Na Damas Makangale, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, teknolojia ya nyuklia mara nyingi kuhusishwa zaidi na vita na nguvu za uharibifu zinazotokana na silaha za nyuklia.
Mtazamo huu umechangia kuwa na uelewa mdogo wa umma kuhusu uwezo wa teknolojia hiyo katika kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, sayansi na teknolojia ya nyuklia zina matumizi mengi zaidi ya masuala ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, kilimo, maendeleo ya viwanda, utafiti wa kisayansi na uzalishaji wa nishati.
Wakati nchi za Afrika zikichunguza fursa zinazotokana na teknolojia ya nyuklia na rasilimali za urani, wataalamu wanasema kuwa kuongeza uelewa wa umma, uwekezaji katika elimu na maendeleo ya ujuzi ni mambo muhimu katika kuhakikisha bara la Afrika linanufaika kikamilifu na teknolojia hiyo.
Masuala hayo yalijadiliwa kwa kina katika Jukwaa la Wanawake wa Urusi na Afrika kuhusu Nyuklia la mwaka 2026 (Russia–Africa Women’s Nuclear Forum 2026), lililofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita, likiwa na kaulimbiu isemayo “Mazungumzo ya Mabara: Nishati ya Nyuklia kwa Mustakabali wa Baadaye.”
Jukwaa hilo liliandaliwa na Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Tanzania (WiN Tanzania) kwa kushirikiana na Chama cha Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Urusi (Association of Women in Nuclear Russia), kwa msaada wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), WiN Afrika, Shirika la Rosatom, Baraza la Jukwaa la Wanawake la Eurasia na Baraza la Kimataifa la Kusaidia na Kuendeleza Wanawake katika Viwanda na Teknolojia (ICWITI).
Washiriki kutoka Tanzania, Urusi, Misri, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia na Afrika Kusini walijadili fursa za kuendeleza sayansi na teknolojia ya nyuklia huku wakihamasisha ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo.
Kwa Tanzania, mojawapo ya vipaumbele ni kuimarisha uelewa wa umma na kuandaa wataalamu wenye ujuzi kupitia elimu, hususan kwa kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi kuanzia shule za msingi na sekondari hadi vyuo vikuu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC ambaye pia ni Rais wa WiN Tanzania, Profesa Najat Mohammed, anasema Tanzania inaendelea kujenga mazingira ya kitaaluma yanayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika sayansi ya nyuklia, nishati, tiba na teknolojia.
“Tunaimarisha mahusiano ya kitaaluma, tunaongeza uelewa kuhusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika huduma za afya, kilimo, viwanda na utafiti wa kisayansi, na tunafanya kazi ili kuwapa wanawake fursa zaidi za kushiriki katika maeneo haya,” anasema.

Profesa Mohammed anasisitiza kuwa maandalizi ya wasichana kwa ajili ya kazi katika sayansi na teknolojia ya nyuklia yanapaswa kuanza mapema katika elimu yao.
Anasema msingi imara katika masomo ya sayansi utawasaidia kupata maarifa na ujuzi unaohitajika ili kushiriki katika sekta hiyo.
“Ikiwa tunataka kuona wanawake wengi zaidi wakifanya kazi katika nishati ya nyuklia, uhandisi na sayansi ndani ya miaka kumi au kumi na tano ijayo, lazima tuanze kuwaunga mkono kabla hawajaingia katika soko la ajira. Lazima tuanze wakiwa shuleni,” alisema.
Alibainisha kuwa licha ya wanawake kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Tanzania, uwakilishi wao katika taaluma za uhandisi na teknolojia bado ni mdogo.
Profesa Mohammed anasema mojawapo ya dhamira kuu za WiN Tanzania ni kuwaonyesha wasichana kuwa sayansi, hisabati, teknolojia ya nyuklia na uhandisi vinaweza kuwapa fursa muhimu za kitaaluma.
Alitaja Mpango wa Ziada wa Scholarship ya Samia (Samia Scholarship Extended Programme), unaotekelezwa kwa ushiriki wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAEC, kuwa nyenzo muhimu katika kukuza rasilimali watu wa nchi katika sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Kwa mujibu wa Profesa Mohammed, mpango huo huwapa wanafunzi wenye vipaji nchini Tanzania fursa ya kusoma sayansi na teknolojia ya nyuklia katika vyuo vikuu vya kimataifa kabla ya kutumia maarifa na ujuzi wanaopata kuchangia maendeleo ya taifa.
Alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za nchi za kuandaa kizazi kipya cha wataalamu huku ikihakikisha wasichana na wanawake vijana wanapata fursa sawa za elimu.
“Hadi sasa, wanufaika 11 wamepatiwa ufadhili wa masomo katika fani za nishati ya nyuklia, fizikia ya tiba na tiba ya nyuklia,” alisema.
“Katika hao, wanafunzi wanne ni wanawake wanaosoma fizikia ya tiba, tiba ya nyuklia na uhandisi wa nyuklia. Tunawahamasisha wasichana wengi zaidi kuomba nafasi katika awamu inayofuata ya ufadhili,” anaongeza.
Profesa Mohammed anasema wawakilishi wa WiN Tanzania wameanza kutembelea shule za sekondari ili kuwafahamisha wasichana kuhusu fursa za elimu na ajira katika sayansi ya nyuklia.
Anasema wanafunzi kutoka shule za sekondari za Jangwani na Chang’ombe pia wameshiriki katika shughuli zilizoandaliwa na mtandao huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuhamasisha shauku ya kusoma sayansi kunapaswa kwenda sambamba na kuwapatia wanawake vijana fursa za vitendo za kukuza ujuzi wao.
Fursa hizo ni pamoja na kukutana na wanawake wanasayansi na wahandisi, kupata nafasi za kutumia maabara, kushiriki katika mafunzo ya vitendo na kujifunza kuhusu teknolojia za kisasa zinazotumika katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu, alisema hatua zinazofuata zinapaswa kujumuisha miradi ya utafiti, programu za ushauri na uelekezaji wa kitaaluma, mafunzo kwa vitendo kazini na ushirikiano na taasisi za viwanda.
TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KAMA NYENZO YA MAENDELEO
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia wa wizara hiyo, Dkt Harun Makandi, alisema teknolojia ya nyuklia inatoa fursa kubwa za kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazolikabili bara la Afrika.
Aliwataka wadau kutambua sayansi na teknolojia ya nyuklia kama nyenzo za maendeleo ya taifa badala ya kuzihusisha pekee na matumizi ya kijeshi au hatari zinazodhaniwa kuambatana nazo.
“Wakati umefika kwa wanasayansi, watunga sera, wahandisi wa nyuklia na washirika wa kimataifa wa maendeleo kubadilishana maarifa, mbinu bora na uzoefu ili kuendeleza teknolojia ya nyuklia na matumizi yake barani Afrika,” alisema Dkt Makandi.
Kauli yake ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, wanasayansi, taasisi za elimu na washirika wa maendeleo katika kupanua matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia barani Afrika.

