Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jana, Agosti 25, 2026, ilikuwa siku iliyozalisha mshituko mkubwa katika taifa letu. Mshituko huo ulitokana na taarifa ya kujiuzulu kwa Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye amesema ataondoka rasmi madarakani Septemba 4, 2026. Rais Samia Suluhu Hassan amepokea na kuridhia ombi hilo. Kwa mujibu wa taarifa yake mwenyewe, Dk. Nchimbi amesema ameamua kuondoka katika siasa na utumishi wa umma baada ya kujiridhisha kwamba Rais Samia anataka mabadiliko katika nafasi hiyo.
Hata mimi nilishituka. Lakini, kwa kufuatilia yanayoendelea katika nchi yetu, nilikuwa nimesikia tetesi hizi miezi kadhaa iliyopita. Sikuamini kama ni za kweli. Baadaye nikaanza kuona dalili za minyukano ya kauli na mijadala katika mitandao ya kijamii. Najua, si busara kuandika tetesi kama ukweli, lakini pia si busara kupuuza kabisa matukio yanayojenga picha ya mabadiliko makubwa katika uongozi wa nchi.
Sitanii, historia ya Tanzania inaonyesha kwamba kujiuzulu kwa viongozi si jambo geni. Mwaka 1977, Mzee Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani baada ya mauaji ya raia katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga yaliyohusisha vyombo vya dola. Mzee Mwinyi mwenyewe baadaye alisisitiza kwamba alijiuzulu kwa hiari yake na si kwa kusukumwa na Mwalimu Julius Nyerere. Katika sakata hilo hilo, Waziri wa Nchi Peter Siyovelwa na Wakuu wa Mikoa Peter Kisumo wa Mwanza na Marco Mabawa wa Shinyanga nao waliondoka madarakani baada ya kuwajibika kuhusu vitendo vya askari na usalama.
Mwaka 1984, Aboud Jumbe, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar, aliondoka katika nafasi zake zote baada ya mgogoro mkubwa kuhusu Muungano. Jumbe alihusishwa na msimamo wa kutaka mfumo wa Serikali Tatu, jambo lililomweka katika mvutano na uongozi wa wakati huo. Vyanzo vya kihistoria vinaonyesha kwamba kuondoka kwake kulitokana na mgogoro huo wa kisiasa na kwamba alilazimika kujiuzulu.
Mwaka 2008, Edward Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu kutokana na sakata la Richmond. Pamoja naye, mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Idrissa Msabaha waliondoka katika nafasi zao. Lowassa alisema amejiuzulu kuonyesha uwajibikaji, lakini akakataa utaratibu alioutumia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe, wa kumtuhumu bila kumpa nafasi ya kujitetea.
Operesheni Tokomeza ya mwaka 2013 nayo inapaswa kutajwa, lakini kwa usahihi. Khamis Kagasheki alitangaza kujiuzulu kama Waziri wa Maliasili na Utalii tarehe 20 Desemba 2013, wakati mawaziri Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na David Mathayo waliondolewa katika nafasi zao katika mazingira ya sakata hilo. Kwa hiyo, si sahihi kuwaweka wote wanne katika kundi moja la “waliojiuzulu kwa hiari”. Hapa ndipo tunapoona maana halisi ya uwajibikaji wa kisiasa.
Mwaka 2015, Profesa Sospeter Muhongo alijiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow, lakini Rais John Magufuli akamrudisha madarakani. Ila, kwa bahati mbaya, sakata la makinikia la mwaka 2017 likamwondoa tena Profesa Muhongo. Mwaka 2025, Balozi Humphrey Polepole alijiuzulu ubalozi wake nchini Cuba na baadaye akaeleza hadharani kutoridhishwa kwake na masuala ya utawala na utawala wa sheria.
Leo tunamshuhudia tena Dk. Nchimbi, ambaye amekuwa Makamu wa Rais kwa siku 295 tu, akiondoka katika nafasi ya pili kwa ukubwa nchini.
