Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika siasa, kuna wakati busara ya kiongozi haipimwi kwa maneno anayosema, bali kwa mambo anayochagua kutoyasema. Kuna wakati ukubwa wa kiongozi hauonekani katika namna anavyomshambulia mpinzani wake, bali katika namna anavyolinda heshima yake hata pale ambapo wamefika mwisho wa safari ya kisiasa pamoja.

Sitanii, katika hili, Rais Samia Suluhu Hassan ametufundisha somo gumu na muhimu katika siasa za ustaarabu. Mjadala kuhusu uhusiano wake kikazi na aliyekuwa Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ni mkubwa. Lakini kwa muda wote ambao tofauti hizo zilionekana kuibuka, Rais hakujenga siasa za kulalamika hadharani, kumdhalilisha Makamu wake au kumwaga maneno ya hasira mbele ya wananchi.

Kinyume chake, Tanzania imeshuhudia viongozi hao wakiendelea kutekeleza majukumu yao ya kitaifa kwa staha. Hata katika matukio makubwa ya kitaifa, walionekana pamoja, wakitabasamu na kuzungumza hadi dakika ya mwisho kama viongozi wanaotambua kuwa masuala ya taifa ni makubwa kuliko hisia za watu wawili.

Sitanii, kwa sura waliyokuwa wanaionyesha hadharani wawili hawa, na hata tukio lile gumu ambalo aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Nchimbi, aliwataka Watanzania kupambania Katiba Mpya, kutokana na majibu aliyotoa Rais Samia, kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, mimi na wengine wengi tuliamini kuwa Dk. Nchimbi alitoa kauli ile kwa ridhaa ya Rais Samia.

Rais Samia alisema kwa ufupi kuwa: “Tanzania itaandika Katiba Mpya kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.” Kilichoshangaza wengi ni kauli ya Nchimbi iliyodhaniwa kuwa imekwenda mbali zaidi, aliposema: “Uamuzi wote katika Baraza la Mawaziri unafanywa na Rais… sisi wengine wote ni washauri… Rais akitaka, tunapata Katiba Mpya.”

Hapa wengi walijiuliza: Kwa nini amesema hivi? Alilenga kuwaaminisha nini Watanzania?

Sitanii, pamoja na hilo lililokuwa gumu kumeza katika muktadha wa ‘uwajibikaji wa pamoja’, bado Rais Samia alionyesha ukomavu wa kisiasa. Mtu anaweza kuwa na tofauti na mwanasiasa mwenzake, lakini tofauti hizo hazilazimiki kuwa tamthilia ya taifa. Tumeyaona haya katika uongozi uliotangulia!

Rais Samia ameonyesha pia kuwa katika CCM, hata pale panapotokea mgogoro mkubwa wa kisiasa, jambo muhimu si kuusambaza kwenye mikutano ya hadhara kama ilivyotokea kati ya mwaka 2008 na 2012, bali kutumia mifumo ya chama. Hatua zilizochukuliwa dhidi ya Dk. Nchimbi zilipitia vikao na taratibu za CCM, huku uamuzi wa chama ukifuatiwa na hatua za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais mpya, Deogratius Ndejembi.

Hapa ndipo tofauti kubwa ilipo. CCM ya leo imetufundisha kwamba chama kikubwa hakiwezi kuendeshwa kwa hasira, wala kwa makundi yanayoshindana kwa kupandisha sauti. Chama kina Katiba, kanuni, vikao na taratibu. Na pale mifumo hiyo inapofanya kazi, migogoro ya kisiasa inaweza kutatuliwa bila taifa kugeuzwa uwanja wa mapambano ya kauli.

Historia ya CCM imeshuhudia nyakati ambazo tofauti za viongozi zilifika hadharani kwa namna iliyopunguza heshima ya taasisi. Lakini katika jambo hili, Rais Samia amechagua njia nyingine: staha kwanza, taasisi kwanza, taifa kwanza.

