Na Francisco Peter, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. BashirAlly Kakurwa, leo Agosti 24, 2026 amefungua Kongamano la Nne la Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji (4tFAR4ViBE) linalowakutanisha Wanasayansi, watafiti na wadau wa uvuvi na wakuzaji viumbe maji na wataalam wa vyuo vikuu kutoka katika Nchi 17 ikiwemo mwenyeji Tanzania kujadili kuhusu maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji na kuweka wazi kiwa sekta ya uvuvi zinahitaji sayansi na tafiti ili kuwanufaisha wavuvi.

Kongamano hilo linalofanyika kwa siku tatu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere International Convetion Center (JNICC) Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amewasisitiza wataalam hao kutumia kongamano hilo kujadili kwa kina jinsi ya kutumia sayansi na tafiti kwa ajili ya uvuvi endelevu na ukuzaji viumbe maji.

“Shughuli za uvuvi ni sayansi, ni jambo linalohitaji utaalam wa wanasayansi na shughuli nyeti katika usalama wa chakula katika dunia yetu, ndio maanda leo nimekuja kuzindua Kongamano lao la Siku tatu lengo kubwa ni kuhakikisha shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji zinafanyika kisayansi, kisasa, zinatumia nyezo za kisasa na ubunifu ili wavuvi wadogo waweze kunufaika na jasho lao” amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Isamel Kimirei ameeem wataalam wakiwemo wanasayansi, watafiti, wasomi wa vyuo Vikuu, wadau wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji kutoka Nchi 17 duniani watajadili taarifa mbalimbali za kisayansi na tafiti ili kuiwezesha sekta ya uchumi wa buluu kuwa endelevu na kuwa na mchango katika uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Katika hatua nyingine Mhe. Waziri Balozi Dkt. Bashiru ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa meli 3 za Uvuvi wa Bahari Kuu kati ya serikali kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na ambapo amesema ujenzi wa meli hizo utasaidia kwenda kuvua samaki bahari pamoja kuifanya bandari ya Uvuvi Kilwa kuwa na tija.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema mpango wa serikali ni kuwa na meli sita kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu ambapo meli nne zitakuwa Tanzania Bara chini ya Usimamizi wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Meli mbili zitakuwa Zanzibar na kutoa rai kwa watekelezaji wa mradi kuzingatia muda na kwa ufanisi ili meli hizo zianze kufanya kazi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani amesema katika kipindi cha miezi tisa tangu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally akabidhiwe kuiongoza wizara hiyo, kumekuwa na hatua nzuri na muhimu za kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ikiwa ni pamoja na hatua hii ya ujenzi wa meli kwa ajili ya Uvuvi wa Bahari Kuu.