Na Peter Haule, WF, Manyara

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, ametoa rai kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya, kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Bw. Mwenda ametoa rai hiyo wakati akiongoza Timu ya Hazina Social Runners iliyoshiriki mbio za Manyara Tanzanite Marathon zilizofanyika Babati mkoani Manyara, huku yeye mwenyewe akikimbia umbali wa kilometa 21, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo.

Alisema watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano katika masuala mbalimbali yenye kutoa hamasa kwa wananchi, ikiwemo kushiriki katika michezo na mazoezi, hatua inayosaidia kujenga jamii yenye afya, nguvu kazi na utimamu wa mwili na akili.

“Uwekezaji katika afya za watumishi ni sehemu muhimu ya kuongeza tija katika utendaji wa kazi, kwa kuwa mtumishi mwenye afya njema ana uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hususan anapokuwa na utimamu wa mwili unaotokana na kushiriki katika mazoezi na michezo mbalimbali,” alisema Bw. Mwenda.

Aidha, Bw. Mwenda aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuwekeza katika afya za watumishi kupitia upimaji wa afya pamoja na kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za michezo, ikiwemo mazoezi, marathoni na mbio za nyika.

Alisema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya bora, hali inayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza tija katika utumishi wa umma.

Aliongeza kuwa kutofanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa mengine, ambayo yanaweza kuathiri afya ya mtu binafsi na kupunguza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.

Katika mbio hizo, Timu ya Hazina Social Runners ilikuwa na jumla ya washiriki 34 kutoka Wizara ya Fedha, walioshiriki katika mbio za umbali tofauti kuanzia kilomita tano hadi 21, ikionesha dhamira ya Wizara ya Fedha ya kuhamasisha watumishi kujenga utamaduni wa mazoezi na michezo, kwa kutambua kuwa afya bora ni msingi wa utendaji wenye tija na maendeleo endelevu.

Mbio za Manyara Tanzanite Marathon zililenga pia kuchangisha takribani shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la watoto njiti katika Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara.