- Ataka kazi ifanyike usiku na mchana inapowezekana;
- Asisitiza mashindano hayo ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Tanzania;
*Awataka wakandarasi kukamilisha mikataba ya wafanyakazi na kushughulikia stahiki zao ndani ya wiki moja.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kuongezwa kasi ya ujenzi wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ili vikamilike kwa wakati na kukidhi viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesema kazi hiyo inapaswa kufanyika kwa kasi, ikiwemo kuongeza muda wa kufanya kazi pale inapobidi, ili viwanja vikamilike kwa wakati na Tanzania iwe tayari kabla ya ukaguzi wa maandalizi unaotarajiwa kufanywa na CAF.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo (Ijumaa, Agosti 21, 2026) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa viwanja vya mazoezi vya Farasi na Leaders Club jijini Dar es Salaam, ambavyo ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumika katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Amesema Tanzania haipaswi kusubiri hadi dakika za mwisho kukamilisha maandalizi yake kwa sababu CAF inahitaji kujiridhisha mapema kuwa miundombinu inayohitajika iko tayari.
“Twendeni tufanye kazi usiku na mchana tumalizie asilimia iliyosalia. Wenzetu wanaosimamia mashindano hawawezi kurisk tu kwamba tuko tayari, wanataka wajionee kwamba tuko tayari kukiwa bado kuna muda wa kutosha,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema mashindano ya AFCON hayapaswi kutazamwa kama tukio la michezo pekee, bali ni fursa kubwa ya kiuchumi ambayo Tanzania inapaswa kujiandaa kuitumia kikamilifu.
“Hii si michezo tu, bali pana uchumi ndani yake,” amesema na kuongeza kuwa baada ya kukamilisha miundombinu, nchi inapaswa kuelekeza nguvu katika kujiandaa kimkakati ili kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazoambatana na mashindano hayo.
Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu pia ametoa maelekezo ya kushughulikia malalamiko ya wafanyakazi wanaoshiriki ujenzi wa viwanja hivyo, hususan kuhusu mikataba ya ajira, malipo ya muda wa ziada na stahiki nyingine.
Ameagiza Wizara yenye dhamana, wasimamizi wa miradi na wadau wengine kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa mikataba yao ndani ya wiki moja, huku hesabu za mishahara, malipo ya muda wa ziada na stahiki nyingine zikihakikiwa kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa.
“Suala la mikataba lishughulikiwe haraka, lakini pia wazingatie hizi hesabu walizozisema wafanyakazi. Hoja yao inaeleweka,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua uzalendo uliooneshwa na wafanyakazi hao kwa kuendelea na kazi licha ya changamoto walizozieleza, hivyo akaagiza masuala yao yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na makubaliano yaliyopo.
Aidha, amesisitiza kuwa mikataba hiyo izingatie kipindi ambacho wafanyakazi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwenye miradi hiyo.
Katika uwanja wa Leaders Club, Waziri Mkuu amewapongeza wafanyakazi kwa kuendelea kuchapa kazi na kuwataka waongeze juhudi ili miradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia changamoto za wafanyakazi sambamba na kuhakikisha kasi ya ujenzi wa miundombinu inaongezeka, kutokana na umuhimu wa AFCON kwa uchumi, michezo na maendeleo ya nchi.
“Tusimwangushe Mheshimiwa Rais. Amejitoa sana kuhakikisha nchi yetu inakuwa mwenyeji wa mashindano haya. Twendeni tukamilishe kwa wakati,” amesema.
Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, alisema viwanja vya Farasi na Leaders Club ni sehemu ya miundombinu inayojengwa ili kukidhi mahitaji ya CAF kwa ajili ya AFCON 2027.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, amesema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa karibu, sambamba na kushughulikia masuala ya wafanyakazi kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na masuala ya ajira na hifadhi ya jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu, ujenzi wa uwanja wa Farasi ulikuwa umefikia asilimia 74 na unatarajiwa kufikia zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwisho wa mwezi huu, wakati ujenzi wa uwanja wa Leaders Club ukiendelea kwa kasi kuelekea hatua zinazotakiwa katika ratiba ya maandalizi.
Uwanja wa Farasi unajengwa kama uwanja wa mazoezi wenye vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya waamuzi, madaktari na huduma nyingine muhimu, pamoja na mfumo wa kisasa wa kuondoa maji uwanjani.
Kwa upande wa Leaders Club, pamoja na huduma hizo, uwanja huo utakuwa na jukwaa lenye uwezo wa kuchukua takribani watazamaji 2,500.