Sitanii, sasa swali kubwa si kwa nini Nchimbi ameondoka, bali tunamhitaji Makamu wa Rais wa aina gani?
Sababu rasmi ni moja: Dk. Nchimbi amesema alimwahidi Rais Samia kwamba kama wakati wowote Rais angeona anahitaji Makamu mwingine, yeye angeondoka, na sasa amejiridhisha kwamba Rais anataka mabadiliko.
Lakini nyuma ya kauli hiyo kuna mambo ambayo yameibua maswali. Kwa miezi ya karibuni kulikuwa na taarifa za madai kwamba Nchimbi alikuwa ametengwa katika baadhi ya shughuli muhimu za Serikali. Gazeti moja lilichapisha habari iliyodai kwamba Makamu huyo alikuwa amekataa kujiuzulu. Hivyo, habari hizo zilikuwepo, lakini hazikuthibitishwa rasmi na Ikulu kama sababu ya kujiuzulu kwa Nchimbi.
Jambo jingine lililovuta macho ya wengi ni kauli ya Dk. Nchimbi ya Julai 24, 2026, alipowataka Watanzania kupambania Katiba Mpya. Alisema Katiba ni msingi wa mageuzi ya utawala, haki na utu wa Watanzania, na akasisitiza umuhimu wa Katiba inayokubalika na wadau wote.
Sitanii, kauli hiyo ilikuwa ya kisiasa kwa uzito wake kwa sababu ilitolewa na Makamu wa Rais mwenyewe, na baadhi ya wachambuzi waliitafsiri kama msimamo ambao ungeweza kutofautiana na namna baadhi ya watu ndani ya Serikali walivyotaka kulishughulikia suala hilo. Lakini pia, tusifanye tafsiri hiyo kuwa ukweli uliothibitishwa.
Kuna pia mjadala mpana kuhusu mazingira ya kisiasa yaliyofuatia uchaguzi wa 2025, maandamano, vifo na malalamiko kuhusu haki za kiraia. Baadhi ya wachambuzi wa kimataifa wamehusisha mvutano huo na tofauti za mitazamo ndani ya uongozi wa nchi. Hilo nalo ni uchambuzi, si sababu rasmi iliyotolewa na Nchimbi au Rais Samia.
Akiwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi alimtetea Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kuwa si mtu wa vurugu na wala hawezi kuua hata panya. Pia amekuwa na msimamo wa wazi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, hapaswi kuwa gerezani kwa kesi aliyoiona haina msingi.
Historia itahitaji majibu kamili siku moja. Kwa sasa, tunachojua ni kwamba Rais amekubali kujiuzulu kwa Makamu wake na mchakato wa kumpata mwingine umeanza.
Sitanii, naamini kila mmoja anajiuliza Tanzania kwa sasa inahitaji Makamu wa Rais wa namna gani? Nchi haihitaji Makamu wa Rais kwa sababu tu mtu ni maarufu, ana nguvu ndani ya chama au amekuwa na cheo kikubwa. Tanzania inahitaji mtu mwenye uwezo wa kuunganisha nchi, kutuliza tofauti, kusikiliza pande mbalimbali na kuwa daraja kati ya Rais na wananchi.
Katika mijadala isiyo rasmi, majina kadhaa yametajwa. Hakuna orodha rasmi iliyotolewa na Serikali au chama, lakini mimi kwa nafasi yangu ya uandishi nimepata orodha ndefu. Natangulia kusema majina haya tuyachukulie kama majina yanayozungumzwa, si walioteuliwa.
Nape Nnauye
Nape ana uzoefu mkubwa wa kisiasa, amekuwa mbunge na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini kama Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa. Ana uwezo wa kuzungumza na vijana, kuishi mitandaoni, na ana uzoefu wa siasa za chama.
Lakini swali ni kama Tanzania ya sasa inahitaji Makamu wa Rais mwenye sura ya siasa za ushindani wa ndani ya chama au mtu mwenye sura pana zaidi ya kitaifa. Nape anaweza kuwa na uwezo wa kisiasa wa kuunganisha makundi, lakini anahitaji kuonyesha zaidi kwamba anaweza kuwa Makamu wa Watanzania wote, si msemaji wa upande mmoja wa siasa, na kwamba masuala ya “goli la mkono” alikuwa anatania na abahatike jamii imwelewe hivyo.