Hata alipowaweka pembeni baadhi ya wanasiasa waliokuwa na uzito mkubwa ndani ya Serikali na CCM, akiwamo Nape Nnauye na January Makamba, hakuwageuza kuwa maadui wa kutukanwa hadharani. Wawili hao waliondolewa katika Baraza la Mawaziri mwaka 2024 bila Rais kutoa hadharani orodha ya makosa yao binafsi.

Na jambo la kuvutia zaidi ni kwamba baadaye Rais Samia alionyesha kwamba kumwondoa mtu katika nafasi ya uongozi si lazima kumvua utu wake. January Makamba alipokutana tena na Rais Samia mwaka 2025, Rais alizungumza naye kwa upendo, akamwita ‘mwanangu’ na hata kumkumbatia hadharani. Hili ni fundisho kubwa kwetu sote.

Kumwondoa mtu madarakani si kumwondoa katika ubinadamu. Ndiyo maana hata katika suala la Nchimbi, Rais Samia hakuchagua utamaduni wa kumdhalilisha aliyekuwa Makamu wake. Mfumo wa chama uliendelea na mchakato wake, huku Rais akiendelea na wajibu wake wa kulinda nchi. Hata siku ya kumwapisha Ndejembi, hakumgusa moja kwa moja Nchimbi.

Sitanii, kusema hayo hakumaanishi kwamba Dk. Nchimbi hakukosea. Kwa mtazamo wangu, kuna mambo makubwa matatu ambayo aliyekuwa Makamu wa Rais hakusoma alama za nyakati.

Kwanza, Dk. Nchimbi alipaswa kutambua zaidi uzito wa nafasi aliyokuwa nayo. Makamu wa Rais si mwanasiasa wa kawaida.

Kila kauli yake inaweza kutafsiriwa kama sehemu ya msimamo wa Serikali. Hivyo, hata hoja nzuri inaweza kupoteza uzito ikiwa inawasilishwa katika mazingira yanayoweza kuonekana kama tofauti ya ndani ya uongozi. Uwajibikaji wa pamoja ni msingi muhimu katika Serikali.

Pili, alipaswa kutenganisha nafasi yake ndani ya Serikali na mijadala yake ya kisiasa ndani ya CCM. Katika chama chenye historia na mifumo kama CCM, tofauti za kimtazamo zinahitaji kujadiliwa kwa kutumia vikao vya ndani ya chama na njia zilizowekwa, badala ya kwenda hadharani kwa namna inayoweza kutafsiriwa kama changamoto kwa uongozi wa juu.

Tatu, alipaswa kuwa makini zaidi katika muda na mazingira ya baadhi ya kauli zake za kisiasa. Kauli kuhusu Katiba Mpya, kwa mfano, zinaweza kuwa hoja halali katika jamii, lakini nafasi ya Makamu wa Rais inahitaji busara ya ziada katika namna na mazingira ya kuziwasilisha.

Sitanii, yapo matukio mengine mawili. Moja ni lile ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na Wazee wa Dar es Salaam Desemba 2, 2025. Aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Nchimbi, aliitwa amkaribishe Rais Samia kuzungumza, ikawa kama vile yeye hakuguswa kabisa na matukio ya Oktoba 29, 2025.

Matarajio halali ya jamii yalikuwa ampe pole Rais Samia, awape pole Watanzania na awaase kutorudia matukio hayo. Hakufanya hivyo.

Agosti 22, 2026, Balozi Nchimbi akapewa tena nafasi ya kuzungumza katika uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji. Kwa mshangao wa washiriki, akasema anaokoa muda; amepewa dakika 10, na badala ya kuzungumza akamwita Rais Samia azungumze.

Baada ya hapo niliwasiliana na Nchimbi, nikamwambia anachokifanya si sawa; mbele ya jamii, kukataa kuzungumza hata neno moja anapopewa nafasi ya kumkaribisha Rais Samia. Alikiri, akasema: “Nimekuelewa, siku nyingine nikipata nafasi nitazungumza.”

