Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia

Shirika la AAWORD limewapatia mafunzo zaidi ya wanafunzi 100 wa Shule ya Sekondari Keko, kuhusu namna ya kurejesha taka ngumu na kuzibadilisha kuwa bidhaa zenye thamani.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo,Mratibu wa Vijana wa Shirika la Active African Women for Research and Development (AAWORD), Magdalena
Bagile, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu kwa vijana katika kuwajengea uelewa kwenye matumizi ya taka ngumu kuwa mapambo ya kujipatia kipato.

Amesema kwa sasa Vijana wanahitaji kupewa maarifa ya vitendo, yatakayo
wawezesha kushiriki katika utunzaji wa mazingira huku wakitengeneza fursa zitakazoweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.

‘’Katika mafunzo, wanafunzi walipata fursa ya kujadili maana ya mazingira, athari za uchafuzi wa mazingira na namna taka ngumu zinavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye matumizi na thamani.

Pia walifanya kazi kwa makundi, wakabuni mawazo mbalimbali ya bidhaa zinazoweza kutengenezwa kutokana na taka.

Walijifunza kutumia chupa za plastiki kutengeneza vyungu vya maua, pamoja na kuzibadilisha kuwa bidhaa mbalimbali pia namna ya kutengeneza mikeka na mazulia kwa kutumia nguo zilizotumika pamoja na mifuko ya unga’’amesema

Magdalena amesema amesema katika kipindi ambacho ajira ni changamoto kwa vijana wengi, ujuzi wa vitendo unaotokana na ubunifu na matumizi ya taka unaweza kuwa msingi wa ujasiriamali na chanzo cha kipato hapo baadaye.

“Tunapowapa vijana ujuzi huu, hatuwafundishi tu namna ya kutunza
mazingira, bali pia tunawapa uwezo wa kuona taka kama rasilimali na
changamoto kama fursa,” amesema

Amesema vijana wakipata ujuzi, mazingira wezeshi na fursa za kuendeleza ubunifu wao, wanaweza kuwa sehemu muhimu ya kutatua changamoto za uchafuzi wa mazingira katika jamii
.

Kwa upande mwingine, shughuli hizo zimeonyesha umuhimu wa elimu ya
mazingira kuhusishwa na vitendo, ili wanafunzi wasibaki na maarifa ya darasani

‘’AAWORD inaamini kuwa kuwajengea vijana uwezo wa kutumia taka ,ngumu
kama malighafi kunaweza kusaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Keko Rushubilwa Robert amesema mafunzo
hayo hayakuhusu kutengeneza bidhaa kutokana na taka pekee, bali
yalikuwa sehemu ya kuwajengea vijana uwezo wa kubuni, kuvumbua na
kutengeneza fursa, sambamba na kushiriki katika kulinda na kurejesha mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Agatha Katamba amesema mafunzo hayo yamemfundisha namna ya kurejesha
taka ngumu na kuzibadilisha kuwa mapambo,ambapo kijana linaweza
kumsaidia kujitegemea kwa kujipatia kipato .

“Mafunzo ya leo yamenifundisha jinsi ya kurejesha taka ngumu na kuzibadilisha kuwa mapambo,ujuzi huu unaweza kunisaidia kujitegemea na kujipatia kipato pale nitakapokuwa sina ajira,” amesema.

Fausali Saidi amesema amejifunza kuwa chupa za plastiki na taka nyingine ngumu zinaweza kubadilishwa kuwa rasilimali zinazoweza kutumika tena na kuwa chanzo cha kipato.

“Mafunzo haya yamenifanya nijue kuwa chupa na taka ngumu zinaweza
kubadilishwa kuwa rasilimali ambayo binadamu anaweza kuitumia tena na
kujipatia kipato,” amesema .


Abdalaa Alfani amesema amejifunza kuwa ujasiriamali unaweza kujengwa
kupitia matumizi ya taka ngumu kwa kutengeneza vifaa mbalimbali
vinavyoweza kuuzwa na kuongeza kipato chake.

Kupitia mafunzo hayo, zaidi ya wanafunzi 50 wa Keko Sekondari wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwamba taka zinaweza kuwa na thamani.