Kassim Majaliwa
Majaliwa ni miongoni mwa majina yenye uzito mkubwa. Ametumikia Tanzania kama Waziri Mkuu kwa miaka kumi, kuanzia 2015 hadi 2025, na ana uzoefu mkubwa wa kuendesha Serikali na kushughulika na viongozi wa mikoa, wilaya na taasisi mbalimbali. Faida yake kubwa ni utulivu, uzoefu na kutokuwa mtu wa makelele ya kisiasa.
Kwa nafasi inayohitaji kuunganisha nchi, Majaliwa ana sifa nzito sana. Changamoto ni kwamba ameshatumikia muda mrefu katika nafasi ya juu na, japo si kanuni iliyoandikwa rasmi katika siasa za Tanzania, ni vigumu Rais na Makamu wa Rais kuwa dini moja. Swali jingine zito ni kama Rais ataona ni wakati wa kurudisha mtu wa kizazi hicho katika nafasi ya pili kwa ukubwa nchini au mtu anayezungumza “meme” kwa maana ya lugha za vijana.

Prof. Kitila Mkumbo
Kitila anaingia kwenye mjadala akiwa na sifa ya msomi na mtaalamu wa uchumi na mipango. Kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, na amekuwa akishughulika na mipango ya maendeleo, uwekezaji na uchumi wa Taifa. Anaweza kuwa chaguo zuri kama Rais anataka Makamu anayesisitiza uchumi, mipango na diplomasia ya uwekezaji.
Lakini Makamu wa Rais si Waziri wa Mipango tu; anahitaji pia mvuto wa kisiasa na uwezo wa kuzungumza na watu wa itikadi, dini, visiwa na Bara, vijana na wapinzani. Kikwazo kingine wanachotaja wachambuzi ni kwamba Kitila anatokea wilaya moja na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, yaani Iramba. Ni vigumu wilaya moja kutoa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.

Dk. Mwigulu Nchemba
Mwigulu ana uzoefu mkubwa wa Serikali na sasa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Amewahi kuwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Katiba na Sheria na Waziri wa Kilimo. Pia ana taaluma ya uchumi. Kwa upande wa uzoefu wa Serikali, ni miongoni mwa majina yenye nguvu zaidi.
Lakini kwa kuwa tayari ni Waziri Mkuu, kumhamisha mara moja kwenda Umakamu wa Rais kunaweza kuleta swali la nani atachukua nafasi ya Waziri Mkuu na kama Rais anataka mabadiliko makubwa au mwendelezo wa timu iliyopo. Ikitokea akapandishwa kuwa Makamu wa Rais, jibu rahisi ni kwamba zile mbio anazotajwa nazo za 2030 zitakuwa zimeingia mchanga!

Dk. Dotto Biteko
Biteko amekuwa mmoja wa viongozi wanaoonekana katika utekelezaji wa shughuli za Serikali, hasa katika maeneo ya nishati na uchumi. Uzoefu wake katika Serikali ya Muungano na uwezo wake wa kuwasiliana na wananchi ni faida. Anaweza kuwa chaguo la kizazi kinachoinuka ndani ya CCM.
Kipindi alichoteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu kilithibitisha pasipo mashaka kuwa ana nidhamu, ni mnyenyekevu, ana weledi na ni kiunganishi mzuri wa watu.
Biteko, kwa Kanda ya Ziwa, anaonekana kama mrithi wa Dk. John Pombe Magufuli, na hivyo ufuasi wake si wa kutilia mashaka. Kwa wingi wa wapigakura wa Kanda ya Ziwa, ambayo mikoa sita ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Geita na Simiyu ina jumla ya wapigakura milioni 16.42, huyu anaweza kuwa kiungo bora kabisa kwa jimbo hili lenye karibu theluthi moja ya Watanzania. Umri wake nao unamweka katika rika la kuaminiwa na vijana na wazee.

Paul Makonda
Makonda ni mwanasiasa mwenye nguvu kubwa ya kisiasa, hasa kwa vijana, na ana uwezo mkubwa wa kuwasiliana na umma. Amekuwa Mkuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Arusha, kiongozi wa CCM katika eneo la Itikadi na Uenezi, na sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Hata hivyo, kwa mtazamo wangu, ingawa umaarufu na uwezo wa kisiasa ni faida, Makamu wa Rais anatakiwa kuwa mtu anayepunguza joto la kisiasa, si kuongeza joto. Nafasi ya Makamu wa Rais inahitaji mshauri, si mtu mwenye misimamo mikali. Nafasi hii inahitaji wale wanaoitwa wapatanishi katika maandiko matakatifu. Sina uhakika kama Makonda ni mmoja wao!

