Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewataka watafiti nchini kuhakikisha tafiti wanazofanya katika sekta ya usafiri na usafirishaji zinatoa suluhisho la changamoto halisi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi, badala ya kuishia kwenye makabrasha na mikutano.
Akifungua Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Usafiri, Lojistiki na Usimamizi jana Agosti 20, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema Serikali inahitaji tafiti zitakazosaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa bandari na reli, kuboresha usalama wa usafiri pamoja na kuimarisha miundombinu inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya usafiri ikiwemo reli ya SGR, bandari, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mabasi yaendayo Haraka (BRT), barabara pamoja na usafiri wa majini.
Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo hiyo ili kujenga mfumo mmoja wa usafiri wenye ufanisi, unaopunguza gharama na muda wa kusafirisha abiria na mizigo, hatua ambayo amesema itasaidia kuongeza ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
“Haipaswi uchumi ukue halafu usafiri ufuate; usafiri wenyewe lazima uwe kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini na miundombinu ya usafiri inapaswa kuzalisha fursa za biashara, ajira na uwekezaji,” amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kuwasilisha mapendekezo yanayotekelezeka na yenye matokeo yanayoweza kupimika, akisema mafanikio ya tafiti hayapaswi kuishia katika machapisho au mijadala pekee, bali yaonekane katika kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi na kuboresha usalama.
Amesema utekelezaji wa matokeo ya tafiti hizo pia unapaswa kusaidia Tanzania kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa, huku sekta ya usafiri ikiwa sehemu muhimu ya kuchochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Mkutano huo unalenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usafiri, lojistiki na usimamizi, pamoja na namna tafiti na ubunifu vinavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuchangia maendeleo ya taifa.





