Tanzania imepata nafasi 150 za ufadhili wa masomo nchini Algeria kwa wanafunzi waliofanya vizuri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza fursa za elimu ya juu nje ya nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali ya Algeria itagharamia ada za masomo, wakati Serikali ya Tanzania itagharamia fedha za kujikimu kwa wanafunzi hao kupitia utaratibu wa Samia Scholarship.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Septemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda amesema fursa hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha wanafunzi wa Kitanzania wanapata nafasi zaidi za kusoma katika vyuo vya nje.

Amesema kati ya wanafunzi 1,000 waliotangazwa kupata Samia Scholarship, wanafunzi 10 tayari wamechaguliwa kwenda kusoma Moscow, Urusi, hatua inayodhihirisha ongezeko la fursa za masomo ya juu nje ya nchi.

Amesema majina ya wanafunzi 150 watakaochaguliwa kwa ajili ya masomo nchini Algeria yatawekwa kwenye tovuti ya Wizara, pamoja na maelekezo kuhusu namna ya kuwasilisha nyaraka na taratibu nyingine muhimu za safari, ikiwemo upatikanaji wa hati za kusafiria.

Prof. Mkenda amesema Serikali inalenga kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha wanafunzi kutoka makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo watoto wa wakulima na wafugaji.

Aidha, amewataka wanafunzi watakaopata nafasi hizo kuwa tayari kujifunza lugha ya Kifaransa, ambayo hutumika katika sehemu kubwa ya masomo nchini Algeria.