Na Dot Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
MFUMO wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni 397,395 zenye thamani ya Sh40.4 trilioni tangu kuanza kutumika, huku vikundi maalum 27,946 vikinufaika na zabuni zenye thamani ya Sh56 bilioni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema hayo Agosti 20, 2026, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo, Dodoma, akieleza namna mfumo huo ulivyobadilisha utekelezaji wa ununuzi wa umma nchini.
Simba amesema NeST imeongeza uwazi, ushindani, ufanisi na uwajibikaji katika ununuzi wa umma, huku ikirahisisha wazabuni kupata na kuomba zabuni bila kulazimika kusafiri hadi kwenye taasisi nunuzi. Amesema takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kupitia ununuzi wa umma, hivyo sekta hiyo ni chanzo muhimu cha fursa za biashara na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema matumizi ya NeST yameongeza uzingatiaji wa sheria katika michakato ya ununuzi kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26. Aidha, mfumo huo umeepusha uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni na kuokoa takribani Sh27.64 bilioni.
Katika hatua ya kukuza ushiriki wa makundi maalum, Simba amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma inaelekeza taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Amesema hadi sasa vikundi 27,946 kutoka makundi hayo vimesajiliwa kwenye NeST, ambapo vijana ni 13,317, wanawake 13,400, wazee 643 na watu wenye ulemavu 586. Vikundi hivyo vimekwishapata zabuni zenye jumla ya Sh56 bilioni.
“PPRA inalenga kuongeza idadi ya makundi yaliyo tayari kushiriki katika zabuni za umma hadi kufikia takribani 300,000, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,”ameeleza.
Simba amesema mpango huo unalenga kuwapa Watanzania fursa ya kupata ajira na kipato kupitia zabuni za Serikali, hata kwa wale ambao hawana uwezo wa kuanzisha kampuni, lakini wanaweza kuungana na kuunda vikundi. Kwa mujibu wa PPRA, kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh500 milioni.
Mkurugenzi huyo amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma pia imeweka utaratibu wa kuwapa kipaumbele wazabuni na bidhaa zinazozalishwa nchini.
Amesema zabuni zote zenye thamani isiyozidi Sh50 bilioni zimetengwa kwa wazabuni wazawa pekee, huku wazabuni wa ndani wakipewa upendeleo wa hadi asilimia 10 katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa.
Aidha, bidhaa zinazozalishwa nchini zinaweza kupata upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa kutoka nje. NeST umewezesha utekelezaji wa utaratibu huo kidigitali, ikiwemo kuzuia wazabuni wa nje kuomba zabuni zilizotengwa kwa wazawa.
Simba amesema PPRA imeanzisha programu ya simu inayojulikana kama NeST Tenderer, inayopatikana kupitia Play Store na App Store, kwa lengo la kuwafikishia wananchi fursa za zabuni moja kwa moja kupitia simu janja.
Amesema kupitia programu hiyo, mtumiaji anaweza kujisajili kwenye NeST, kutafuta na kuomba zabuni pamoja na kufuatilia taarifa za malipo.
Akizungumzia mafanikio ya mfumo huo, Simba amesema NeST umetambuliwa ndani na nje ya Tanzania baada ya kushinda tuzo ya Mfumo Bora Zaidi wa Ununuzi wa Umma Barani Afrika mwaka 2024 katika tuzo za African Association for Public Administration and Management (AAPAM) zilizofanyika Kampala, Uganda.
Amesema mwaka huu, 2026, mfumo huo umetambuliwa pia miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali Mtandao duniani katika tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026, zilizofanyika Julai 8, 2026, Geneva, Uswisi.
Kutokana na mafanikio hayo, amesema Tanzania imekuwa ikipokea wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Botswana na Sudan, wanaofika kujifunza uzoefu wa Tanzania katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma.