Dk. Rhimo Nyansaho
Nyansaho ni jina linalovutia kwa sababu ana uzoefu wa kitaaluma na kiutendaji, na kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Anaweza kuleta taswira ya nidhamu, usalama na utaalamu katika uongozi wa juu.
Ni kijana, hana makeke wala vurugu na mtu yeyote. Ni mnyenyekevu ambaye, kwa hakika, ikiwa kweli anatafutwa msaidizi wa Rais, kumpendekeza ni uamuzi sahihi. Kwa umri wake, utendaji wake na uzoefu katika masuala ya uchumi, na kwamba hataki kutumia maguvu, anayo nafasi ya kulisaidia Taifa kuondokana na siasa za “jino kwa jino”.
Lakini Umakamu wa Rais unahitaji pia uzoefu mkubwa wa siasa za kitaifa, Muungano na maridhiano ya kijamii. Kwa vigezo hivyo, Nyansaho ni muungwana kwa kauli na vitendo ambaye anaweza kuwa chaguo sahihi.

Prof. Palamagamba Kabudi
Kabudi ni miongoni mwa wanasiasa wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya katiba, sheria na diplomasia. Amekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Nje na sasa anaendelea kuwa mmoja wa mawaziri wenye uzoefu mkubwa katika Serikali.
Kwa Tanzania inayojadili Katiba, Muungano na maridhiano, Kabudi anaweza kuwa na uzito mkubwa sana wa kiakili na kikatiba. Changamoto yake ni umri na ukweli kwamba amekuwa ndani ya mfumo kwa muda mrefu; hivyo, kama Rais anataka sura mpya kabisa, huenda asiwe chaguo la kwanza.
Tunafahamu kuwa ya kale ni dhahabu, lakini hata maandiko matakatifu yana “Agano la Kale” na “Agano Jipya”; nyakati za Gen-Z zinaelekeza abaki kuwa mshauri zaidi. Hata kama Ikulu hakuna kubeba zege, mbio za mwenge zitampa shida.

Deogratius Ndejembi
Ndejembi ni miongoni mwa viongozi wa kizazi kipya wanaopata uzoefu mkubwa wa Serikali. Kwa sasa ni Waziri wa Nishati, sekta ambayo ina uzito mkubwa katika uchumi wa Tanzania. Anaweza kuwakilisha kizazi kipya chenye mtazamo wa maendeleo na uchumi. Lakini Umakamu wa Rais ni nafasi pana kuliko kusimamia sekta; inahitaji uzoefu wa kutosha wa siasa za Muungano na uwezo wa kuwa daraja la kitaifa.
Kwa hakika, anavyoendesha Wizara ya Nishati sasa, mipango mikubwa aliyonayo ya ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta Tanga, kuongeza umeme kufikia megawati 8,000 kabla ya 2030 na kurekebisha mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini, kumpandisha atakuwa amepewa heshima, lakini uwaziri hapa alipo, naona analitumikia vyema Taifa kwa uadilifu mkubwa. Hata hivyo, ikiwa atapewa Umakamu, Rais anaweza kumwongezea nguvu ya kuisimamia sekta hii anayoonekana kuimudu vilivyo.

George Simbachawene
Simbachawene ana uzoefu wa muda mrefu serikalini na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uwaziri, ikiwa ni pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Rais, Utumishi na Mambo ya Ndani. Anaelewa vizuri mfumo wa utawala wa nchi na siasa za ngazi za chini.
Hiyo ni faida kubwa kwa Makamu wa Rais anayepaswa kuelewa maisha ya wananchi kutoka ngazi ya kijiji hadi Serikali Kuu. Hata hivyo, wapo wanaomwona ni mpole mno, maana pamoja na kwamba Makamu wa Rais hapaswi kuwa na makeke, ni lazima awe kama chupa ya chai: ndani chai ya moto, nje unaiweka kwenye shavu.

Daniel Chongolo
Chongolo ni mwanasiasa mwenye uzoefu wa ndani ya CCM aliyepanda na kufikia ngazi ya Katibu Mkuu na sasa ni Waziri wa Kilimo. Ana faida ya kukielewa chama, Serikali na masuala yanayowagusa moja kwa moja wananchi, hasa wakulima. Hilo ni muhimu kwa nchi ambayo wananchi wake wengi wanategemea kilimo.
Chongolo ana sifa ya unyenyekevu na utulivu katika kufanya uamuzi. Si mtu wa kukurupuka wala kusema uongo. Chongolo ana sifa moja ya kipekee: akikwambia ndiyo, ujue hiyo ni ndiyo ya kweli. Akikwambia hapana, ujue hiyo ni hapana kamili, si nusu hapana. Amepitia milima na mabonde, hivyo anaweza kuwa kiunganishi mzuri kati ya Rais na wananchi kwa wadhifa huu.

