Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Benki ya Dunia imesifu uhusiano kati yake na Tanzania na kusifu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kusimamia vizuri wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam chini ya mpango unaofadhiliwa na benki hiyo.

Mpango huo unajulikana kwa jina la Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP), awamu ya kwanza imekwisha na Benki ya Dunia imeahidi kufikiria kufadhili awamu ijayo.

Akizungumza jana jijini hapa mara baada ya kikao kifupi na wajumbe wa TPA, Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshuhulikia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, alisema kuwa maboresho yaliyofanywa mpaka sasa yanaakisi utendaji bora wa TPA.

“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika bandari hii. Tumeona idadi ya shehena inayoingia hivi sasa imeongezeka. Hii nikutokana na ushirikiano mzuri katika ya Tanzania na Benki ya Dunia,” alisema Dkt Diop,” na kuongeza kwamba umuhimu wa bandari hiyo ni mkubwa sana kwa sababu ameelezwa kuwa bandari inahudumia nchi sita zinazoizunguka Tanzania na ambazo hazina bandari.

Dkt Diop ameahidi kuendelea kuishawishi Benki ya Dunia kuunga mkono awamu ya pili ya maboresho ya bandari hiyo ambayo yatajikiata kwenye ujenzi wa gati nyingine na eneo la kuegeshea magari.

“Tunaamini maboresho hayo yanaenda kuboresha maisha ya Watanzania ambao watapata kazi katika mnyororo mzima wa thamani, pamoja na kuboresha maisha yao” alisema

Aliongeza kuwa hii ni fursa kwa wawekezaji wakubwa na wadogo ambao watajenga viwanda vya bidhaa mbalimbali vitakavyokuwa na soko la ndani na nje ya nchi.

“Tanzania ina fursa nyingi hususani za kilimo, hivyo basi kupitia maboresho haya ya bandari yatasaidia vijana wengi wa Kitanzania kujiajiri na kuuza mazao yao nje ya nchi kwa kutumia bandari hii, na kupunguza tatizo la ajira nchini”, alisema Dkt Diop.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw Plsduce Mbossa, alisema kuwa ujio wa Benki ya Dunia ni ishara ya wazi ya Tanzania ya kuwa na mahusiano mazuri na washirika mbali mbali wa maendeleo.

Benki ya Dunia walitoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania wa Dola za Marekani milioni 421na Serikali ya Tanzania iliongeza Dola milioni 64 za Marekani kwa ajili ya maboresho katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Maboresho haya yametusaidia kuweza kuteka soko la nchi zinazotuzunguka hasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Burundi, Rwanda na Zambia”, alisema Bw Mbossa.

Maboresho hayo yameifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kupitisha shehena mara mbili ikilinganishwa na hapo awali. Ripoti iliyopatikana inaonyesha kuwa kwa mwaka 2015/2016 bandari ilipitisha tani milioni 14, na mwaka huu ni tani milioni 33.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia kanda ya Africa Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa mwenyeji wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi Bw. David Kihenzile (kushoto) walipo tembelea bandari ya dar es salaam kujionea ufanisi na maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo.