Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Zanzibar

Wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewakutanisha wahariri wakuu wa wilaya zote za Dar es Salaam na watendaji wa mkoa huo kujadili jinsi ya kuboresha usafi katika Jiji hilo kubwa kuliko yote nchini Tanzania. Mkutano huu umekuja baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza anavyokerwa na hatua ya Jiji hilo kuwa chafu. Nilikuja Zanzibar baada ya mkutano huo, na naandika makala hii nikiwa hapa.

Sitanii, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa kila siku Dar es Salaam inazalisha maelfu ya tani za taka. Takwimu zinatofautiana, lakini baadhi ya vyanzo vinaweka kiwango cha taka kinachozalishwa kati ya tani 4,000 na zaidi ya 5,000 kwa siku. Sehemu kubwa ya taka hizi bado ni mzigo kwa jiji. Lakini je, taka lazima ziwe mzigo?

Nampongeza Mkuu wa Mkoa Chalamila kwa hatua yake hiyo ya kukutana na wahariri, lakini pia na hatua za haraka alizotangaza kuchukua, ikiwamo kuwaondoa wadogo wadogo maarufu kama wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi, ikiwamo kupanga meza Kariakoo. Amesema wazi kuwa kama ilivyo kwenye kodi kwamba kuna mlipakodi mdogo, wa kati na mkubwa, sasa itakuwa hivyo kwa maeneo ya kufanyia biashara.

Amenifurahisha aliposema meza zote zinazopanga bidhaa barabarani zitaondolewa Kariakoo. Akaongeza kuwa majengo yanayojengwa Kariakoo yameongeza nafasi za maduka, hivyo wanaotaka kufanya biashara Kariakoo wote wakodishe vyumba. Kwa kweli naunga mkono uamuzi huu, maana ilivyo sasa haieleweki lipi ni duka na lipi ni gulio. Hata kama ni wapigakura, hatuwezi kwenda hivyo. Tufike mahala tuseme imetosha.

Sitanii, nimekuwa nikitafakari jambo hili na kuangalia uzoefu wa miji mingine duniani. Nimekutana na mfano unaovutia sana wa Shenzhen, China. Huko, taka si uchafu wa kutupwa tu; ni malighafi. Katika mji huu kuna kiwanda kiitwacho Longgang Energy Ecological Park. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuteketeza tani 5,000 za taka kwa siku. Joto linalopatikana linatumika kuchemsha maji, mvuke unaendesha turbine na hatimaye kuzalisha umeme.

Mfumo huu unaonesha jambo moja muhimu: taka za mijini zinaweza kugeuzwa kuwa chanzo cha uhakika cha nishati. Hawajaishia hapo. Majivu ya chini yanayobaki baada ya uchomaji huchakatwa, nayo yanatumika kuzalisha bidhaa za ujenzi, ikiwamo matofali rafiki kwa mazingira. Gesi moshi na majivu hatarishi hushughulikiwa kwa teknolojia maalumu ili kupunguza athari kwa mazingira na afya.

Sasa turudi Dar es Salaam. Badala ya kuendelea kuona taka kama tatizo la malori, madampo na harufu, tunahitaji kujiuliza: je, taka zinaweza kuwa sehemu ya uchumi wa jiji la Dar es Salaam? Kwamba Jiji hili sasa linaweza kuamua kuwekeza, na katika bajeti zake za kila mwaka taka zikahesabiwa kama chanzo cha mapato manono kwa jiji letu?

Sitanii, katika hili tumekubaliana ni letu sote kama jamii. Si la Serikali wala watendaji pekee. Nasi wahariri tunaweza kusaidia wakiona inafaa na tupo tayari kushiriki kumaliza tatizo hili la taka. Dar es Salaam inaweza kufanya upembuzi yakinifu wa kiwanda cha awali chenye uwezo wa kuchakata tani 1,500 za taka kwa siku.