John Shigela
Shigela ana uzoefu wa uongozi wa kisiasa na kiutawala, na amekuwa akifanya kazi katika mfumo wa Serikali na chama. Hilo linaweza kumsaidia kuelewa namna ya kuunganisha Serikali na chama.
Lakini katika orodha hii, jina lake linaonekana kuwa na uzito mwingi katika uzoefu alioupata kupitia chama na hasa vijana wa UVCCM. Mikoa yote aliyopata kuiongoza – Tanga, Morogoro na sasa Geita – imepata utulivu mkubwa. Ni msikivu na hakurupuki katika kufanya uamuzi.

Anthony Mtaka
Mtaka ni jina ambalo linaweza kuvutia kutokana na uzoefu wake wa uongozi wa mikoa na uwezo wa kushughulika na wananchi moja kwa moja. Uzoefu wa uongozi wa mikoa unaweza kuwa faida kubwa kwa Makamu wa Rais kwa sababu nafasi hiyo inahitaji kuelewa changamoto za wananchi nje ya Dar es Salaam na Dodoma.
Kwa hakika, Mtaka amekuwa na mikoa aliyopewa dhamana kuiongoza, huku wengi wakidhani ingekuwa changamoto kwake kutokana na kuwa pembezoni, lakini akaigeuza kuwa fursa. Mikoa ya Simiyu, Dodoma na sasa Njombe aliyoiongoza imethibitisha kuwa yeye ni mmoja wa wasuluhishi na wapatanishi.
Mtaka amekuwa karibu na vijana si tu kupitia mikutano ya hadhara, bali hata kwenye mitandao ya kijamii. Anazungumza nao “meme” na, kwa hakika, anayo sifa ya ziada. Ni mnyenyekevu. Bila kujali wadhifa wake, haoni aibu kumwamkia mtu anayemzidi umri hadharani. Si viongozi wengi wanaofanya hivyo. Si mtu wa kupandisha mabega.
Faida nyingine ni kwamba anatokea katika Kanda ya Ziwa, yenye mikoa sita na Watanzania milioni 16.4, karibu theluthi moja ya Watanzania wote. Mikoa hii haina kiongozi wa juu serikalini; hiyo Mtaka anayo nafasi ya kuwa mwakilishi sahihi. Umri wake pia, unamweka kwenye kundi la vijana wanaotafuta kubadili upepo wa kiuchumi kwa vijana wenzao.

