NA EMMANUEL MBATILO, PWANI
SERIKALI iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kitaifa wa huduma za magari ya wagonjwa (ambulance), utakaoboresha uratibu wa huduma hizo, ufuatiliaji wa magari na kuziunganisha na namba ya dharura 115, inayopigwa bila malipo.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema mfumo huo utakapokamilika utawezesha wananchi wanaopata dharura za kiafya kupata msaada kwa wakati, kwa usalama na kwa uratibu mzuri, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza na kutunza magari ya wagonjwa nchini.
Mchengerwa ameyasema hayo leo Agosti 24, 2026 Mlandizi mkoani Pwani wakati akikabidhi gari la wagonjwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, ambalo litatumika katika Kituo cha Afya Magindu kwa ajili ya kuimarisha huduma za dharura na rufaa.
Amesema Serikali haitaki mafanikio ya huduma za ambulance yapimwe kwa idadi ya magari yanayokabidhiwa pekee, bali kwa uwezo wa magari hayo kuwa tayari muda wote, kuwafikia wagonjwa kwa wakati na kuokoa maisha.
Amesema mfumo huo utahusisha vituo vya kupokea na kuratibu huduma za dharura pamoja na mifumo ya kufuatilia magari, hatua itakayosaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wakati wanapohitaji msaada wa haraka.





