Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph Abdulkarim amewataka watumishi kuhakikisha kuwa wanakuwa suluhu ya changamoto za wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kwa kusikiliza, kutoa majawabu ya uhakika kwa wakati na kutoa mrejesho kwa wafanyabiashara hao kwa wakati na kuzingatia mkataba wa huduma kwa mteja.
CPA. Abdulkarim ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku moja ambacho kimelenga kujadili utekelezaji wa shughuli za shirika hilo mwaka 2025/2026 na kupitia mipango ya mwaka 2026/2027 ikiwa ni pamoja na kuainisha changamoto za mwaka 2025/2026 na kuweka mkakati wa kutatua changamoto hizo.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea Soko Kuu la Kariakoo na kukubali kulifungua yeye mwenyewe, kilichobaki kwetu ni kufanya kazi kwa ari, maarifa, weledi na kujituma zaidi ili watanzania wenzetu waweze kunufaika na uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Serikali yetu” ameongeza CPA. Abdulkarim.
CPA. Abdulkarim amebainisha kuwa kipaumbele cha shirika ni kutoa huduma bora na uhakika kwa wateja ili kila mtu anayehudumiwa katika shirika hilo anatoka akiwa ameridhika na anakuwa balozi mzuri kwa shirika kutokana na huduma alizopata.
Shirika la Masoko ya Kariakoo limekuwa na utaratibu wa kukutana na watumishi wake kila robo ya mwaka wa fedha kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli za shirika, kujadili changamoto zilizojitokeza kipindi husika na kushirikishana mambo mbalimbali za shirika.


