Na, Mwandishi Wetu, Ulaanbaatar, Mongolia
Tanzania inashiriki Mkutano wa Kumi na Saba wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD COP 17) unaofanyika katika Jiji la Ulaanbaatar nchini Mongolia.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiambata na Ujumbe wa Tanzania wameshiriki Mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Mongolia Mhe. Khurelsukh Ukhnaa, Agosti 24, 2026.
Mhe. Masauni amesema Mkutano huo umeweka msisitizo kupitia kaulimbiu yake ya “Ongoa Ardhi, Ongoa Matumaini”, kaliuambiu ambayo inasisitiza kuongeza uwekezaji katika urejeshaji wa ardhi, ustahimilivu dhidi ya kuenea kwa hali ya jangwa, ukame na usimamizi endelevu wa maeneo ya malisho.
Aidha, Mwaka 2026 pia umetangazwa kuwa Mwaka wa Wafugaji na nyanda za Malisho jambo linalofanya ajenda ya Tanzania kuhusu uhifadhi wa malisho na ustawi wa wafugaji kuwa muhimu zaidi katika mkutano huu.
“Kwa Tanzania, changamoto ya uharibifu wa ardhi inahusishwa na sababu mbalimbali, zikiwemo ukataji na uharibifu wa misitu, upanuzi wa mashamba kwaajili ya kilimo, uchomaji moto usiodhibitiwa, mmomonyoko wa udongo, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na uendelezaji wa makazi.”
“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unatoa fursa ya kupata uzoefu, teknolojia, ushirikiano na rasilimali za kifedha kwa ajili ya kuimarisha usimamizi endelevu wa malisho, urejeshaji wa ardhi iliyoharibika, uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji na bioanuwai, pamoja na kuongeza ustahimilivu wa jamii za wakulima na wafugaji katika kupambana na kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.” Amesema Mhe. Masauni.
Kwa upande wake, Afisa Kiungo wa Mkataba huo kutoka Tanzania Bw. Thimoth Mande amesema Ushirikiano huu unawezesha Tanzania kushughulikia kwa pamoja changamoto za uharibifu wa ardhi, upotevu wa bioanuwai na mabadiliko ya tabianchi, badala ya kuzishughulikia kama changamoto zinazojitegemea.
Amesema, ushiriki wa Tanzania si wa kuhudhuria mkutano pekee, bali ni fursa ya kuonesha hatua ambazo tayari Tanzania inachukua katika kupambana na changamoto hii, huku ikiomba kuongezewa uwekezaji na teknolojia.
Tanzania inaweza kutumia matokeo ya mkutano huu kuhamasisha rasilimali zaidi kutoka katika mifuko ya kifedha za mazingira kama vile GEF, IFAD, UNDP, FAO, UNEP, sekta binafsi na mifumo bunifu ya fedha, ili kuongeza miradi hii kutoka kiwango cha maeneo maalum kwenda maeneo makubwa zaidi.
Naye, Meneja wa Kanda ya Mashariki Kusini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bi. Aminata Kirama amesema Baraza hilo linalowajibu wa kufanya kupitia maeneo ambayo yamebainishwa hasa katika kufanya tafiti.






