Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Morogoro

Watanzania wenzangu, kuna wakati taifa linapaswa kusimama na kujiuliza: tunataka kutumia muda wetu mwingi kujadili nani amesema nini, nani amegombana na nani na nani anastahili cheo gani, au tunataka kujadili namna ya kutengeneza fedha, ajira kwa vijana na uchumi imara kwa taifa letu?

Sitanii, nimejiuliza swali hili baada ya kusikia taarifa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwamba kwa sasa bandari zetu zinahudumia shehena ya takribani tani milioni 33, huku lengo likiwa kufikia tani milioni 62 mwaka 2031.

Hili si jambo la kupita nalo kama taarifa ya kawaida. Hapa kuna karibu mara mbili ya mzigo tunaoushughulikia sasa kama nchi. Mzigo huu utahitaji malori, madereva, maghala, mawakala wa forodha, kampuni za usafirishaji, bima, benki, hoteli, migahawa, mama na baba lishe, mafundi, teknolojia na huduma nyingine nyingi.

Swali langu kwa Watanzania ni moja. Je, tunajiandaa? Nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa. Kazi inayofanyika katika bandari zetu ina maana kubwa kuliko meli kuingia na kutoka. Bandari ikifanya kazi vizuri, uchumi unasogea mbele. Shehena ikiongezeka, biashara inaongezeka, ajira zinaongezeka na Serikali inakusanya mapato zaidi.

Lakini vijana wetu wakibaki mitandaoni wakibishana kuhusu siasa kuanzia asubuhi hadi usiku, hizo tani milioni 62 zitafika? Jibu ni hapana. Zitabebwa na wengine, fedha itatengenezwa na wengine, halafu sisi tutabaki kuulizana kwa nini hatuna ajira. Tutarudi katika ndoto ya kuwaza kuwa Serikali ‘itutetee’. Hapo ndipo ninaposema Bandari ni njia, TRA ni njia, lakini mwisho wa yote uwe uchumi wa Mtanzania.

Nimpongeze pia Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda. Kuna jambo kubwa limefanyika katika ukusanyaji wa mapato chini ya uongozi wake. TRA imefikia hatua ya kuvuka Sh trilioni 4 kwa mwezi. Desemba 2025 ilikusanya Sh trilioni 4.13, rekodi ambayo haikuwa imewahi kufikiwa kwa mwezi mmoja. Mwaka wa fedha 2025/26, makusanyo yalifikia Sh trilioni 37.957. Haya ni mafanikio makubwa.

Kinachonivutia zaidi ni mabadiliko ya falsafa ya ukusanyaji. TRA sasa inatumia mifumo, teknolojia, ushirikiano na ustaarabu badala ya kumwona mfanyabiashara kama adui. Serikali inahitaji kodi, lakini mfanyabiashara ndiye anayezalisha kodi hiyo. Ukimuua kibiashara mfanyabiashara leo, kesho utamtoza nani kodi?

Sitanii, hapa nina hoja nyingine. Tanzania ianze mjadala wa namna ya kuwalinda watendaji mahiri. Nafasi za kisiasa zinaweza kuwa na ukomo wake wa miaka mitano au 10 kwa mujibu wa Katiba na sheria. Lakini kwa nini mtendaji wa kitaalamu anayefanya vizuri lazima abadilishwe kwa sababu tu muda fulani umepita?

Kama sheria zetu zinaruhusu, au kama zinahitaji kurekebishwa, tujadili uwezekano wa viongozi mahiri wa taasisi muhimu kupewa muda wa kutosha—miaka 10, 20 au hata zaidi kulingana na umri, matokeo na mahitaji ya taasisi. Lakini hilo lisiwe kinga kwa uzembe. Akishindwa kazi, mlango wa kumwondoa uwe wazi hata baada ya miezi miwili.

Mfano mzuri unatoka Misri. Profesa Mahmoud Abu-Zeid alitumikia kwa muda mrefu katika sekta ya maji, akiongoza taasisi za utafiti kabla ya kuwa Waziri wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji kuanzia 1997 hadi 2009. Alizaliwa Julai 29, 1935 na kwa sasa ana miaka 91. Alipata Shahada ya Kwanza ya Uhandisi wa Ujenzi (Bachelor of Civil Engineering) kutoka Chuo Kikuu cha Cairo mwaka 1957.

Kisha akapata Shahada ya Uzamili katika Umwagiliaji (Master’s in Irrigation) kutoka Chuo Kikuu cha California mwaka 1959, na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Hidrolojia ya Maji ya Chini ya Ardhi (Groundwater Hydrology) kutoka Chuo Kikuu cha California mwaka 1962.

