Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo kuhusu msimu wa mvua za Vuli 2026, ambao unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño. Kwa mujibu wa TMA, mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
TMA imeeleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba 2026, na baadaye kusambaa katika maeneo mengine. Ingawa kwa kawaida msimu wa Vuli huisha Desemba, mwaka huu mvua za nje ya msimu zinaweza kuendelea hadi Januari 2027, huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Novemba.
Katika kukabiliana na ongezeko la mvua hizo Serikali inapaswa kujiandaa mapema, si kusubiri mafuriko yatokee. Kwa kuzingatia taarifa rasmi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ya Agosti 2026, mvua za Vuli 2026 zinatarajiwa kuwa wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali, huku El Niño ikitarajiwa kuathiri msimu huo.
TMA imetahadharisha pia kuhusu uwezekano wa mafuriko, kuongezeka kwa kina cha mito na mabwawa, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu.
Hivyo katika kuzingatia taarifa hivyo ni vyema Serikali ikayapa kipaumbele masuala kama kusafisha na kuboresha mifumo ya maji kwa kushirikiana na wananchi hasa kwenye maeneo ambayo kwa kipindi cha mvua yamekuwa korofi.
Hata hivyo Serikali za mitaa zinapaswa kuhakikisha mifereji ya maji, mitaro na njia za kupitisha maji inasafishwa na kuboreshwa kabla ya mvua kubwa kuanza. Maeneo yanayojulikana kuwa hatarishi kwa mafuriko yawekwe kwenye ramani na hatua zichukuliwe mapema. TMA yenyewe imeshauri kuboresha mifumo ya mifereji ili kupunguza madhara ya mafuriko.

Pia kuimarisha mfumo wa tahadhari za mapema kwani taarifa za TMA zisitolewe tu kama taarifa za kawaida, bali zifike kwa wananchi kwa wakati kupitia redio, televisheni, simu, mitandao ya kijamii, viongozi wa mitaa na vijiji. TMA imeeleza umuhimu wa kutumia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari za hali mbaya ya hewa katika kufanya maamuzi.
Pia ni vyema Serikali ikaandaa mpango wa kukabiliana na mafuriko kwani Serikali za mikoa, wilaya, kata na vijiji/mitaa zinapaswa kuwa na mipango ya dharura inayoeleza watu watahamishwaje, wapelekwe wapi, nani ataratibu uokoaji na huduma zipi zitolewe. TMA imesisitiza kuimarishwa kwa kamati za maafa katika ngazi mbalimbali.
Jambo lingine ni kuandaa vifaa vya uokoaji mapema, vifaa kama boti, vifaa vya kuokoa watu, magari yanayoweza kufika maeneo yenye mafuriko, vifaa vya huduma ya kwanza, mawasiliano ya dharura na maeneo ya hifadhi ya muda vinapaswa kutayarishwa kabla ya hali kuwa mbaya.
Kulinda barabara, madaraja na reli ni kati ya ajenda ambazo Serikali inapaswa kufanya ukaguzi wa madaraja, makaravati, barabara na reli, hasa maeneo ambayo tayari yanajulikana kuathiriwa na maji ili kuhakikisha huduma za usafirishaji zinaendelea. TMA imeonya kuwa mvua kubwa zinaweza kusababisha mmomonyoko, kuharibika kwa kingo za barabara na uharibifu wa madaraja na reli.
Kwa upande wa sekta ya afya Serikali ijiandae vituo vya afya ambavyo vinapaswa kuwa na akiba ya kutosha ya dawa, vifaa tiba na mipango ya kuendelea kutoa huduma endapo barabara au miundombinu itaharibiwa. Serikali pia inapaswa kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayoweza kuongezeka baada ya mafuriko na maji machafu.
Pia jambo lingine la msingi ambalo Serikali inapaswa kujiandaa ni kulinda usalama wa chakula, Wizara na mamlaka za kilimo zinapaswa kuwasaidia wakulima kutumia taarifa za hali ya hewa kupanga upandaji na uvunaji, pamoja na kuzuia maji kutuama mashambani. Pia ni muhimu kujiandaa dhidi ya upotevu wa mazao na magonjwa yanayoweza kuongezeka kutokana na unyevu mwingi.
Pia Serikali inapaswa kusimamia mito, mabwawa na vyanzo vya maji kwa kuwa TMA imetabiri kuongezeka kwa kina cha maji katika baadhi ya mito na mabwawa, mamlaka zinazohusika zinapaswa kufuatilia viwango vya maji kwa karibu na kuchukua hatua kabla havijafikia kiwango hatari.
Serikali pia ina wajibu wa kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi hivyo Serikali za Mitaa zinapaswa kudhibiti ujenzi katika mabonde, njia za maji na maeneo mengine yanayoweza kuathiriwa na mafuriko. Hili ni muhimu zaidi kuliko kusubiri kujenga upya nyumba na miundombinu baada ya mafuriko.
Kazi nyigine ambayo Serikali inapaswa kujiandaa na kipindi hicho ni kutoa elimu kwa wananchi, wananchi wanapaswa kufundishwa namna ya kutambua tahadhari za mafuriko, sehemu za kukimbilia, namna ya kulinda watoto na wazee, na kwa nini si salama kuvuka mito au barabara zilizojaa maji. TMA imesisitiza kuwa taarifa za hali ya hewa zinapaswa kutumiwa katika kufanya maandalizi ya kisekta, si kusubiri majanga yatokee.
Serikali inapaswa kuhamia kutoka kwenye mfumo wa “kusubiri maafa yatokee ndipo ichukue hatua” kwenda kwenye mfumo wa “kutabiri, kujiandaa na kuzuia madhara kabla hayajatokea.”
Hata hivyo ili kupata matokeo chanya ya jambo hilo kunahitaji ushirikiano wa TMA, Menejimenti ya Maafa, Wizara ya Afya, Kilimo, Maji, Ujenzi, TAMISEMI, vyombo vya usalama, serikali za mitaa na sekta binafsi kwani TMA pia imesisitiza ushirikiano wa sekta na kamati za maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji/mitaa.

