WATU 30 wamekufa baada ya mlima wa taka kuporomoka katika dampo kubwa zaidi mjini Conakry, Guinea. Mvua kubwa ilisomba taka na kufukia nyumba zilizokuwa karibu.

Serikali imesema mvua kubwa iliyoanza kunyesha mwendo wa saa mbili usiku ilisomba taka katika dampo la Dar Es Salam na kusababisha maporomoko yaliyofukia nyumba za muda zilizokuwa karibu.

Watu sita wamejeruhiwa vibaya na nyumba kadhaa zimeharibiwa. Vikosi vya uokoaji vinaendelea kutafuta manusura wanaoweza kuwa wamefukiwa chini ya taka.

Dampo hilo la wazi, ambalo ni kubwa zaidi mjini Conakry, lilikuwa limepangwa kufungwa Jumapili, siku hiyohiyo ambayo maafa hayo yalitokea.

Mamlaka zinasema wakazi wa maeneo yanayozunguka dampo hilo walikuwa wamepewa maagizo ya kuondoka. Wengi wao walikuwa wamehama, lakini baadhi walikuwa bado wanaishi eneo hilo wakati wa maporomoko.

Waziri wa Utawala wa Maeneo na Ugatuzi, Dienabou Touré, amesema serikali itahakikisha familia zote zilizosalia zinahamishiwa katika maeneo mengine.