Na Dennisi Luambano, JamhuriMedia, Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kutoa adhabu kali kwa wanaoingiza dawa bandia, duni na zisizosajiliwa na iendelee kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
Kauli hiyo ameitoa mjini hapa Agosti 20, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha TMDA na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Amesema wanaoziingiza na wanaowasaidia wanakosa huruma na uzalendo kutokana na madhara ya dawa hizo kwa binadamu na mifugo kwa sababu suala la afya ni moja ya vipaumbele vya serikali na limeainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050).
Amesema taarifa sahihi kuhusu bidhaa za tiba ni muhimu kwa sababu sekta hiyo inahusisha moja kwa moja afya na mustakabali wa jamii na wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili waweze kufanya uamuzi salama kuhusu matumizi ya dawa na vifaa tiba.
Vilevile amesema TMDA ina jukumu muhimu la kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyowafikia wananchi vinakuwa na ubora, usalama na ufanisi na utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari.
Pia ameshauri ufanyike utafiti zaidi kuhusu matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali.
“Dawa za asili zina mchango mkubwa katika tiba na nchi nyingi kwa sasa wanazitumia, amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Dk. Yonah Mwalwisi, amesema wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, inayowawezesha kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Pia amesema TMDA imejenga utamaduni wa kukutana na wahariri na waandishi wa habari kila mwaka kwa ajili ya kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuboresha udhibiti wa bidhaa za tiba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma wanazozitoa.
Amesema utafiti wa kuridhika kwa wananchi na wateja uliofanywa Desemba, 2022 na Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) katika halmashauri 35 za mikoa 16, umeonyesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu TMDA kutoka asilimia 47 mwaka 2020 huku kiwango cha kuridhika na huduma zake kikiwa asilimia 82.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari vinavyofikisha elimu kwa wananchi ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba na kuwaelimisha kuhusu hatari za dawa bandia, duni na zisizosajiliwa.
Kuhusu mafanikio, amesema wanatambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni mamlaka iliyofikia ngazi ya tatu ya ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa bidhaa za tiba na wanaendelea na juhudi za kufikia ngazi ya nne; ya juu zaidi na kuendelea kuwa miongoni mwa mamlaka zinazoongoza Afrika.
Pia amesema wameimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa na chanjo baada ya kuingia sokoni kwa kuongeza vituo hadi kufikia 33 huku mtandao wa maabara hamishika ukiongezeka kutoka 19 hadi 28.
Naye Meneja wa Huduma za Sheria wa TMDA, Martha Malle, amesema wanakusudia kufanya maboresho ya sheria ili kuongeza adhabu kwa wanaopatikana na dawa bandia, duni na zisizosajiliwa.
Kwa kushirikiana na vyombo vya dola, amesema wameendelea kudhibiti dawa bandia, duni na zisizojasajiliwa huku baadhi ya watuhumiwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.







