Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kuna wakati viongozi wanapaswa kusimama juu ya tofauti zao na kujiuliza: tunataka historia itukumbuke kwa kushindana kiasi gani, au kwa kulinda taifa letu kiasi gani? Zanzibar wametupa jibu kupitia maridhiano ya CCM na ACT Wazalendo. Sisi Tanzania Bara tunashindwa nini?

Nampongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kukubali mazungumzo na kuyapa nafasi ya kuzaa mwafaka. Kusainiwa kwa tamko la pamoja na hatua ya kumuapisha Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kumeyapa maridhiano hayo sura ya vitendo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Huo ni uongozi unaostahili pongezi. Wameteuliwa mawaziri wanne kutoka ACT Wazalendo na wameingia serikalini.

Sitanii, Rais Mwinyi ameonesha kwamba kiongozi anaweza kusimamia chama chake huku akiwatambua wapinzani kuwa washirika katika ujenzi wa nchi. Kukaa meza moja hakupunguzi mamlaka ya Rais. Kunapanua nafasi ya wananchi kuamini kwamba nchi yao ina nafasi kwa wote.

Pongezi pia ziwaendee viongozi wa ACT Wazalendo. Kukubali mazungumzo kunahitaji ujasiri, hasa pale ambapo wafuasi wamebeba maumivu na malalamiko. Viongozi wanapaswa kuwaongoza wananchi kuelekea suluhisho, hata inapohitaji maamuzi magumu.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye Mwenyekiti wa CCM. Ni wazi mazungumzo haya yamefanikishwa na uongozi wake. Naye anastahili kupongezwa, hasa kwa kutilia maanani kuwa huu ni mwendelezo wa falsafa ya 4R: maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya. Alitambua mapema umuhimu wa kulirejesha taifa katika njia ya kuaminiana na kushirikiana. Huo ulikuwa msingi wenye matumaini makubwa.

Sitanii, leo najiuliza: matumaini yale yameelekea wapi? Kwa mtazamo wangu, bila hatua mpya zinazoonekana na kugusa chanzo cha migogoro, 4R zinaelekea kuishia hewani. Wananchi wanahitaji kuona maridhiano katika namna tunavyoshughulikia tofauti, tunavyosikiliza malalamiko na tunavyoheshimu haki za kila mmoja.

Ili tutoke hapa tulipo, lazima tuangalie tulipotoka. Uchaguzi wa mwaka 2020 uliacha malalamiko makubwa kuhusu kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani. Migogoro ya uteuzi na hisia za kutotendewa haki viliongeza ufa wa kisiasa. Ufa huo hauwezi kufunikwa kwa kauli za kutaka watu wasahau yaliyopita.

Malalamiko kuhusu wagombea kuambiwa hawajui kusoma na kuandika yanahitaji kuchunguzwa kwa ushahidi wa kila tukio. Hoja pana, hata hivyo, ni nzito: mwananchi anapoamini kwamba mgombea wake ameondolewa kwa sababu isiyo ya haki, imani yake katika uchaguzi inayumba. Tunapaswa kujibu malalamiko hayo kwa uwazi.

Mwaka 2025 tulifikia hatua nyingine ngumu. CHADEMA ilishikilia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi bila mageuzi; kutosaini kanuni za maadili kulifuatiwa na kuondolewa kwake katika ushiriki. Katika kipindi hicho, Tundu Lissu alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini. Mlolongo huo ulizidisha mvutano badala ya kuutuliza.

Hadi ninapoandika makala hii, sijafahamu matokeo ya hukumu itakayotolewa na Mahakama Kuu katika kesi ya Lissu. Sitabashiri uamuzi wa mahakama. Lakini ninachosema bayana ni hiki: iwe Lissu ameshinda au ameshindwa, pande zote mbili zirudishe moyo.

Uamuzi wowote usigeuzwe kuwa sababu ya kushangilia maumivu ya wengine, kulipizana kisasi au kuongeza uhasama. Wanaoridhika na uamuzi wawe na kiasi; wasiokubaliana nao watumie njia za kisheria. Wote waendelee kuona thamani ya kuishi pamoja.

Sitanii, CCM na CHADEMA waone fahari kujenga taifa lenye amani na haki. Ushindani wao uwe wa sera, hoja na uwezo wa kutatua shida za wananchi. Watanzania wanahitaji ajira, huduma bora, usalama na nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

Ninawasihi viongozi wa pande hizi wakubali kukaa meza moja. Zanzibar wameonesha kwamba mazungumzo yanawezekana hata baada ya tofauti nzito. Bara tunaweza kujifunza ujasiri huo na kuutumia katika mazingira yetu.

Mazungumzo yawe na ajenda zinazoeleweka: malalamiko ya uchaguzi, mageuzi ya kisiasa, haki za wananchi na namna ya kujenga tena imani katika taasisi. Yawe na ratiba, uwakilishi unaoaminika na utaratibu wa kufuatilia utekelezaji. Wananchi waone kinachobadilika.

Wakati tukisubiri matokeo ya Tume ya Uchunguzi wa Kijinai inayoongozwa na Jaji Shaban Ally Lila, nchi ianze hatua za awali za kurejesha umoja wa kitaifa. Tume hiyo inachunguza wahusika na ukiukwaji wa sheria katika matukio ya wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Sitanii, mazungumzo yasisubiri matokeo ya uchunguzi. Uchunguzi unaweza kuendelea huku viongozi wakifungua milango ya kuaminiana. Ukweli na uwajibikaji vipewe nafasi, sambamba na juhudi za kuponya majeraha ya taifa.

Rais Samia ana nafasi ya kuzipa 4R nguvu mpya. CCM na CHADEMA wana nafasi ya kuonesha kwamba maslahi ya Tanzania yanatangulia fahari ya chama. Hatua ya kwanza inaweza kuwa ndogo: kukutana, kusikilizana na kukubaliana namna ya kuendelea. Viongozi wa vyama hivi wanaweza kukutana tu, wakanywa chai kama hatua ya kwanza, baada ya hapo waanze kuzungumza masuala ya nchini kwa uzito wake. Inawezekana, tuanze sasa. Zanzibar wameweza. Sisi Bara tunashindwa nini? Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827