Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Wawakilishi 16 wa mashirika ya kiraia kutoka nchi tisa za Afrika wameimarisha uwezo wao wa kuandaa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji yanayolenga kufanikisha Lengo la Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (Land Degradation Neutrality – LDN), kufuatia mafunzo ya kikanda yaliyofanyika kwa siku tatu jijini Nairobi, Kenya.
Mafunzo hayo yalifanyika Karen Country Club Juni 26 hadi 28, 2026, yakiandaliwa chini ya mradi wa Kuimarisha Nafasi ya Mashirika ya Kiraia katika Kufanikisha Lengo la Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (CS4LDN).
Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (Global Environment Facility – GEF), ukitekelezwa na Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mazingira (International Union for Conservation of Nature – IUCN), kwa ushirikiano wa Drynet na Both ENDS.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha washiriki kutoka Burkina Faso, Cameroon, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mali, Senegal, Sudan Kusini, Tanzania na Zambia, yakionesha dhamira ya pamoja ya kikanda ya kuimarisha uongozi wa mashirika ya kiraia katika usimamizi endelevu wa ardhi, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na mapambano dhidi ya uharibifu wa ardhi.
Lengo kuu la mafunzo hayo lilikuwa ni -kuyapatia mashirika ya kiraia na wadau wengine ujuzi wa vitendo wa kuandaa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji yenye ubora, yanayotekelezeka kifedha na yanayoweza kuvutia ufadhili kwa ajili ya mipango ya kufanikisha LDN.
Aidha, mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo wa washiriki kutambua fursa za ufadhili, kushirikiana na wafadhili watarajiwa na kusimamia rasilimali za kifedha kwa ufanisi ili kusaidia urejeshaji endelevu wa ardhi.
Katika kipindi chote cha siku tatu, washiriki walishiriki katika vipindi vya mafunzo shirikishi ya vitendo yaliyojikita katika vipengele muhimu vya uandaaji wa mipango ya biashara na mapendekezo ya uwekezaji.
Vipindi hivyo viliwawezesha kubadilishana uzoefu, kujifunza kutokana na mafanikio na changamoto katika nchi zao, na kujadili mbinu za vitendo za kupata rasilimali za kifedha kwa ajili ya mipango ya urejeshaji wa ardhi.
Mbinu shirikishi iliyotumika ilihamasisha washiriki kuchangia kikamilifu, kujifunza kutoka kwa wenzao na kuimarisha uelewa kuhusu namna ya kuandaa mapendekezo yanayokidhi vipaumbele vya wafadhili huku yakionesha manufaa ya kimazingira na kijamii yanayoweza kupimika.
Kipaumbele cha mafunzo hayo kilikuwa kushughulikia vikwazo vya kifedha vinavyozuia mashirika ya kiraia kutekeleza mipango yenye manufaa ya urejeshaji wa ardhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za ardhi.
Ingawa mashirika ya kiraia yana nafasi muhimu katika kushirikiana na jamii za maeneo husika, jamii za Watu wa Asili na kukuza uendelevu wa mazingira, ukosefu wa upatikanaji wa kutosha wa rasilimali za kifedha unaweza kupunguza uwezo wao wa kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi yenye mafanikio.
Mafunzo hayo yalijengwa juu ya matokeo ya ripoti ya mradi wa CS4LDN uliobeba kauli mbiu ya Kufungua Fursa za Ufadhili kwa Ajili ya Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi (Unlocking Finance for Land Degradation Neutrality).
Ripoti hiyo inachambua changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha LDN na kupendekeza mbinu shirikishi zaidi za kuimarisha ushirikiano kati ya wafadhili na mashirika ya kiraia.
Ripoti hiyo inapatikana katika lugha za Kihispania, Kifaransa na Kiingereza.
Kupitia majadiliano na mazoezi ya vitendo, washiriki walijadili mbinu bunifu za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa fedha, kuboresha ubora wa mapendekezo ya uwekezaji na kuimarisha ushirikiano na wadau wanaoweza kutoa ufadhili.
Vipindi hivyo pia vilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji, usawa, kuzingatia mahitaji ya kijinsia na kutumia mbinu zinazozingatia mifumo ya ikolojia katika kubuni na kutekeleza mipango ya LDN.
Kanuni hizo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa juhudi za kurejesha ardhi zinaleta manufaa ya kudumu, hususan kwa jamii zinazotegemea ardhi na rasilimali za asili kwa ajili ya maisha na shughuli zao za kiuchumi.
Kufikia mwisho wa mafunzo, washiriki walikuwa wameimarisha uwezo wao wa kuandaa na kuwasilisha mipango ya biashara pamoja na mapendekezo ya uwekezaji yaliyoandaliwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wafadhili.
Pia walipata maarifa na uzoefu wa vitendo ambao wanaweza kuutumia katika nchi zao kuhamasisha rasilimali, kuimarisha utekelezaji wa miradi na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya LDN katika ngazi za kitaifa na kikanda.
Mafunzo hayo yalitoa pia fursa muhimu ya kujenga mitandao ya kikanda, kubadilishana maarifa na kuimarisha ushirikiano kati ya wawakilishi wa mashirika ya kiraia yanayopambana na uharibifu wa ardhi barani Afrika.
Mashirika yaliyoshiriki yamekubaliana kuhakikisha kuwa mashirika mengine ambayo hayakuhudhuria mafunzo hayo nayo yanapata maarifa yaliyopatikana kupitia mfumo wa ushauri na ulezi wa kitaalamu (mentorship).
Kila shirika litachukua jukumu la kusaidia angalau shirika moja au mshiriki mmoja wa malezi hayo na kushirikisha maarifa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Ushirikiano huo unaweza kusaidia mashirika kutambua changamoto zinazofanana, kujenga ushirikiano wa kimkakati na kuendeleza mbinu zilizoratibiwa vizuri zaidi za usimamizi endelevu wa ardhi.
Mradi wa CS4LDN unalenga kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia duniani kote ili yaweze kushawishi na kuchangia utekelezaji wa sera na uwekezaji unaolenga kufanikisha LDN.
Ukiungwa mkono na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD) pamoja na Jopo la Mashirika ya Kiraia, mradi huo unaunganisha hatua zinazochukuliwa katika ngazi ya jamii na michakato ya sera na ufadhili katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kwa kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia kuandaa mapendekezo ya uwekezaji yenye ubora na kushirikiana kwa ufanisi na wadau wa ufadhili, mradi unalenga kufungua fursa za kupata rasilimali kwa ajili ya urejeshaji wa ardhi unaozingatia ushirikishwaji na uendelevu.
Mafunzo yaliyofanyika Nairobi yamekuwa hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa mashirika ya kiraia barani Afrika yanakuwa na uwezo mkubwa zaidi, si tu wa kutetea na kuhamasisha utekelezaji wa Lengo la Kutokuwa na Upotevu wa Ardhi, bali pia wa kuhamasisha rasilimali za kifedha zinazohitajika kubadilisha dhamira hizo kuwa matokeo halisi, yanayopimika na yenye manufaa ya kudumu.




