Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imewataka viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kuacha migogoro ya kiutendaji na badala yake kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao, ikisisitiza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana katika mazingira yenye migogoro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ametoa kauli hiyo Agosti 21, 2026 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 16 wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), akisisitiza kuwa mshikamano, kuheshimiana na kutambua mipaka ya mamlaka ni muhimu katika kuhakikisha Serikali za Mitaa zinatoa huduma bora kwa wananchi.

Prof. Shemdoe amesema kwa uzoefu wake wa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Mkoa umemfundisha kuwa uongozi wenye mafanikio hujengwa kwa ushirikiano badala ya migogoro, huku akiwakumbusha viongozi kutambua kuwa nafasi za uongozi hubadilika lakini mahusiano mema hubaki kuwa muhimu.

“ Nimewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Mkoa,nilijitahidi kuepuka migogoro na viongozi niliokuwa nikifanya nao kazi Kwa sababu niliamini mahali ambapo kuna migogoro hakuna maendeleo, wala hapawi mahali pazuri pa kufanyia kazi,” amesema Prof. Shemdoe.

Amesema viongozi na watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kufanya kazi kwa kuheshimiana, akisisitiza kuwa hakuna sababu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kupambana na Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya.

Prof. Shemdoe amesema uzoefu wake katika uongozi umemfundisha umuhimu wa ushirikiano na kuheshimiana, akieleza kuwa alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hakuwahi kugombana na Mwenyekiti wa Halmashauri, na alipokuwa Katibu Tawala wa Mkoa hakuwahi kupishana lugha na Mkuu wa Mkoa.

Aidha, Prof. Shemdoe amewataka viongozi hao kutumia maarifa, weledi na uzoefu wao katika kuwatumikia wananchi, akieleza kuwa Serikali za Mitaa ziko karibu zaidi na wananchi na hivyo ni kimbilio lao katika kupata huduma mbalimbali.
Amesema wananchi wanapopima mafanikio ya Serikali, kwa kiasi kikubwa huyapima kupitia huduma wanazozipata katika maeneo yao, zikiwemo huduma za afya ya msingi, elimu ya msingi, usafiri na usafirishaji.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuidhinisha na kuleta fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Taasisi za Umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema fedha hizo zinaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kujiingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), Bw. Albert Gabriel Msovela, amemhakikishia Prof. Shemdoe kuwa wajumbe wa taasisi hiyo ni askari wake kiutendaji na kwamba TOA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa Katiba.

Bw. Msovela amesema TOA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza malengo mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Mhe. Waziri, naomba nikuhakikishie kwamba kupitia Mkutano Mkuu huu wa 16 wa Mwaka wa TOA, tutatoka na mikakati, maazimio pamoja na mipango madhubuti ambayo tutakwenda kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wake kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Bw. Msovela.

Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa TOA uliowakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Makatibu Tawala wa Wilaya, umefanyika chini ya Kaulimbiu isemayo: “Ugatuzi wa Madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo Madhubuti ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”