi milioni 109 ambao umewasaidia kununua gari aina ya Fuso Figher 16 ili kufanya mradi wa kusafirisha madini ya ujenzi.
Mradi huo umeleta neema kubwa kwa vijana hao kwani tangu wamepata gari hilo kila siku wana uhakika wa kuingiza kiasi cha shilingi laki 5 au zaidi kutokana na usafirishaji wa madini ya ujenzi.
Akizindua mradi huo leo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Michael Mwang’onda amepongeza ubunifu wa vijana hao wa kuanzisha mradi ambao utawaingiza kipato halali na cha uhakika.
Aidha amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dk John Pima na Madiwani kwa kusimamia vizuri utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
Amesisitiza kuwa mikopo hiyo ni utekelezaji agizo la serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa wananchi wake.
‘Mikopo hii ni fursa muhimu sana kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi, ichangamkieni, lakini mkipewa hakikisheni mnarejesha kidogo kidogo ili kumaliza haraka mikopo yenu’, ameeleza.
Mwang’onda ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na serikali yao ili kuharakisha maendeleo yao, amebainisha kuwa tayari Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya sh bilioni 200 kwa ajili ya vijana nchi nzima.
Aidha Rais ametoa fursa nyingine kwa wananchi kunufaika na asilimia 30 ya tenda za ujenzi zinazotangazwa na serikali ambapo vijana pia wananufaika moja kwa moja kupitia miradi hiyo, hivyo akawataka kuzichangamkia.
Mwenyekiti wa Kikundi hicho Juma Omary Mpine ameeleza kuwa awali walichukua mkopo wa sh mil 5, awamu ya pili sh mil 10 kwa ajili ya mradi wa usafirishaji abiria kwa bodaboda na sasa wamechukua mkopo wa mil 109 na wamenunua gari.
Amebainisha kuwa kupitia mradi huo tayari wamerejesha zaidi ya sh mil 39 na wanaendelea kurejesha kidogo kidogo, hadi wamalize, mradi huo pia umetoa ajira za muda kwa vijana wenzao zaidi ya 50.


