Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika biashara ya umeme kikanda, huku Mradi wa Kuunganisha Gridi za Umeme Tanzania na Zambia ukifikia asilimia 90 ya utekelezaji na kutarajiwa kukamilika Februari 2027, hatua itakayoiunganisha Tanzania na soko la umeme la Kusini mwa Afrika na kuongeza fursa za biashara ya umeme kuvuka mipaka.
Akizungumza, Septemba 11, 2026, katika ufunguzi wa Mkutano wa 67 wa Kamati ya Usimamizi ya Jumuiya ya Umeme ya Kusini mwa Afrika (SAPP), Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe. Seif Kombo, amesema kuimarisha biashara ya umeme kuvuka mipaka ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa nishati, kuimarisha usalama wa gridi na kupunguza gharama za umeme katika ukanda huo.
Ameeleza kuwa Tanzania, kupitia Serikali na TANESCO, inaendelea kuwekeza katika kuimarisha miunganisho ya gridi, ikiwemo Mradi wa Tanzania-Zambia wa msongo wa kilovoti 400 ambao, utakapokamilika, utaongeza uwezo wa Tanzania kushiriki katika biashara ya umeme ndani ya SAPP.
“Kuimarisha biashara ya umeme kuvuka mipaka kutaziwezesha nchi kutumia kikamilifu rasilimali za nishati zilizopo, kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha usalama wa gridi,” amesema Mhe. Kombo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya SAPP, Andrew Etzinger, amesema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati, hususan wakati mabadiliko ya tabianchi, ukame na matukio ya hali ya hewa yanapoendelea kuathiri mifumo ya uzalishaji wa umeme.
Amesema kukamilika kwa muunganisho wa Tanzania na Zambia kutakuwa hatua muhimu katika kuunganisha SAPP na Jumuiya ya Biashara ya Umeme Mashariki mwa Afrika (EAPP), hivyo kupanua wigo wa ushirikiano na biashara ya umeme kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usafirishaji Umeme wa TANESCO, Mha. Zakaria Mgalama, amesema mkutano huo umetoa fursa kwa nchi wanachama na wadau wa sekta ya umeme kujadili namna ya kuimarisha biashara ya umeme, miundombinu na usalama wa nishati katika ukanda huo.
“Kwa Tanzania, kukamilika kwa Mradi wa Tanzania-Zambia kutakuwa hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa nchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya umeme ya kikanda, ikiwemo kuuza umeme katika masoko ya nchi wanachama wa SAPP,” amesema Mha. Mgalama.
Muunganisho huo pia utaimarisha nafasi ya Tanzania katika mtandao mpana wa biashara ya umeme unaounganisha Afrika Mashariki na Kusini, na kuongeza fursa za matumizi bora ya uwezo wa uzalishaji na miundombinu ya umeme iliyopo.
Mikutano ya 67 ya SAPP, iliyofanyika Zanzibar kuanzia Septemba 7 hadi 11, 2026, imejadili masuala ya mipango ya mifumo ya umeme, miundombinu ya usafirishaji, biashara ya umeme na hatua za kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.




