Dar es Salaam
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) iko katika hatua za mwisho za kukamilisha hati mbili za makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Tume ya Usimamizi wa Mali za Serikali za China (SASAC) pamoja na Jumuiya ya China ya Mageuzi na Maendeleo ya Mashirika (CERDS), katika hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, utafiti na kuimarisha uwezo katika usimamizi wa mali za Serikali.
Hayo yalisemwa Jumatano, Agosti 26, 2026, na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na ujumbe wa wataalamu kutoka SASAC.
Bw. Mchechu alisema makubaliano hayo, yanayotarajiwa kuwa tayari ifikapo Ijumaa au Jumatatu ijayo, yanalenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo kupitia kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaalamu katika maeneo ya utafiti, ujenzi wa uwezo wa taasisi, sera, mageuzi ya utawala bora na tathmini ya utendaji.
Alisema ushirikiano huo utawezesha Tanzania kujifunza kutoka China katika usimamizi wa mali za Serikali, mageuzi ya mashirika ya umma yanayoongozwa na misingi ya soko, usimamizi wa utendaji pamoja na kuongeza ubora na ufanisi wa mtaji wa Serikali.
“Kupitia uhusiano wetu wa pande mbili na SASAC, tunalenga kujifunza namna China ilivyofanikiwa kufanya mageuzi na kuelekeza mtaji wa Serikali katika sekta muhimu za kimkakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema.
Kwa sasa, OTR inasimamia taasisi za umma 308, zikiwamo 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na 56 ambazo Serikali inamiliki hisa chache.
Rais wa CERDS, Peng Huagang, alisema uzoefu wa China unaonesha umuhimu wa kuendesha mashirika ya umma kwa misingi ya soko huku yakitekeleza majukumu ya kimkakati kwa taifa.
“Tafsiri ya mageuzi ya mashirika ya umma ni kuyafanya kuwa imara zaidi, bora zaidi na kuwa mashirika ya kiwango cha dunia yanayoendeshwa kwa misingi ya soko,” alisema.
Bw. Peng alisema mageuzi yanayozingatia misingi ya soko ni muhimu katika kuongeza ushindani wa mashirika ya umma, huku usimamizi wa mali za Serikali ukihakikisha mali hizo zinalindwa na kuongezeka thamani bila kuingilia uhuru wa menejimenti katika uendeshaji wa taasisi.
“Mageuzi yanayozingatia misingi ya soko ndiyo njia ya msingi ya kuongeza ushindani wa mashirika ya umma, na kuyawezesha kufanya kazi kwa ufanisi sambamba na aina nyingine za umiliki,” alisema.

Bw. Peng alisema ushirikiano huo unaendana pia na mahusiano ya muda mrefu kati ya Tanzania na China pamoja na utekelezaji wa ahadi zilizowekwa kupitia Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Alitaja ufufuaji wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuunganisha korido za usafirishaji na sekta za madini, kilimo, usafirishaji na viwanda.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi na wataalamu kutoka OTR, SASAC na CERDS, Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, pamoja na viongozi waandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dkt. Boniphace Nobeji, alisema uboreshaji wa utendaji na ufanisi wa bandari nchini una umuhimu mkubwa katika kukuza biashara na maendeleo ya kiuchumi ya ukanda.
“Tunaamini ustawi wa taifa lolote unatokana na biashara, na sehemu kubwa ya biashara inawezeshwa na bandari zenye ufanisi. Hakuna shaka kwamba maboresho katika utendaji na ufanisi wa TPA yataharakisha maendeleo ya kiuchumi ya Afrika Mashariki na Kati,” alisema Dk Nobeji.
Alitaja uendelezaji wa bandari kavu, uhamishaji wa teknolojia, ujenzi wa uwezo na kujifunza kutoka kwa uzoefu wa China katika usimamizi wa bandari kuwa miongoni mwa maeneo ya ushirikiano.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, alitaja fursa za uwekezaji kuwa ni vituo vya usafirishaji wa mizigo, uendeshaji binafsi wa huduma za usafirishaji wa mizigo, kongani za viwanda zinazohusishwa na vituo vya reli pamoja na vituo shirikishi vya usafirishaji wa mizigo.
Alisema pia kuna fursa ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) katika ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kando ya korido za reli, ambapo wawekezaji binafsi wanaweza kurejesha mitaji yao kupitia tozo zinazohusishwa na kiasi cha mizigo kinachosafirishwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mkuu Mtendaji wa ATCL, Bw John Nzunda, alitaja usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga, matengenezo na uhandisi, teknolojia za kidijitali, usimamizi wa mafuta na mafunzo maalumu kwa wataalamu wa sekta ya anga kuwa maeneo yanayoweza kuimarisha ushirikiano na mashirika ya umma ya China.
Mkurugenzi Mtendaji wa CCECC East Africa Ltd, Bw Lu Haiqiang, amesema kampuni hiyo iko tayari kuimarisha ushirikiano na mashirika ya umma ya Tanzania katika maeneo ya miundombinu, uhandisi, ujenzi na uendeshaji.
Alitaja ufufuaji wa TAZARA kuwa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, akisema reli hiyo inaweza kuunganisha korido muhimu za biashara na shughuli za madini, kilimo, usafirishaji na vituo vya viwanda.