Umakamu umeondoka!

Hata hivyo, makosa haya hayahalalishi mtu kudhalilishwa. Hapa ndipo Mama Samia anapotufundisha. Mama si yule anayemnyamazisha mtoto kwa kumvunjia heshima mbele za watu. Mama ameonyesha busara ya hali ya juu kwa kumkemea mtoto, kumweka pembeni na hata kumzuia kufanya jambo fulani, lakini bado akalinda utu wake.

Hivyo ndivyo siasa zinavyopaswa kuwa. Na sasa tumempata Deogratius Ndejembi. Ni Makamu wa Rais wa tatu katika Awamu ya Sita. Alianza Dk. Philip Mpango, akafuatiwa na aliyejiuzulu, Balozi Dk. Nchimbi.

Ndejembi si mtu aliyeingia katika nafasi hii kwa makeke. Amefika kwa mchakato wa chama na baadaye taratibu za kikatiba. CCM ilimpendekeza, Bunge likamthibitisha kwa kura zote za wabunge 324 na, Agosti 29, 2026, ameapishwa rasmi kuwa Makamu wa Rais.

Hii ni nafasi ambayo Ndejembi anapaswa kuitazama kama dhamana, si zawadi. Wanaomfahamu wamemwelezea kuwa ni mtu mchapakazi, mwenye uwezo wa kufanya kazi na anayependa watu. Hizo ni sifa muhimu sana kwa Makamu wa Rais. Lakini zaidi ya yote, Ndejembi anapaswa kubaki kuwa Ndejembi yuleyule.

Wabunge waliochangia bungeni wameeleza upendo alionao Ndejembi, uchapa kazi wake na ukweli katika analoliamini. Nami naomba kutoa ushuhuda angalau mmoja.

Desemba 2023 nilikuwa nakwenda nchini India kwa matibabu. Mke wangu ni mtumishi wa umma. Ili kunisindikiza, alipaswa kupata kibali cha kusafiri nje ya nchi.

Nilikwama pale jijini Dar es Salaam. Ndejembi alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Kuidhinisha vibali vya watumishi wa umma kusafiri nje ya nchi ilikuwa moja ya majukumu yake katika wizara hii. Alikuwa kikaoni Tanga. Nilipompigia simu, alitoka nje ya kikao, nikamweleza tatizo langu.

Aliniambia amenielewa. Alichukua kompyuta yake (laptop), akaingia kwenye mfumo na kuidhinisha kibali cha mke wangu kusafiri nje ya nchi. Aliniambia anakishughulikia hadi Ikulu kikamilike na baada ya nusu saa akaniambia tunaweza kwenda uwanja wa ndege tayari kwa safari.

Namshukuru Mungu, nilikwenda India, nikafanyiwa upasuaji na kupona. Ndejembi alikuwa sehemu ya uponyaji kwangu. Mungu ambariki sana.

Naamini kwa sifa alizonazo Ndejembi, hastahili hata kupewa ushauri. Anafahamu vyema kuwa yeye ni msaidizi wa Rais Samia. Jambo moja nimshauri; ikiwa hajawahi kusoma kitabu muhimu, basi akitafute kitabu kiitwacho The 48 Laws of Power (Kanuni 48 za Madaraka), kilichoandikwa na Robert Greene.

Kwa ufupi, moja ya kanuni muhimu ni: “Bosi hakosei.” Naomba ukisome, ila utambue wadhifa wako ni wa kumshauri bosi wako, si wa kushindana naye!

Naomba kuhitimisha makala hii kwa aya moja. CCM imezidi kutufundisha. Mabadiliko yaliyotokea yamethibitisha pasipo chembe ya mashaka kuwa chama ni kikubwa kuliko mtu. Naamini mmenielewa.

Hongera Rais Samia kwa kuziishi siasa za kistaarabu na kurekebisha wanaokosea kwa kalamu, badala ya mapambano.

Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827