Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaofanywa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la lake la kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira katika miradi ya maendeleo nchini.

Ushiriki wa NEMC katika uzinduzi wa mradi huu wa kimkakati unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa maendeleo ya sekta ya nishati yanaenda sambamba na ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Akieleza ushiriki wa NEMC katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema NEMC inaendelea kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi wa JNHPP unazingatia Sheria, Kanuni, miongozo na masharti ya mazingira yaliyowekwa.

Amesema katika kutekeleza majukumu yake, NEMC imeendelea kufuatilia uzingatiaji wa masharti ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM), ikiwemo ufuatiliaji wa ubora wa maji, hewa na udongo, usimamizi wa taka, udhibiti wa uchafuzi pamoja na utekelezaji wa hatua za kupunguza athari za kimazingira.

Aidha, NEMC inaendelea kusimamia masuala ya uhifadhi wa bioanuwai, ulinzi wa Mto Rufiji na mifumo yake ya ikolojia, kuhakikisha shughuli za mradi zinafanyika kwa kuzingatia wajibu wa kulinda mazingira na rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

NEMC itaendelea kushirikiana na Serikali, taasisi na wadau mbalimbali katika kuhakikisha JNHPP, kama mradi muhimu wa kimkakati kwa Taifa, unatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu, huku ulinzi wa mazingira ukipewa kipaumbele. NEMC: Mazingira Salama, Maendeleo Endelevu.