Na Deodatus Balile, JahuriMedia, Bagamoyo

Kuna msemo wa Kiswahili unaosema, “Mti haujinyanyui, huinuliwa na mizizi yake.” Maana yake ni kwamba, unapofika mahali fulani katika maisha, usisahau watu waliokuwa sehemu ya safari yako. Madaraka yanaweza kubadilika, nafasi zinaweza kubadilika, lakini urafiki wa kweli na historia ya pamoja ni hazina isiyopaswa kutupwa.

Sitanii, hili ndilo jambo ambalo namwandikia leo Makamu wa Rais Deogratias Ndejembi na kumsihi kulizingatia katika safari yake ya kisiasa. Nafahamu baada ya kuwa Makamu wa Rais, Ndejembi sasa watajitokeza marafiki wapya kutoka kila kona. Watajitokeza wataalamu wa migogoro watakaompa ushauri wa kila aina kumtenganisha na marafiki zake wa zamani.

Wengi tunakumbuka jinsi Ndejembi alivyomkumbatia Anthony Mavunde, kijana ambaye wamekua na kuwa pamoja katika safari yao ya kisiasa. Ni picha yenye ujumbe mkubwa kuliko maneno mengi. Ilikuwa ni ishara ya mtu anayekumbuka alikotoka na watu aliokuwa nao katika safari hiyo. Lakini sasa ameingia katika mikono mipya. Utaona hata kwenda kusali kanisani anasindikizwa.

Ni katika hatua hii, bila kuuma maneno, ninasema Ndejembi sasa atapata marafiki na washauri wa kujitokeza. Wataanza kumshushia ‘litania ya watakatifu wote’ na kumwonyesha orodha ya ‘wabaya’ wake. Atashangaa kujikuta katikati ya jungu lililokomaa. Zipo nyakati atatajiwa hata majina ambayo hataamini, akiambiwa wanamhujumu katika safari yake ya kisiasa.

Sitanii, katika siasa, si kila anayekuja kwako leo ni yule uliyekuwa naye jana. Katika hili usifunge milango pia. Ruhusu marafiki wapya. Wapo wanaoweza kuwa wa msaada kwako kuliko baadhi ya marafiki wa zamani. Lakini ufahamu kuwa asilimia kubwa ya marafiki wapya watakaojitokeza sasa na kuanza kukuaminisha kuwa wao wanakupenda kuliko wote wa zamani, wengi wao wanatokea ‘ukoo wa kutafuta ugali.’

Wapo wanaoweza kuonekana wako karibu na wewe kwa sababu ya nafasi uliyonayo, lakini nafasi ikibadilika, ukaribu nao utabadilika. Ndiyo maana mwanadamu anatakiwa kuwaheshimu na kuwathamini marafiki zake wa zamani. Naamini Ndejembi amelifahamu hili tangu enzi za ujana wake kuwa utu, heshima na uhusiano mwema ndiyo hubaki milele.

Kauli yake kwamba, “Wana, sitawazingua na sitamzingua Mama,” pia inaonyesha kwamba anaelewa uzito wa nafasi aliyopewa na umuhimu wa kutengeneza mazingira ya utulivu. Katika mazingira kama haya, ni muhimu zaidi kuwa na watu wanaokujenga kuliko wale wanaokupa majungu na kukusukuma kwenye migogoro isiyokuwa na tija.

Ndejembi anatakiwa kujilinda na watu wanaoweza kumshawishi aamini kwamba kila aliyekuwa rafiki yake jana sasa ni mpinzani wake. Huo ni mtego ambao viongozi wengi wameuingia. Wakati mwingine mtu anapopata madaraka, huanza kuzungukwa na watu wapya wanaomwambia yale anayopenda kusikia, huku wakimfanya awasahau wale aliokuwa nao wakati hana kitu.

Hata katika mafundisho ya Biblia, katika Mathayo 4:3–7, tunakumbushwa kuhusu majaribu yanayoweza kumkabili mtu anapokuwa katika nafasi kubwa. Madaraka nayo ni mtihani. Mtu anaweza kujaribiwa na kiburi, tamaa, sifa na watu wanaomzunguka. Lakini mwenye hekima hutambua kwamba nafasi ni ya muda, huku utu ukiwa urithi wa kudumu.

Huku kwetu Uswahilini, wanasema usiache mbachao kwa msala upitao. Usimkumbuke mtu kwa sababu tu unamhitaji leo, wala usimsahau kwa sababu tu mazingira yamebadilika. Usishangae siku moja akaja mtu akakwambia Anthony Mavunde, mtu ambaye amekuwa sehemu ya safari yako kisiasa, naye uchunguze nyendo zake. Yapo haya na tumeyashuhudia katika nchi hii. Waliokuwa ‘wana’, waliokuwa wanakula sahani moja, kivuruge kikapita katikati yao, wakaanza kutoleana lugha za kuvuana gamba!

Sitanii, nafahamu kuwa ujio wa Ndejembi umevuruga rada za wengi katika safari ya kisiasa kuelekea mwaka 2030. Ni katika hatua hii, wataalamu wa migogoro watakuwa wameshaingia kazini. Ndiyo maana ndani ya siku mbili tu, tulisikia wakidai Ndejembi amezaliwa Pemba. Hii haikutamkwa kimakosa. Hii ina lengo la ziada. Ni pasi ndefu. Wanaangalia zaidi ya Umakamu wa Rais. Nitaliandika kwa kina siku za usoni hili.

Ndejembi, nafasi uliyonayo leo si mwisho wa safari. Usiruhusu marafiki wapya wakufanye uwachukie watu wako wa zamani. Wathamini waliokupenda kabla ya cheo, kabla ya madaraka na kabla ya umaarufu. Na hata ikitokea vipi, liepuke jaribu la ‘kuwapiga shoti’ wenzako. Mungu atanyoosha mapito yako.

Nafahamu huko utakutana na wataalamu wa kupika migogoro waliosomea Urusi, Bulgaria na Cuba. Watakushushia litania ya wabaya wako. Ni katika hatua hii itakupasa kuazima maneno ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, kwamba: “Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.”

Ikitokea, narudia, ikitokea mtu akaandaa mazingira ya wewe kugombana na Rais Samia Suluhu Hassan, mtu huyo mwingize katika kundi la shetani bila kusita. Nakwambia hivyo si kwa jingine, bali kwa ukweli kwamba kama Rais Samia asingetaka uwe Makamu wa Rais, usingekuwa. Ni kwa minajili hiyo nasema, akija mtu na kukwambia mtilie shaka Rais Samia, mtu huyo ndiye atakuwa mbaya wako, mwepuke, shikamana na Rais Samia.

Nahitimisha kwa kusema nchi yetu inahitaji maendeleo na si migogoro ya kisiasa. Wapo watu wanaoipika migogoro hadi tunawashangaa. Wapo pia viongozi wanaowasikiliza na kufikia katika tuliyoyashuhudia. Kama ulivyosema, naamini unafahamu kuwa kwa sasa urais si mali yako. “Usitamani mali ya mtu mwingine.” Wewe ni msaidizi wa Rais Samia. Msaidie Rais ajenge uchumi ili Dira 2050 itufikishe katika uchumi wa dola trilioni moja. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827