📌Ataka kasi ya utekelezaji wa mradi na wazawa kupewa kipaumbele
📌Wachimbaji wapongeza
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya shilingi bilioni 198.67 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Iganjo mkoani Mbeya hadi Saza mkoani Songwe pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Saza, mradi unaotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Songwe na Wilaya ya Chunya.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Septemba 11, 2026 katika eneo la Saza-Mkwajuni, Wilaya ya Songwe, Mhe. Salome amesema mradi huo utaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo ambayo kwa sasa yanategemea umeme unaotoka mkoani Mbeya unaohudumia maeneo mengi kwa umbali mrefu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa mfumo wa umeme kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ukiweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, zikiwemo biashara, kilimo, viwanda na uchimbaji wa madini.
Mhe. Salome amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya nishati ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Ameeleza kuwa Mradi wa Iganjo–Saza pia ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 wa Tanzania–Zambia (TAZA), ambao kwa upande wa Tanzania unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa kupitia Kisada, Iganjo na Tunduma hadi Sumbawanga, yenye urefu wa kilomita 616.
Amesema miundombinu ya Mradi wa TAZA inahusisha pia ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya, ambacho ndicho kitakachowezesha kusafirisha umeme kwenda Saza mkoani Songwe ambapo kwa ujumla utekelezaji wa Mradi wa TAZA umefikia asilimia 89.46 na unatarajiwa kukamilika Februari 2027, kabla ya kukamilika kwa Mradi wa Iganjo–Saza.
“Tunataka Songwe, Mbeya, Rukwa, Iringa na mikoa mingine katika ukanda huu iwe na uwezo wa kuvutia uwekezaji, kukuza viwanda, kuongeza shughuli za kilimo, uchimbaji madini na biashara pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo,” amesema Mhe. Salome
Aidha, Mhe. Salome ameipongeza TANESCO kwa kutumia taasisi yake ya ndani, TANESCO Engineering Consultancy Unit (TANECU), kuwa Mhandisi Mshauri wa mradi huo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga na kuimarisha uwezo wa wataalam wa ndani kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya umeme.
Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa kuendelea kutekeleza miradi inayolenga kuongeza matumizi ya umeme na mapato ya Shirika, Mhe. Salome amesisitiza kuwa Serikali inataka kuona thamani ya fedha, ubora na uzingatiaji wa muda wa mikataba katika utekelezaji wa miradi ya umeme.
“Naielekeza TANESCO na Mkandarasi kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa kasi inayostahili, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia masharti yote ya mkataba. Serikali na wananchi wa Songwe hatutegemei kusikia muda wa utekelezaji wa mradi umeongezeka; tutafurahi kuona mradi umekamilika ndani ya wakati na kwa ubora,” amesema.
Vilevile, ameelekeza taratibu za ulipaji fidia kwa wananchi watakaopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kufanyika kwa haki na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi kupewa kipaumbele katika fursa za ajira na utoaji wa huduma mbalimbali wakati wa utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amewahakikishia wananchi wa Songwe na Mbeya, hususan maeneo ya Chunya, kuwa Serikali inatambua changamoto za upatikanaji wa umeme wanazokabiliana nazo na inaendelea kuchukua hatua za kuzitatua, mojawapo ni ujenzi wa njia ya umeme kutoka Mwakibete-Mbeya hadi wilayani Songwe ya kV 33 itakayokamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Awali, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Amos Kaihula amesema Mradi wa Iganjo–Saza unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na Kituo cha Kupoza Umeme cha Saza, utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi 18.
Amesema Kituo cha Saza kitakuwa na transfoma mbili zenye uwezo wa MV 50 kila moja na kwamba mradi huo utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme Songwe na Chunya, maeneo ambayo kwa sasa yanapata umeme kutoka Mbeya unaosafirishwa kwa umbali wa takribani kilomita 116.
Amesema Mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya TBEA ya China.
Kwa upande wao, wachimbaji wa madini mkoani Songwe kupitia mwakilishi wao, Shadrack Mwakyalabwe, wameipongeza Serikali kwa mradi huo, wakisema utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kuwawezesha kufanya shughuli za uchimbaji kwa ufanisi zaidi. Wamesema kwa sasa baadhi yao wanakabiliwa na gharama kubwa za uzalishaji kutokana na kutegemea mafuta kuendesha shughuli zao.