Mmisri huyo aliongoza sekta ya maji nchini Misri kwa miaka 30. Aliongoza Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Maji cha Misri (National Water Research Center) kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1979 hadi 1997, baadaye, kama nilivyosema hapo juu, akawa Waziri wa Maji kwa miaka 12. Jumla aliongoza sekta kwa miaka 30. Mapito yake hayafutiki nchini Misri.

Utaalamu wake ulikuwa hasa katika maji ya ardhini. Misri imejenga uwezo mkubwa wa muda mrefu wa kusimamia Mto Nile, maji ya ardhini, mifumo ya umwagiliaji na usalama wa maji. Wanahifadhi maji kwenye miamba, wanaita aquifer recharge. Hadi sasa wana hifadhi ya maji ya miaka 200. Nashukuru Mungu nilimhoji mwaka 2004 nikiwa jijini Cairo, Misri. Aliniambia umuhimu wa kutunza na kuendeleza kumbukumbu za kitaasisi kwa utaratibu wa kutobadili watendaji wakuu mara kwa mara, ikiwa wanafanya vizuri.

Somo hapa si kwamba kila kiongozi akae miaka 30. Somo ni kwamba taifa lisipoteze utaalamu, kumbukumbu ya taasisi na mipango ya muda mrefu kwa kubadilisha watu wanaofanya kazi vizuri bila sababu. Tunataka uchumi wa miaka 30, lakini wakati mwingine tunawapa wanaoutekeleza muda mfupi mno wa kujenga mifumo. Dira 2050 itatekelezeka vyema iwapo watendaji wataifahamu na kuiishi.

Sitanii, kuna ugonjwa mwingine unatunyemelea Waafrika. Siasa nyingi kuliko uzalishaji. Okot p’Bitek, kupitia vitabu vyake vya Song of Lawino na Song of Ocol, alitupatia taswira kali ya Afrika baada ya Uhuru. Watu wanaweza kushangilia Uhuru, viongozi wakabishana na vyama vikapambana, lakini kama fikra za mwananchi hazijabadilika, maskini anaweza kuendelea kulala katika boksi lilelile alilokuwa analalia kabla ya Uhuru.

Hapo ndipo tunapaswa kujiuliza: Uhuru wa kisiasa bila uhuru wa kiuchumi una maana gani kwa tumbo la mwananchi? Maandiko Matakatifu yanafundisha kwa ukali: “Asiyefanya kazi, asile.” Hii ni falsafa inayopaswa kurudi katika jamii yetu. Pia tusitumie dini kama mbadala wa kazi. Tusali, ndiyo. Tumwombe Mungu, ndiyo. Lakini baada ya sala, twende kazini. Mungu ametupa akili, mikono, ardhi, bahari, madini, bandari na nafasi ya kijiografia.

Unaweza kusali saa 24 katika haya makanisa ya kisasa yanayoahidi maajabu na miujiza, lakini nyama iliyopo buchani haitahamia nyumbani kwako kwa muujiza bila kuilipia. Lazima uifanyie kazi, upate fedha, uende dukani na uinunue.

Vivyo hivyo kwa taifa. Bandari ikifikia tani milioni 62, lakini kampuni za usafirishaji zikawa za wengine, maghala yakawa ya wengine, malori yakawa ya wengine, clearing and forwarding wakafanya wengine na Watanzania tukabaki watazamaji, tutakuwa tumepoteza fursa ya kihistoria.

Tuanze sasa kuandaa vijana kuwa madereva wa kitaalamu, mawakala wa forodha, wataalamu wa logistics, kodi, wamiliki wa maghala, waendeshaji wa malori, wataalamu wa TEHAMA na wajasiriamali wanaohudumia mnyororo mzima wa bandari.

Siasa ni muhimu. Demokrasia ni muhimu. Lakini tusifanye siasa kuwa kazi yetu ya saa 24. Mjadala wetu mkubwa uwe: ninatengenezaje fedha? Tanzania inauzaje zaidi nje? Tunamilikije sehemu kubwa ya biashara inayopita bandarini? Tunatengeneza ajira kutokana na tani milioni 62? Tunawezaje kupanua wigo wa kodi bila kuua biashara? Huduma za afya, barabara, SGR na meli katika maziwa yetu ziwe bora kiasi gani baada ya nchi yetu kukusanya kodi za kutosha?

Hizo ndizo siasa ninazozitaka. Siasa ziwe uchumi. Bandari iwe fursa. TRA iwe mshirika wa uzalishaji. Na Mtanzania afanye kazi. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827