Na Benny Mwaipaja, Addis Ababa

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khams Mussa Omar, amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo asilimia 100 ya kaya zitakuwa zimesajiliwa katika Mpango wa Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika rasilimali watu, kuimarisha huduma za jamii na kuchochea mageuzi ya uchumi yanayowanufaisha wananchi wote.

Mhe. Balozi Omar ametoa rai hiyo Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, wakati akishiriki kama mwanajopo katika mjadala wa Mawaziri wa Fedha, kuhusu “Ufadhili Endelevu wa Afya: Kugharamia Mustakabali wa Afya Barani Afrika katika Kipindi cha Ufinyu wa Bajeti na Kujitegemea katika Masuala ya Afya.” kabla ya Kikao cha Sabini na Sita cha Kamati ya Kanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika.

Alisema kuwa usajili wa wananchi katika mpango huo hivi sasa umefikia asilimia kumi na kwamba jitihada zinafanywa na Serikali kuhakikisha kuwa katika mwaka wa fedha 2028/2029 kaya zote zitakuwa zmesajiliwa katika mfumo huo, na kwamba kaya masikini na zilizo katika mazingira hatarishi zitagharamiwa na Serikali.

Alitaja vyanzo muhimu vitakavyo imarisha ufadhili wa utoaji wa huduma za afya nchini kuwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi, ukusanyaji bora wa mapato ya ndani, kodi zinazolenga bidhaa hatarishi kwa afya, matumizi bora ya fedha za umma, Bima ya Afya kwa Wote, uwekezaji wa sekta binafsi na mifumo bunifu ya ufadhili akisisitiza kuwa ufadhili wa afya kuwa moja ya vipaumbele vya kitaifa.

Aidha, alisema kuwa Serikali inaendelea kupanua Mfuko wa Usawa wa Afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi maskini na walio katika mazingira hatarishi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, alisema kuwa Tanzania, imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kwa kuongeza bajeti ya sekta ya afya pamoja na kuboresha miundombinu ya matibabu kwa kuwa afya ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

Mhe. Dkt. Samizi alisema kuwa kujitegemea kiafya kunamaanisha kuwa na uwezo wa kugharamia huduma na kuzalisha dawa pamoja na teknolojia muhimu karibu na wananchi hivyo aliitaka sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa dawa, vipimo vya uchunguzi, huduma za kibingwa, teknolojia za tiba na mifumo ya afya ya kidijitali

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, alisema kuwa suala la afya ni muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote na kuzishauri nchi za Afrika kuwekeza kwenye mambo matatu ikiwemo kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na chanjo, kuimarisha afya ya msingi na kutekeleza mpango wa huduma ya afya kwa wote ili kila mtu katika nchi hizo awe na uhakika wa kupata huduma za afya.

Alisema kuwa asilimia 80 ya mahitaji ya dawa zinazohitajika zinaagizwa nje ya Bara la Afrika huku baadhi ya wananchi katika nchi za Afrika wakitoa fedha zao zaidi ya asilimia 70 kwa ajili ya kulipia matibabu kutoka mifukoni mwao na akatoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda hivyo vya dawa na chanjo pamoja na miundombinu mingine itakayosaidia ustawi wa rasilimali watu.

Mjadala huo uliwakutanisha Mawaziri wa Afya na Fedha, washirika wa maendeleo, pamoja na viongozi wa kikanda ili kubadilishana mitazamo kuhusu shinikizo la kifedha linaloathiri maendeleo kuelekea huduma za afya kwa wote (UHC). Shinikizo hilo linajumuisha kupungua kwa misaada kutoka nje, ufinyu wa bajeti, na kuongezeka kwa mzigo wa madeni.

Mkutano huo umemshirikisha pia Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw Rished Bade, pamoja na baadhi ya wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Omar (Mb), akishiriki kama mwanajopo katika mjadala wa Mawaziri wa Fedha na Afya, kuhusu “Ufadhili Endelevu wa Afya: Kugharamia Mustakabali wa Afya Barani Afrika katika Kipindi cha Ufinyu wa Bajeti na Kujitegemea katika Masuala ya Afya.” kabla ya Kikao cha Sabini na Sita cha Kamati ya Kanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika, Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Addis Ababa
Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Omar (Mb), (wa sita mstari wa pili mbele-kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Afya na baadhi ya Mawaziri wenzake wa Fedha pamoja na wadau mbalimbali aliposhiriki kama mwanajopo katika mjadala wa Mawaziri wa Fedha na Afya, kuhusu “Ufadhili Endelevu wa Afya: Kugharamia Mustakabali wa Afya Barani Afrika katika Kipindi cha Ufinyu wa Bajeti na Kujitegemea katika Masuala ya Afya.” kabla ya Kikao cha Sabini na Sita cha Kamati ya Kanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika, Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.