Bangkok, Thailand

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, leo ameshiriki katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Kimataifa wa Nishati wa Gastech 2026, unaofanyika Bangkok, Thailand, ukiwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu, wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kutoka zaidi ya nchi 150 duniani.

Gastech 2026 inafanyika katika kipindi ambacho mahitaji ya nishati duniani yanaendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na upanuzi wa viwanda, huku changamoto za kijiografia na kisiasa, kuvurugika kwa mifumo ya usambazaji na mabadiliko ya masoko zikiendelea kuathiri usalama wa nishati duniani.

Mkutano wa mwaka huu unafanyika kwa kaulimbiu “Advancing Global Energy Market Stability”, ukilenga kujadili hatua na suluhisho za kuimarisha usalama, uhimilivu na upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa gharama nafuu.

Katika mkutano huo, gesi asilia, LNG, umeme, teknolojia za kupunguza hewa ukaa na Akili Bandia (AI) vinajadiliwa kama miongoni mwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati, unyumbufu wa mifumo ya nishati na ustahimilivu wa viwanda.

Ushiriki wa Naibu Waziri Mhe. Salome katika Mkutano wa Gastech 2026 unaipa Tanzania fursa ya kuendelea kutangaza uwezo na fursa za uwekezaji katika rasilimali za gesi asilia, pamoja na kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya nishati.

Gastech 2026 inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wataalamu 50,000 wa sekta ya nishati kutoka zaidi ya nchi 150 na kufunguliwa Rasmi na Waziri Mkuu wa Thailand Mhe. Anutin Charnvirakul.

Ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hili unaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kutumia rasilimali za nishati kuchochea uwekezaji, ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu, sambamba na kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kujenga mifumo ya nishati yenye uhakika na ustahimilivu.