Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema iwapo chama hicho kitashika madaraka Zanzibar, watampendekeza Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Othman aliyasema hayo Agosti 25, 2026 katika Ukumbi wa Elimu Mbadala, Wilaya ya Kusini Unguja, alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya ACT Wazalendo na CCM.

Alisema ACT Wazalendo inalenga kuendesha nchi kwa misingi bora, hivyo inahitaji viongozi wenye uwezo na uadilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Tukishika madaraka, chama chetu tunataka kuendesha nchi kwa misingi iliyobora na watu wake lazima wawe bora,” alisema Othman.

Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema licha ya Jussa kueleza kuwa hataki kushika nafasi za Serikali na badala yake angependa kujikita katika shughuli za chama, iwapo ACT Wazalendo itashika madaraka, watamteua kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi.

“Baraza linataka mtu madhubuti Ismail Jussa ambaye ataliendesha katika misingi ya uadilifu wa hali ya juu,” alisema.

Aidha, Othman alisema uzalendo ndio uliowasukuma kufikia makubaliano yaliyolenga kuondoa mkwamo wa kisiasa Zanzibar.

Alisema mambo saba yaliyokubaliwa na kusainiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo yanaweza kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua kiuchumi na kimaendeleo.

Aliwataka wananchi kuondoa hofu kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo, akisisitiza kuwa yatatekelezwa kwa wakati uliowekwa na pande hizo.

“Madhumuni yetu ni kuinyoosha nchi pale ambapo imepinda ili iongozwe kwa misingi ya haki,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, aliwataka viongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kujiandaa na kujenga ofisi za kisasa za chama zitakazowezesha shughuli za chama kufanyika kwa mtindo wa kisasa.

Alisema lakini uimarishaji wa chama hauishii katika ujenzi wa majengo pekee, bali unahusisha pia kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa vikao na shughuli za chama kwa kuzingatia katiba na taratibu zilizowekwa.

“Mbali ya majengo, lazima tukaimarishe chama hiki. Vikao vya chama vifanyike kwa mujibu wa katiba na taratibu tulizojiwekea wenyewe,” alisema Jussa.

Jussa aliwataka viongozi na wanachama kujipanga upya, akisema kumalizika kwa uchaguzi kunapaswa kuwa mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi unaofuata.

Alisema anajivunia Wilaya ya Kusini Unguja kwa namna viongozi na wanachama wanavyojitolea kukiimarisha chama licha ya changamoto wanazokabiliana nazo za kimaisha

Jussa alisema wananchi wanakitegemea ACT Wazalendo kuja kuwakomboa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo suala la wananchi kuporwa ardhi zao.

“Msingi wa harakati hizi ni kupigania haki za watu na jambo jingine ni hadhi na heshima ya nchi yetu,” alisema.

Naye Mwenyekiti Mstaafu wa ACT Wazalendo, Babu Juma Duni Haji, alisema hana wasiwasi kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo, akieleza kuwa Rais wa Zanzibar aliahidi mbele ya umma kuwa yote yaliyokubaliwa yatatekelezwa kwa njia zilizowekwa na pande hizo.

Mapema, akitoa maelezo kuhusu kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, alisema chama hicho kinaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na kuwa na safu imara ya viongozi kuanzia ngazi ya Taifa hadi majimbo.

Mwenyekiti katika ziara hiyo ameongozana na viongozi mbali mbali wakiwemo wajumbe wa Baraza la wawakilishi kupitia chama hocho wakiongozwa na mnadhimuwa baraza la wawakilishi Pro. Fakih Hamad , Katibu wa Habari na Uenezi Salim Biman , pamoja niongozi wa mikoa na wajimbe wa Halimashauri kuu na kamati kuu za taifa.