UGANDA YAANGAZIA MCHANGO WA WANAWAKE
Kwa upande wake, Rais wa Wanawake katika Nyuklia Uganda na mtaalamu katika Baraza la Nguvu za Atomiki la Uganda, Ruth Asaba, alisema wanawake wanatoa mchango muhimu katika programu za nyuklia nchini humo.
Anabainisha kuwa sayansi na teknolojia ya nyuklia vina matumizi katika tiba, elimu na utafiti, huku vikiwa na uwezo wa kuchangia maendeleo mapana ya kijamii na kiuchumi nchini Uganda.
“Uganda inatambua uwezo wa sayansi na teknolojia ya nyuklia katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa na kutatua changamoto katika kila sekta inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida, kuanzia maeneo ya mijini hadi vijijini,” anasema.
Asaba alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa wasichana na wanawake vijana ili kuandaa kizazi kijacho cha wahandisi na wanasayansi wa nyuklia watakaoweza kuchangia ustawi wa Afrika.
Anasema wanawake nchini Uganda wana jukumu muhimu katika kujenga mustakabali wa teknolojia ya nyuklia ulio salama, jumuishi na endelevu.
“Wanawake nchini Uganda wanazidi kushika majukumu muhimu ya kitaalamu na uongozi katika sekta ya nyuklia, huku wakifungua njia kwa wanawake wengi zaidi kujiunga na sekta hiyo,” alisema.
Asaba aliongeza kuwa jukwaa hilo ni hatua muhimu katika kuunga mkono azma ya Afrika ya kukuza viwanda na kutatua changamoto zinazohusiana na ajira, huduma za afya, miundombinu na kilimo.
Rais wa Women in Nuclear Afrika Kusini (WiNSA), Bi Noxolo Kunene, alitoa wito wa kuongeza uwekezaji katika kukuza vipaji na kuhakikisha kuwa watu wanaopata ujuzi wa kitaaluma wanapewa fursa za kuutumia.
“Moja ya changamoto kubwa katika maendeleo si vipaji tunavyoshindwa kuviendeleza pekee, bali pia ni vipaji tunavyovikuza na baadaye kushindwa kuvitumia,” alisema.
Kunene anasema wahandisi, wataalamu wa teknolojia, watunga sera na waelimishaji wana wajibu wa kuwaandaa watoto kwa ajili ya kazi za baadaye katika sayansi na teknolojia ya nyuklia kupitia elimu bora, mwongozo na nidhamu.
Alisisitiza pia umuhimu wa nishati katika kukuza viwanda, akibainisha kuwa upatikanaji wa nishati ya uhakika unaweza kuimarisha uwezo wa uzalishaji na kusaidia kubadilisha fursa za kiuchumi kuwa manufaa halisi ya maendeleo.

USHIRIKIANO KATI YA URUSI NA AFRIKA
Awali, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, anasema kuimarisha ushirikiano kati ya Urusi na nchi za Afrika ni muhimu katika kuendeleza sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Anasema kubadilishana utaalamu, uzoefu na maarifa kati ya wanasayansi wa Urusi na Afrika kunaweza kusaidia kupanua matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika huduma za afya, kilimo na sekta nyingine muhimu za maendeleo.
Jukwaa hilo liliwakutanisha wawakilishi kutoka nchi nane—Tanzania, Urusi, Misri, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia na Afrika Kusini—kwa ajili ya kubadilishana maarifa, kuimarisha mitandao ya kitaaluma na kutafuta fursa za ushirikiano.
Mbali na kuhamasisha matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia, mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa kujenga utaalamu wa ndani, kupanua fursa za elimu na kuongeza uwakilishi wa wanawake katika taaluma za sayansi na teknolojia.
Majadiliano hayo yalisisitiza kuwa uwezo wa Afrika kunufaika na sayansi na teknolojia ya nyuklia hautategemea maendeleo ya kiteknolojia na ushirikiano wa kimataifa pekee, bali pia uelewa wa umma, uwekezaji katika rasilimali watu na ushiriki wa wanawake katika kuamua mustakabali wa kisayansi na viwanda wa bara la Afrika.