Kwa makadirio ya awali, kiwanda cha ukubwa huu kinaweza kuwa na uwezo wa kuzalisha takribani megawati 40 hadi 45 za umeme, kutegemea aina ya taka, kiwango cha unyevunyevu, thamani yake ya nishati na teknolojia itakayotumika. Huo si umeme mdogo.

Na kama Dar es Salaam itaamua baadaye kupanua mfumo kufikia uwezo wa kuchakata takribani tani 3,000 kwa siku, uwezo wa mitambo unaweza kufikia takribani megawati 70 hadi 90. Hata hivyo, takwimu hizi zinahitaji kuthibitishwa na upembuzi yakinifu kwa kutumia taka halisi zinazozalishwa Dar es Salaam.

Nafahamu, gharama si ndogo. Kiwanda cha kisasa cha kuchakata tani 1,500 kwa siku kinaweza kuhitaji uwekezaji wa mamia ya mamilioni ya dola. Makadirio ya awali yanaweza kuwa karibu dola milioni 300 hadi 500, kutegemea teknolojia, miundombinu na viwango vya udhibiti wa mazingira. Ndiyo maana nashauri Dar es Salaam isianze kwa kununua mtambo; ianze kwa upembuzi yakinifu wa kitaalamu.

Kwa kuchakata tani 1,500 za taka kwa siku, Dar es Salaam inaweza kuwa na mtambo wenye uwezo wa kuzalisha takribani MW 40–45 za umeme kama nilivyosema. Kwa makadirio ya awali, mauzo ya umeme yanaweza kuingiza Sh bilioni 45–75 kwa mwaka, kutegemea bei ya TANESCO.

Si mauzo ya umeme tu, matofali, paving blocks, aggregate na metali zinazopatikana baada ya uchakataji zinaweza kuongeza takribani Sh bilioni 3–8. Ada ya kuchakata taka inaweza kuongeza karibu Sh bilioni 16. Hivyo, mradi unaweza kuwa na mapato ghafi ya takribani Sh bilioni 64–99 kwa mwaka, huku ukisafisha jiji, kuzalisha ajira na kuongeza MW 40–45 kwenye mfumo wa umeme nchini.

Naomba nieleweke. Hapa sizungumzi siasa. Nimekwenda Shenzhen, China; kiwanda cha aina hii nimekishuhudia kwa macho yangu mwaka 2019. Tunapaswa kufanya upembuzi kubainisha Dar es Salaam ina taka kiasi gani hasa kwa uhalisia, badala ya mazoea yetu ya kusema zipo takataka nyingi.

Tuchambue na kufahamu zina thamani gani ya nishati? Tani ngapi zichomwe, ngapi zitengeneze mboji na ngapi zizalishe bidhaa mbadala? TANESCO inaweza kununua umeme huo kwa bei gani? Mradi ujengwe na Serikali au kwa ubia na sekta binafsi? Sitanii, huu utakuwa mwanzo wa kugeuza tatizo kuwa rasilimali.

Natamani kuandika zaidi, ila leo nafasi ni finyu. Eneo hili nalifahamu vilivyo. Ningependa kuona Mkoa wa Dar es Salaam ukikusanya wataalamu wa mazingira, nishati, fedha, mipango miji na sekta binafsi mezani kuchunguza wazo hili. Natamani ukutanaji huo uwe kwa mfumo wa Kikosi Kazi kitakachotoa majibu ndani ya mwezi mmoja na utekelezaji ukaanza bila kusubiri mchakato wa sheria ya ununuzi!

Badala ya kuuliza, tutazipeleka wapi taka za Dar? Tuanze kuuliza: Taka za Dar zinatutosha au SGR iwe na mabehewa ya kusafirisha taka kutoka Morogoro, Pwani na mikoa mingine kuja Dar? Usishangae. Taka ni mali. Zipo tayari. Tunakosa jambo dogo tu, UAMUZI. Kila wakati tunaambizana mchakato unaendelea. Kwa kuandika wazo hili, kuna anayewaza dili, badala ya matokeo. Tuanze sasa. Inawezekana. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827