Sitanii, katika majina yote haya, kuna jambo moja ambalo ningependa Rais Samia alitazame kwa umakini. Makamu wa Rais ajaye asiwe tu mtu anayemsaidia Rais kuendesha Serikali; awe mtu anayemsaidia Rais kuunganisha Tanzania. Waziri Mkuu ndiye aendeshe Serikali.
Tanzania imeingia katika kipindi tofauti na kisiasa zimeongezeka, mjadala wa Katiba Mpya umechukua nafasi kubwa, uchaguzi wa 2025 umeacha maswali na majeraha kwa baadhi ya Watanzania, na mjadala kuhusu haki za kiraia na utawala wa sheria umeongezeka.
Hivyo, Makamu wa Rais ajaye anapaswa kuwa mtu ambaye akizungumza, watu wa CCM wamsikilize, wapinzani wamsikilize, vijana wamsikilize, Zanzibar wamsikilize, Bara wamsikilize, Waislamu wamsikilize, Wakristo wamsikilize, Walokole wamsikilize na hata wale wasiokubaliana na Serikali waseme: “Hakika huyu ni kiongozi anayetusikia.”
Hapo ndipo ninapoona uzito wa historia ya viongozi waliowahi kujiuzulu Tanzania. Mzee Mwinyi alijiuzulu kwa sababu aliona dhamana ya kisiasa iliyokuwa mbele yake ilihitaji uwajibikaji. Jumbe aliondoka katika mazingira ya mgogoro wa Muungano. Lowassa na mawaziri wenzake waliwajibika katika Richmond. Muhongo aliondoka katika Escrow. Polepole aliondoka na baadaye kueleza hadharani masuala yaliyomsukuma. Nchimbi sasa ameondoka akisema Rais anataka mabadiliko.
Hii ndiyo maana ya uongozi: madaraka si mali ya mtu. Unapewa kwa dhamana na yanaweza kuachwa pale mazingira yanapobadilika.
Kwa vyovyote iwavyo, narudia, tunahitaji wapatanishi. Serikali hii mpya ikianza kazi, basi ifanye mawasiliano ya haraka na ya karibu na wananchi. Nasema bila woga kuwa kuna kosa la kiufundi katika mawasiliano serikalini. Serikali inafanya mambo makubwa, lakini mawasiliano hayawafikii wananchi kwa ufasaha.
Naangalia wasemaji wa nchi kubwa kama Urusi na Marekani, wanaripoti moja kwa moja kwa Mkuu wa Nchi. Hapa kwetu, Msemaji Mkuu anaripoti kwa Waziri. Vyeo vimeunganishwa, anakuwa Msemaji na Katibu Mkuu. Mshika mbili, moja humponyoka.
Hii inampunguzia uwezo wa kiutendaji. Msemaji Mkuu wa Serikali anapaswa kuwasiliana na Wizara zote zikampatia cha kusema. Sasa akiwa ameunganisha vyeo au yupo chini ya Waziri, nakuhakikishia hadi siku ya mwisho hatakaa awe msemaji. Hili tulisahihishe.
Sitanii, nikirejea katika hoja ya msingi, katika kumtafuta atakayechukua nafasi ya Dk. Nchimbi, tusitafute mtu anayejua kusema “ndiyo” kwa kila jambo. Tusitafute pia mtu anayejua kusema “hapana” kwa kila jambo. Tafuteni mtu anayejua lini na wapi pa kusema ndiyo, lini na wapi pa kusema hapana na, kama ni hapana ajue kuisema kiungwana bila ukakasi na bado aeleweke.
Muhimu zaidi, ajue lini atapaswa kukaa kimya na lini atapaswa kuwakutanisha watu watu wenye mitazamo tofauti. Hizi zimekuwa sifa muda wote. Tanzania inaendelea kumhitaji Makamu wa Rais mwenye busara, uvumilivu, uzoefu, uadilifu, uwezo wa kusikiliza na moyo wa Muungano.
Kwa maoni yangu, kama kipimo kikuu ni kuunganisha nchi, uchambuzi nilioufanya kwa uwazi kabisa bila hata kuambiwa, naamini hata wewe msomaji kuna ambao tayari umewaondoa kwenye orodha hii inayotajwa. Lakini mwisho wa siku, Makamu wa Rais si tu nafasi ya pili kwa ukubwa, bali ni nafasi ya pili kwa dhamana.
Na dhamana hiyo kwa Tanzania ya leo inahitaji mtu anayefahamu uwajibikaji wa pamoja zaidi kuliko kitu kingine chochote: mtu wa kuunganisha nchi.
Inahitaji mtu ambaye hata atakaposhauri na ushauri wake ukakataliwa, hatakuja hadharani kusema nilishauri, ushauri ukakataliwa. Hata akishauri na ushauri ukachukuliwa, hatasimama hadharani kusema hiki kinachotekelezwa kama si mimi kisingekuwa.
Namshukuru Dk. Nchimbi kwa uamuzi aliouchukua. Wakati mwingine, kama binadamu, ni vyema ukiona unayemsaidia hampikiki tena chungu kimoja, unampisha, na unaendelea kumsaidia kutokea pembeni. Naamini Balozi Nchimbi ni mtu mwema, ataendelea kuisaidia Serikali, japo kwa ushauri.
Sitanii, ni matarajio yangu atapatikana Makamu wa Rais na nchi yetu haitatumbukia tena kwenye mgogoro kama tulioushuhudia kati ya mwaka 2007 hadi 2015 kati ya Lowassa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, uliotupeleka katika msamiati wa “kuvua gamba”, tukaishia kupiga siasa kama nchini na kusahau maendeleo kwa kipindi chote hicho.
Naomba Makamu wa Rais apatikane, amani itamalaki, maridhiano ya kitaifa kati ya chama tawala na wapinzani yaanze haraka na hatimaye sote tuelekeze macho mbele kuelekea Dira 2050.
Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

